Allaah (Ta´ala) kuwa juu ni katika sifa za kidhati na imegawanyika sehemu mbili:

Ya kwanza: Ujuu wa dhati.

Ya pili: Ujuu wa sifa.

Ujuu wa sifa ina maana ya kwamba hakuna sifa yoyote kamilifu, isipokuwa ujuu na ukamilifu wake unamrudilia Allaah (Ta´ala). Mambo ni namna hivi sawa ikiwa inahusiana na sifa za utukufu na nguvu au sifa nzuri na kubwa.

Ujuu wa dhati ina maana ya kwamba Allaah yuko juu ya vyote kwa dhati Yake. Haya yamethibitishwa na Qur-aan, Sunnah, maafikiano, akili na maumbile.

Ama Qur-aan na Sunanah, kumejaa yote mawili kwa dalili za wazi na za dhahiri juu ya kwamba Allaah (Ta´ala) yuko juu ya viumbe Vyake kwa dhati Yake. Dalili hizi zimetajwa kwa mitazamo mbalimbali. Mara zinatajwa kama ujuu, ungatikaji, kulingana juu ya ´Arshi na kwamba yuko juu mbingu. Ni kama mfano wa maneno Yake (Ta´ala):

وَهُوَ الْعَلِيُّ الْعَظِيمُ

“Na Yeye ndiye Aliye juu, na ndiye Mkuu.”[1]

سَبِّحِ اسْمَ رَبِّكَ الْأَعْلَى

“Sabihi Jina la Mola wako Aliye juu.”[2]

يَخَافُونَ رَبَّهُم مِّن فَوْقِهِمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ

“Wanamuogopa Mola wao Aliye juu yao na wanafanya yale wanayoamrishwa.”[3]

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ

”Mwingi wa rehema amelingana juu ya ´Arshi.”[4]

أَأَمِنتُم مَّن فِي السَّمَاءِ أَن يَخْسِفَ بِكُمُ الْأَرْضَ فَإِذَا هِيَ تَمُورُ أَمْ أَمِنتُم مَّن فِي السَّمَاءِ أَن يُرْسِلَ عَلَيْكُمْ حَاصِبًا ۖ فَسَتَعْلَمُونَ كَيْفَ نَذِيرِ

”Je, mnadhani mko [katika] amani na Aliyeko mbinguni [juu] kwamba Hatokudidimizeni ardhini, tahamaki hiyo inatikisika? Au mnadhani mko [katika] amani na Aliyeko mbinguni [juu] kwamba Hatokutumieni kimbunga [cha mawe], basi mtajua vipi [makali] maonyo Yangu.”[5]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“´Arshi iko juu yake na Allaah yuko juu ya ´Arshi.”[6]

“Hivi kweli hamniamini ilihali mimi naaminiwa na Aliyeko mbinguni? Nateremshiwa Wahy asubuhi na jioni.”[7]

Wakati mwingine ujuu unatajwa kwa kupandishwa na kunyanyuliwa kitu Kwake. Mfano wa hilo ni maneno ya Allaah (Ta´ala):

إِلَيْهِ يَصْعَدُ الْكَلِمُ الطَّيِّبُ وَالْعَمَلُ الصَّالِحُ يَرْفَعُهُ

“Kwake pekee linapanda neno zuri na tendo jema analitukuza.”[8]

تَعْرُجُ الْمَلائِكَةُ وَالرُّوحُ إِلَيْهِ

“Malaika na Roho [Jibrily] wanapanda Kwake katika siku kiasi chake ni miaka elfu khamsini.”[9]

بَلْ رَفَعَهُ اللَّهُ إِلَيْهِ

”Bali Allaah alimnyanyua Kwake.”[10]

Abu Hurayrah ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna mja yeyote muumini anayetoa swadaqah kutoka katika pato zuri – na wala hakuna kinachopanda kwa Allaah isipokuwa kilicho kizuri – isipokuwa Allaah anaiweka kwenye mkono Wake wa kuume na anailea kama anavyolea mmoja wenu kitekli chake ambapo tende inakuwa kama mlima mkubwa.”[11]

Abu Muusa al-Ash´ariy (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah halali na wala haimstahikii Yeye kulala. Anainyanyua mizani kuishusha. Kwake hupanda matendo ya usiku kabla ya matendo ya mchana na matendo ya mchana kabla ya matendo ya usiku. Pazia Yake ni Nuru; lau ataifunua, basi mwanga wa uso Wake ungeliunguza kila akionacho katika viumbe Wake.” [12]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kuna Malaika wanaokujieni asubuhi na Malaika wanaokujieni usiku. Wanakusanyika swalah ya Fajr na swalah ya ´Aswr. Halafu wanapanda Kwake wale waliokuwa kwenu usiku. Halafu anawauliza – ilihali anajua zaidi kuliko wao – “Waja Wangu mmewaacha katika hali gani?” Wanasema: “Tulipofika tumewakuta wakiswali na tulipoenda tumewaacha wanaswali.”[13]

Imepokelewa na Ahmad.

