09. Vitu vyenye kuharibu swawm


Ee muislamu! Tambua mambo yanayofuata ambayo yanaharibu swawm:

1- Kula na kunywa

Ni wajibu kwa muislamu anayefunga swawm ya faradhi ajizuie na kula inapoingia alfajiri. Iwapo atakula au atakunywa baada ya kuingia alfajiri swawm yake inabatilika na hivyo ni wajibu kwake kuilipa siku hiyo. Allaah (Subhaanah) amesema:

وَكُلُوا وَاشْرَبُوا حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الْأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الْأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِۖ ثُمَّ أَتِمُّوا الصِّيَامَ إِلَى اللَّيْلِ

“Kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku. Kisha timizeni swawm mpaka usiku.”[1]

Atayekula na kunywa hali ya kuwa na mashaka kama alfajiri imeingia hailazimu kitu na swawm yake ni sahihi midhali haikuthibiti kuwa amekula au kunywa baada ya alfajiri kuingia. Asli ni kubaki usiku.

Lililo salama imewekwa katika Shari´ah kwa muumini kula na kunywa kabla ya kuingia muda wa mashaka. Anatakiwa afanye hivo pia ili swawm yake iwe kamilifu. Hata hivyo yule atayekula na kunywa hali ya kuwa na mashaka ya kuzama kwa jua amefanya kosa. Huyu anatakiwa kulipa siku hii. Asli ni kubaki mchana. Haijuzu kwa muislamu kukata swawm isipokuwa baada ya kuhakikisha kama jua limezama kweli au awe na dhana yenye nguvu kuwa limezama.

Ambaye atamuona muislamu anakula, anakunywa au anafanya kitu kingine kinachoharibu swawm mchana wa Ramadhaan ni wajibu kwake kumkataza jambo hilo pasi na kujali sawa awe anafanya yaliyotajwa kwa kusahau au kwa kukusudia. Ni uovu kufanya kitu kama hicho mchana wa swawm hata kama mwenye kufanya hivo amepewa udhuru. Mambo yanatakiwa kuwa namna hiyo ili watu wasiwe na ujasiri kufanya mambo aliyoharamisha Allaah mchana wa swawm na kudai kuwa wamefanya hivo kwa kusahau. Ambaye kweli amefanya hivo kwa kusahau haimuwajibikii kulipa siku hiyo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atayesahau hali ya kuwa amefunga akala au akanywa, akamilishe swawm yake. Hakika si mwingine bali ni Allaah ndiye kamlisha na kamnywesha.”[2]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

2- Vitu vilivyo na maana ya kula na kunywa na vimegawanyika sehemu mbili:

Ya kwanza: Kumpiga sindano ya damu mfungaji. Midhali anapata malisho kupitia njia ya damu ilio safi basi ni wajibu kwake kulipa siku hiyo. Ikiwa pamoja na hivyo anapata malisho vilevile kwa nyenzo nyingine basi vitenguzi vimekuwa viwili.

Ya pili: Sindano ya chakula. Sindano kama hiyo inaharibu swawm iwapo mtu atakusudia kufanya hivo. Sindano za kawaida haziharibu swawm.

3- Kutokwa na hedhi au nifasi

Mwanamke aliye na hedhi na nifasi wanatakiwa kuacha kufunga pindi wapo katika hali zao hizo. Haijuzu na wala si sahihi kwao kuswali wala kufunga katika hali zao hizo. Wanalazimika kulipa swawm na si swalah. Imethibiti kuwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) aliulizwa kama mwanamke mwenye hedhi anatakiwa kulipa swawm na swalah. Akajibu: “Tulikuwa tukipata hedhi wakati wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Tulikuwa tukiamrishwa kulipa swawm na si swalah.”[3]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Mwanamke akihisi maumivu ya hedhi kabla ya jua kuzama na akaja kuona hedhi baada ya kuwa jua limeshazama swawm yake ni sahihi. Damu ya hedhi ndio inayoharibu swawm na sio maumivu ya hedhi.

4- Kujitapikisha

Mwenye kutapika kwa kusudi swawm yake inaharibika. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kutapita sio wajibu kwake kulipa. Ambaye kajitapikisha ni wajibu kwake kulipa.”[4]

Ninamuomba Allaah kwa majina Yake mazuri atuwafikishe sisi, nyinyi na waislamu wengine wote katika yale anayoyaridhia, atufanye sote kushikamana na haki, ainusuru dini Yake, ayanyanyue maneno Yake, azitengeneze hali za waislamu wote kila mahali, awape watawala bora na awaongoze katika yale Anayoyaridhia na kila lile ambalo lina manufaa kwa waja na miji. Ninamuomba awasaidie kwa kila kheri, awatengenezee matangamano yao, awafanye kuwa waongofu na waongozaji wema wenye kuzirekebisha hali za wengine, awawafikishe wawaongoze watu kwa Shari´ah ya Allaah na awakinge kutokamana na njama za shaytwaan na fitina zenye kupotosha. Hakika Yeye ni muweza juu ya hilo. Kadhalika ninamuomba Allaah awawafikishe waislamu wote ulimwenguni waweze kuifahamu dini, wawe na msimamo juu yake, kusaidizana katika wema na uchaji Allaah na atusaidie sisi na nyinyi katika yote anayoyaridhia.

Swalah na salaam zimwendee mja na Mtume Wake, Mtume wetu Muhammad, kizazi chake, Maswahabah wake na wenye kuwafuata kwa wema.

[1] 02:187

[2] al-Bukhaariy (1933) na Muslim (1155).

[3] al-Bukhaariy (321) na Muslim (335).

[4] Abu Daawuud (2380), at-Tirmidhiy (720), Ibn Maajah (1676) na Ahmad (10468). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaami´ (6243).