09. Uwajibu wa swalah ya mkusanyiko kwa anayesikia adhaana

Swali 09: Sisi tuko mbali na msikiti wa kijiji. Lakini tunaswali mkusanyiko maeneo ambapo tumepafanya Muswallaa wetu. Je, tunapata dhambi kwa kutoenda kwetu msikitini[1]?

Jibu: Ikiwa mnasikia adhaana kwa sauti ya kawaida isiyokuwa na spika kutokana na ukaribu wake kwenu, basi itakulazimuni kwenda kuswali pamoja nao. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yeyote atakayesikia adhaana na asiitikie basi hana swalah isipokuwa akiwa na udhuru.”[2]

Alikuja bwana mmoja kipofu akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Sina kiongozi wa kuniongoza msikitini. Je, ninayo ruhusa ya kuswali nyumbani kwangu?” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamuuliza: “Je, wasikia wito wa swalah?” Akasema: “Ndio.” Akasema: “Basi imewajibika.”[3]

Kwa hiyo ni lazima kwenu kuswali pamoja na mkusanyiko msikitini mkiwa mnasikia wito na mnaweza kuuendea. Lakini ukiwa mbali nanyi na mnapata uzito wa kuuendea kutokana na umbali wake au kwa sababu mmoja wenu ni mgonjwa, hawezi kutokana na uzee wake na mfano wa hayo, basi hapana vibaya kuswali mahali penu. Allaah (Subhaanah) amesema:

فَاتَّقُوا اللَّـهَ مَا اسْتَطَعْتُمْ

”Mcheni Allaah muwezavyo.” (64:16)

Kwa kumalizia ni kwamba ni lazima kwenu kuswali pamoja na mkusanyiko muda wa kuwa mnasikia wito wa sauti ya kawaida wakati hakuna fujo. Ni lazima kwenu kuharakia. Ama ikiwa ni mbali nanyi kidesturi kiasi cha kwamba inakuwa vigumu kwenu kuuendea na wala hamsikii wito, basi hapana neno kuswali mahali penu na wala hapana vibaya.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (12/66-67).

[2] Ibn Maajah (785).

[3] Muslim (653) na an-Nasaa´iy (850).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam Swalaat-il-Jumu´ah wal-Jamaa´ah, uk. 33-35
  • Imechapishwa: 26/11/2021