09. Sunnah ni mapokezi ya Mtume wa Allaah

Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Tunaonelea kuwa Sunnah ni mapokezi ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Sunnah inaifasiri Qur-aan na kuiweka wazi Qur-aan.”

MAELEZO

Mapokezi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kinachokusudiwa ni yale maneno, matendo na yale yaliyokubaliwa ambayo yalinukuliwa kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amesema:

“Sunnah inaifasiri Qur-aan na kuiweka wazi Qur-aan.”

Dalili ya hayo ni maneno ya Allaah (Ta´ala):

وَأَنزَلْنَا إِلَيْكَ الذِّكْرَ لِتُبَيِّنَ لِلنَّاسِ مَا نُزِّلَ إِلَيْهِمْ وَلَعَلَّهُمْ يَتَفَكَّرُونَ

“Tumekuteremshia Ukumbusho ili uwabainishie watu yaliyoteremshwa kwao na huenda wakapata kutafakari.”[1]

هُوَ الَّذِي بَعَثَ فِي الْأُمِّيِّينَ رَسُولًا مِّنْهُمْ يَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِهِ وَيُزَكِّيهِمْ وَيُعَلِّمُهُمُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ

”Yeye ndiye aliyepeleka Mtume kwa wasiojua kusoma wala kuandika miongoni mwao anawasomea Aayah Zake na anawatakasa na awafunze Kitabu na Hekima.” [2]

Kitabu ni Qur-aan na hekima ni Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Tanabahini! Hakika mimi nimekuachieni Qur-aan na mfano wake pamoja.”[3]

Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amemuamrisha Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwabainishia watu yale yaliyoteremshwa kwao katika Kitabu. Kwa mfano swalah imeamrishwa kwa jumla na Sunnah ndio ikaja kubainisha idadi yake, wakati wake, faradhi zake, twahara iliyolazimishwa kwayo na mengineyo. Vivyo hivyo kuhusu zakaah.

[1] 16:44

[2] 62:02

[3] Ahmad (04/130) na Abu Daawuud (4604). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”al-Mishkaah” (163).

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Itmaam-ul-Minnah, uk. 83-84
  • Imechapishwa: 18/02/2017