Wakati mwingine ujuu unatajwa kwa kushuka kitu kutoka Kwake. Mfano wa maneno Yake (Ta´ala):

تَنْزِيلٌ مِنْ رَبِّ الْعَالَمِينَ

“Ni uteremsho kutoka kwa Mola wa walimwengu.”[14]

قُلْ نَزَّلَهُ رُوحُ الْقُدُسِ مِنْ رَبِّكَ

“Sema: ”Roho takatifu ameiteremsha kutoka kwa Mola wako kwa haki.”[15]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mola Wetu (Tabaarak wa Ta´ala) huteremka katika mbingu ya karibu na dunia pale kunapobaki theluthi ya mwisho ya usiku na kusema: “Ni nani mwenye kuniomba Nimpe? Ni nani mwenye kuniomba Nimuitikie? Ni nani mwenye kuniomba msamaha Nimsamehe?”[16]

Kuna Aayah na Hadiyth nyenginezo mfano wa hizo zilizopokelewa tele kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu ujuu wa Allaah (Ta´ala) juu ya viumbe Wake. Ni mapokezi tele ambayo yanawajibisha elimu ya kilazima juu ya kwamba ni kweli Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema hivo kuhusu Mola Wake na kwamba Ummah umepokea hilo kutoka kwake.

Kuhusiana na maafikiano, Maswahabah, wale waliowafuata kwa wema na maimamu wa Ahl-us-Sunnah wameafikiana juu ya kwamba Allaah (Ta´ala) yuko juu ya mbingu juu ya ´Arshi Yake. Maneno yao yamejaa hayo. Al-Awzaa´iy amesema:

“Tulikuwa, pindi wanafunzi wa Maswahabah (Taabi´uun) wamejaa, tukisema: “Allaah (Ta´ala Dhikruh) yuko juu ya ´Arshi Yake na tukiamini yale yaliyotajwa na Sunnah juu ya sifa Zake (Jalla wa ´Alaa).””[17]

Haya yamesemwa na al-Awzaa´iy baada ya madhehebu ya Jahm kuenea ambaye alikuwa akikanusha sifa na ujuu wa Allaah. Alisema haya ili watu waweze kujua kuwa mfumo wa Salaf ulikuwa ukitofautiana na wa Jahm.

Hakuna yeyote katika Salaf kamwe ambaye alipatapo kusema kuwa Allaah hayuko juu ya mbingu au kwamba yuko kila sehemu kwa dhati Yake au sehemu zote kwa nisba yake ni sawasawa au kwamba hayuko ndani ya ulimwengu wala nje yake, hakufungamana nayo na wala hakuachana nayo, au kwamba haijuzu kumuashiria. Uhakika wa mambo ni kwamba kiumbe mjuzi zaidi kumtambua alimuashiria katika hajj ya kuaga siku ya ´Arafah kati ya watu chungunzima. Alinyanyua kidole chake kukielekeza mbinguni na akasema:

“Ee Allaah! Shuhudia!”[18]

Anamuomba Allaah ashuhudie juu ya kwamba Ummah wake umefikishiwa Ujumbe.

Kuhusu akili, hakika kila akili timamu inafahamisha kwamba ni lazima Allaah awepo juu ya viumbe Wake kwa dhati Yake. Hili ni kutokana na sababu mbili:

Ya kwanza: Ujuu ni sifa ya ukamilifu na Allaah ni lazima asifike na sifa ya ukamilifu kwa njia zote. Hivyo ni lazima ujuu wa Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) uthibitishwe.

Ya pili: Kinyume cha ujuu ni uchini. Uchini ni sifa pungufu na Allaah (Ta´ala) ni mwenye kutakasika na sifa zote zenye mapungufu. Hivyo ni lazima atakasike na uchini na kuthibitisha badala yake, nayo ni ujuu.

Ama kuhusu maumbile, Allaah amewaumba viumbe wote; waarabu na wasiokuwa waarabu mpaka wanyama, kwa maumbile ya kumuamini Allaah na ujuu Wake. Hakuna mja anayemwelekea Mola Wake kwa kumuomba du´aa au ´ibaadah, isipokuwa anahisi ulazima wa kutafuta ujuu. Moyo wake unaelekea mbinguni na wala hauelekei si kuliani wala kushotoni. Hakuna anayepinda katika maumbile haya isipokuwa tu yule aliyezugwa na mashaytwaan na matamanio.

Abul-Ma´aaliy al-Juwayniy alikuwa akisema katika vikao vyake:

“Allaah alikuwepo pasi na kitu na sasa yupo Alipokuwa.”

