09. Ulazima wa kulingania wengine


Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Suala la tatu: Kuilingania.

MAELEZO

Kuilingania – Kwa msemo mwingine ni kwamba haitoshi kwa mtu akafundishika, akatendea kazi kwa nafsi yake na wala halingii kwa Allaah (´Azza wa Jall). Bali ni lazima awalinganie wengine pia ili anufaike yeye mwenyewe na awanufaishe wengine. Jengine ni kwa sababu elimu hii ni amana. Sio milki yako ambayo unaiweka hazina na kuwanyima watu nayo. Watu wanaihitajia. Kilicho cha wajibu kwako ni kufikisha, kubainisha na kuwalingania watu katika kheri. Hii elimu ambayo Allaah amekubebesha sio wakfu yako. Ni wakfu yako na ya wengine pia. Kwa hiyo usiliimbikize kwa nafsi yako na ukawanyima watu kunufaika nayo. Bali ni lazima kuifikisha na ni lazima kuibainisha kwa watu. Amesema (Ta´ala):

وَإِذْ أَخَذَ اللَّـهُ مِيثَاقَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ لَتُبَيِّنُنَّهُ لِلنَّاسِ وَلَا تَكْتُمُونَهُ

“Wakati alipochukua Allaah fungamano la wale waliopewa Kitabu [akawaambia:] “Bila shaka mtakibainisha kwa watu na wala hamtokificha.””[1]

Hii ni ahadi Allaah kaichukua kutoka kwa wanachuoni kwamba wawafikishie watu yale waliyofunzwa na Allaah ili waieneze kheri na wawaondoshe watu kutoka katika giza na kwenda katika nuru. Hii ndio kazi ya Mitume  (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) na wafuasi wao. Amesema (Ta´ala):

قُلْ هَـٰذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّـهِ ۚ عَلَىٰ بَصِيرَةٍ أَنَا وَمَنِ اتَّبَعَنِي ۖ وَسُبْحَانَ اللَّـهِ وَمَا أَنَا مِنَ الْمُشْرِكِينَ

“Sema: “Hii ndio njia yangu: nalingania kwa Allaah, juu ya ujuzi na umaizi – mimi na anayenifuata. Utakasifu ni wa Allaah na mimi si miongoni mwa washirikina.”[2]

Huu ndio mfumo wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wafuasi Wake; elimu, matendo na kulingania kwa Allaah (´Azza wa Jall). Yule ambaye halinganii na ana upeo wa kufanya hivo na ana elimu lakini hata hivyo akaificha, basi atalishwa kaa la kutoka Motoni siku ya Qiyaamah, kama ilivyokuja katika Hadiyth[3].

[1] 03:187

[2] 12:108

[3] Abu Daawuud (3658), at-Tirmidhiy (2649) na Ibn Maajah (261, 266) kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) aliyeeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atakayeulizwa juu ya elimu ambapo akaificha, basi Allaah atamlisha kaa la kutoka Motoni siku ya Qiyaamah.”

Ibn Maajah (265) amepokea kupitia kwa Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) aliyeeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kunyamazia elimu katika yale anayonufaisha Allaah kwayo kuhusu jambo la watu na jambo la dini, basi Allaah siku ya Qiyaamah atamlisha kaa la kutoka Motoni.”

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 26-27
  • Imechapishwa: 24/11/2020