09. Zipitishe kama zilivyokuja


28- Abu ´Umar bin ´Abdil-Barr amesema:

“Tumepokea kwamba Maalik bin Anas, Sufyaan ath-Thawriy, Sufyaan bin ´Uyaynah, al-Awzaa´iy na Ma´mar bin Raashid wamesema kuhusu Hadiyth zinazozungumzia sifa: “Zipitisheni kama zilivyokuja.”

29- Amesema mmoja katika wanachuoni wa al-Madiynah:

“Hakika Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) anayajua mambo ambayo Amewafunza waja Wake. Na anayajua mambo ambayo Hakuwafunza waja Wake. Yule mwenye kutafuta kuyajua mambo ambayo Hakuwafunza waja Wake basi hakuna kitachozidi kwake isipokuwa kuzidi kuwa mbali Naye. Katika hayo ni Qadar.”

30- Sa´iyd bin Jubayr amesema:

“Yale yasiyojulikana na watu wa Badr basi hayo si katika dini.”

31- Abu ´Umar amesema:

“Zile nukuu sahihi zilizopokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au kutoka kwa Masahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) ni elimu ambayo inatakiwa kuabudia kwayo. Yale yaliyozuliwa baada yao na yakawa hayana msingi kuhusu yale yaliyokuja kutoka kwao basi hayo ni Bid´ah na upotevu. Yale yaliyopokelewa kutoka kwao kuhusu majina na sifa za Allaah yanatakiwa kukubaliwa. Kama ambavyo hawakujadili kwayo, basi haitakiwi kwa yeyote kujadili kwayo.”

32- Abu Bakr al-Khallaal amesema: al-Murruudhiy ametukhabarisha:

“Nilimuuliza Abu ´Abdillaah kuhusu Hadiyth zinazozungumzia sifa. Akajibu: “Tunazipitisha kama zilivyokuja.”

33- Amesema: “´Aliy bin ´Iysaa amenikhabarisha kwamba Hanbal amewahadithia na kusema:

“Nilimuuliza Abu ´Abdillaah kuhusu Hadiyth kama:

“Allaah hushuka katika mbingu ya dunia.”

“Hakika nyinyi mtamuona Mola wenu kama mnavyouona mwezi mwandamo.”

“Mpaka pale Atapouweka unyayo Wake juu yake ambapo utasema: “Tosha, tosha.”

Abu ´Abdillaah akasema: “Tunaziamini na tunazisadikisha pasi na namna wala maana. Haturudishi kitu katika hayo. Tunatambua kwamba yale yote yaliyopokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni ya kweli midhali yana isinadi zilizo Swahiyh. Haturudishi neno hata moja kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Allaah (Ta´ala) hasifiwi zaidi kuliko vile alivyojisifu Yeye Mwenyewe au alivyomsifu Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), pasi na kikomo wala mwisho:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖوَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”[1]

Wenye kusifu hawawezi kufikia sifa Zake. Hatuvuki Qur-aan na Hadiyth. Tunasema kama Alivosema, tunamsifu kama Alivyojisifu Mwenyewe na wala hatuvuki hilo. Tunaiamini Qur-aan yote; zile Aayah zilizo wazi na zile Aayah zisizokuwa wazi. Haturudishi chochote katika sifa Zake kwa sababu ya matusi.

[1] 42:11

  • Mhusika: Imaam Muwaffaq-ud-Diyn bin Qudaamah al-Maqdisiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Dhamm-ut-Ta'wiyl, uk. 19-20
  • Imechapishwa: 02/06/2018