Kwa haya anachotaka ni kukanusha kulingana kwa Allaah juu ya ´Arshi. Ndipo Abu Ja´faar al-Hamadaaniy akamwambia:

“Achana na ´Arshi. Tueleze kuhusu ulazima ambao tunauhisi mioyoni mwetu: Kila pale ambapo mtu anayemjua Allaah anaposema “Ee Allaah!” anahisi namna ambavyo moyo wake kilazima unatafuta ujuu. Hautafuti kuliani wala kushotoni. Ni vipi tunaweza kuondosha hili kwenye mioyo yetu?”

Abul-Ma´aaliy akaanza kupiga kelele na kupiga kichwa chake na huku akisema:

“al-Hamadaaniy amenichanganya! al-Hamadaaniy amenichanganya!”[19]

Dalili zote hizi tano zinaafikiana juu ya kuthibitisha ujuu wa Allaah (Ta´ala) kwa dhati Yake juu ya viumbe.

Kuhusiana na Aayah:

وَهُوَ اللَّهُ فِي السَّمَاوَاتِ وَفِي الْأَرْضِ يَعْلَمُ سِرَّكُمْ وَجَهْرَكُم

“Naye ndiye Allaah katika mbingu na katika ardhi; Anajua ya siri yenu na ya dhahiri yenu na anajua yale mnayoyachuma.”[20]

na:

وَهُوَ الَّذِي فِي السَّمَاءِ إِلَهٌ وَفِي الْأَرْضِ إِلَهٌ

“Na Yeye ndiye Mungu mbinguni na ardhini[21]“,

hazina maana ya kwamba Allaah yuko ardhini kama ambavyo vilevile yuko mbinguni. Atayefikiria hivi au imepokelewa hilo kutoka kwa yeyote katika Salaf, basi amekosea katika ufikiriaji wake na amesema uongo katika nukuu yake.

Kuhusiana na Aayah ya kwanza, ina maana kwamba Allaah ni mwenye kuabudiwa mbinguni na ardhini. Vyote vilivyomo ndani na juu yake vinamuabudu Yeye. Imesemekana vilevile kuwa maana yake ni kuwa Allaah yuko juu ya mbingu halafu baada ya hapo mtu asimame. Kisha asome:

وَفِي الأَرْضِ يَعْلَمُ سِرَّكُمْ وَجَهرَكُمْ وَيَعْلَمُ مَا تَكْسِبُونَ

”… katika na ardhi; Anajua ya siri yenu na ya dhahiri yenu na anajua yale mnayoyachuma.”

Bi maana Allaah anajua ya siri yenu na ya dhahiri yenu katika ardhi. Ujuu Wake juu ya mbingu haumzuii kujua ya siri yenu na ya dhahiri yenu katika ardhi.

Ama Aayah ya pili, maana yake ni kwamba Allaah ndiye mwenye kuabudiwa mbinguni na ardhini. Uungu Wake umethibiti mbinguni na ardhini japokuwa Yeye yuko juu ya mbingu. Ni kama mtu kusema fulani ni kiongozi Makkah na al-Madiynah. Bi maana uongozi wake umethibiti katika miji yote miwili hata kama yeye Mwenyewe yuko katika mji mmoja wapo. Taabiri hii ni sahihi kilugha na kidesturi na Allaah ndiye anajua zaidi.

[1] 02:255

[2] 87:01

[3] 16:50

[4] 20:05

[5] 67:16-18

[6] Tazama ”Sharh Usuwl-il-I´tiqaad” (3/395/659)) na ”Mukhtaswar-ul-´Uluww” (48) ya al-Albaaniy. Ni Swahiyh kwa mujibu wa adh-Dhahabiy na Ibn-ul-Qayyim. al-Albaaniy amesema kuwa ni nzuri na mnyororo wake unatoka kwa Swahabah.

[7] al-Bukhaariy (4351) na Muslim (1064).

[8] 35:10

[9] 70:04

[10] 04:158

[11] al-Bukhaariy (7430).

[12] Muslim (179), Ibn Maajah (195) na Ahmad (4/405).

[13] al-Bukhaariy (5550) na Muslim (1/439).

[14] 56:80

[15] 16:102

[16] al-Bukhaariy (1145), Muslim (758), Abu Daawuud (4717), at-Tirmidhiy (3729) na wengineo.

[17] Kitaab-ul-Asmaa’ was-Swifaat, uk. 515, cha al-Bayhaqiy. Ibn-ul-Qayyim amesema:

”Imepokelewa na al-Bayhaqiy ikiwa na mlolongo wa wapokezi Swahiyh.” (al-Ijtimaa´, uk. 93)

[18] Muslim (4/41).

[19] Tazama ”Siyar A´laam-in-Nubalaa’” (18/475).

[20] 06:03

[21] 43:84

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyah, uk. 34-37
  • Imechapishwa: 13/01/2020