09. Yaliyotangulia yanamtosha yule mwenye kutaka haki

Zile Aayah, Hadiyth na maneno ya wanazuoni yaliyotangulia mbele inapata kuwa wazi kwa yule anayetafuta haki ya kwamba kusherehekea usiku wa nusu ya Sha´baan – ni mamoja kusherehekea kwa njia ya mtu kuswali au aina nyingine – na kufanya usiku wake maalum kwa kufunga ni Bid´ah ovu kwa wanazuoni wengi. Ni kitu kisichokuwa na msingi katika Shari´ah takasifu. Bali ni miongoni mwa mambo yaliyozuliwa ndani ya Uislamu baada ya zama za Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum). Inatosha kwa yule anayetafuta haki juu ya maudhui haya na nyinginezo maneno ya Allaah (´Azza wa Jall):

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا

 “Leo wamekata tamaa wale waliokufuru juu ya dini yenu, hivyo basi msiwaogope na niogopeni Mimi. Leo nimekukamilishieni dini yenu na nimekutimizieni neema Yangu na nimekuridhieni Uislamu uwe dini yenu.”[1]

na zile Aayah nyinginezo zilizo na maana kama hiyo.

Vilevile maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Yeyote atakayezua katika amri yetu hii yale yasiyokuwemo basi atarudishiwa.”[2]

na zile Hadiyth nyinginezo zilizo na maana kama hiyo.

Katika “as-Swahiyh” Muslim amepokea kupitia kwa Abu Huryurah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Msiufanye usiku wa ijumaa kuwa maalum kwa kisimamo kati ya nyusiku nyingine na wala msifanye mchana wake kuwa maalum kwa kufunga kati ya michana minigine; isipokuwa iwe kwa funga anayoifunga mmoja wenu.”[3]

Ingelikuwa inafaa kufanya maalum kitu katika ´ibaadah katika usiku wowote basi usiku wa ijumaa ungelikuwa na haki zaidi kuliko nyusiku nyenginezo. Kwa sababu mchana wake ndio mchana bora uliochomozewa na jua kwa dalili ya wazi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wakati ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitahadharisha kuufanya maalum kati ya nyusiku nyinginezo ndipo ikafahamisha kuwa nyusiku nyenginezo zitakuwa na haki zaidi ya kutokufaa kufanya maalum kitu chochote katika ´ibaadah isipokuwa kwa dalili sahihi inayofahamisha juu ya umaalum huo.

[1] 05:03

[2] al-Bukhaariy (2550) na Muslim (1718).

[3] Muslim (1144).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tahdhiyr minal-Bid´ah, uk. 30-31
  • Imechapishwa: 18/01/2022