Allaah (Ta´ala) amesema:

وَعَلَى الَّذِينَ يُطِيقُونَهُ فِدْيَةٌ طَعَامُ مِسْكِينٍ ۖفَمَن تَطَوَّعَ خَيْرًا فَهُوَ خَيْرٌ لَّهُ ۚ وَأَن تَصُومُوا خَيْرٌ لَّكُمْ ۖ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ

“… na kwa wale wanaoiweza lakini kwa tabu watoe fidia kulisha masikini. Na atakayejitolea kwa jema lolote lile basi ni bora kwake. Na mkifunga ni bora kwenu – mkiwa mnajua [namna ilivyo kheri kwenu]!”[1]

Mwanzoni ilikuwa yule anayetaka kufunga anafunga na yule anayetaka kuacha anaacha na badala yake anamlisha maskini kwa kila siku moja. Baada ya hapo Allaah (´Azza wa Jall) akateremsha Aayah ya pili:

شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ ۚ فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ

“Mwezi wa Ramadhaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan ili iwe mwongozo kwa watu na hoja bayana za mwongozo na pambanuo la batili. Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi mpya na afunge.”[2]

Hapo ndipo kufunga kukawa ni wajibu kwa kila mwenye uwezo. Kwa hivyo ile hukumu ya kwanza imefutwa na kwa hivi sasa inawahusu tu wale wazee na wanawake wajawazito na wanyonyeshaji ikiwa wanachelea juu ya nafsi zao au watoto wao. Inajuzu kwa mzee kuacha kufunga na badala yake akawalisha masikini. Hivyo ndivyo alivyofanya Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh)[3].

Inajuzu vilevile kwa mwanamke mjamzito na mnyonyeshaji kuacha kufunga. Ni wajibu kwao kuyalipa masiku hayo na kuwalisha masikini au ni wajibu tu kuyalipa masiku yao au ni wajibu tu kuwalisha masikini? Wanachuoni wana maoni haya matatu. Maoni yaliyo karibu na usahihi ni kwamba ni wajibu kwao kuyalipa masiku yao pindi watapoweza kufunga. Hawahitajii kuwalisha masikini midhali hawachelei juu ya watoto wao. Hapo ndipo itakuwa ni wajibu kulisha na kuyalipa masiku yaliyowapita. Kwa kuwa walikuwa ni wenye uwezo lakini hata hivyo wakaacha kufunga kwa sababu ya kuchelea juu ya watoto wao.

Allaah (Ta´ala) amesema:

فَمَن تَطَوَّعَ خَيْرًا فَهُوَ خَيْرٌ لَّهُ

“Na atakayejitolea kwa jema lolote lile basi ni bora kwake.”[4]

Bi maana kulisha zaidi ya masikini mmoja. Hilo ni bora kwake.

Allaah (Ta´ala) amesema:

وَأَن تَصُومُوا خَيْرٌ لَّكُمْ ۖ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ

Na mkifunga ni bora kwenu – mkiwa mnajua [namna ilivyo kheri kwenu]!”[5]

Allaah ameimalizia Aayah kwa kulenga ya kwamba swawm ni bora kwa wale wenye kuweza katika ile Aayah iliyofutwa.

Halafu msafiri na mgonjwa pia wanaweza kuacha kufunga wakati wa safari na maradhi. Lililo bora kwa msafiri ni kufunga au kuacha kufunga? Wanachuoni wametofautiana juu ya hilo. Baadhi wanaonelea kuwa afunge ikiwa anaweza na wengine wanaonelea aache kufunga hata kama anaweza kufunga. Hata hivyo imechukizwa ikiwa anapata uzito wa kusafiri ilihali amefunga. Ikiwa msafiri anachelea kifo juu ya nafsi yake inakuwa ni haramu kwake kufunga.

[1] 02:184

[2] 02:185

[3] Maalik katika “al-Muwattwa´” (01/307).

[4] 02:184

[5] 02:184

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tafsiyr Aayaat-is-Swiyaam, uk. 16-19
  • Imechapishwa: 02/06/2017