Shaykh-ul-Islaam na Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Sharti ya sita ni kufunika viungo ambavyo havitakiwi kuonekana (´Awrah). Wanachuoni wote wameafikiana juu ya kuharibika kwa swalah ya mwenye kuswali uchi ilihali anaweza kujifunika. Mpaka wa uchi wa mwanaume ni kuanzia kwenye kitovu mpaka kwenye magoti na vivyo hivyo kuhusu mjakazi. Ama mwanamke aliyehuru, mwili wake wote huzingatiwa kuwa ni haramu kuuonesha isipokuwa uso. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

يَا بَنِي آدَمَ خُذُواْ زِينَتَكُمْ عِندَ كُلِّ مَسْجِدٍ

“Enyi wana wa Aadam! Chukueni mapambo yenu [mnapoenda] katika kila msikiti.”[1]

Bi maana katika kila swalah.

MAELEZO

Ni lazima kwa mswaliji kufunika viungo visivyoonekana. ´Awrah ya mwanaume ni kutoka kwenye kitovu mpaka kwenye magoti. Maoni sahihi ni kwamba anatakiwa kufunika sehemu hizo.

Mwanamke mwili wake mzima hautakiwi kuonekana isipokuwa tu uso. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwanamke ni ´Awrah.”[2]

Uso tu ndio anatakiwa kuuonyesha ndani ya swalah ikiwa pale anaposwali hakuna wanaume ambao ni ajinabi kwake. Katika hali hiyo Sunnah ni kuufunua.

Wanachuoni wametofautiana juu ya vitanga vya mikono. Kuna wanachuoni ambao wanaonelea kwamba anatakiwa kuvifunua. Baadhi ya wanachuoni wengine wamewajibisha kuvifunika ndani ya swalah. Lililo salama zaidi ni kuvifunika, kama alivosema mtunzi wa kitabu. Ama mwili wake mwingine uliobaki, kukiwemo nyayo, anatakiwa kuufunika pindi anaposwali. Kukiwa wanaume ambao ni ajinabi kwake anatakiwa kufunika uso wake pia.

Kuhusu mjakazi kuna tofauti kwa wanachuoni. Baadhi ya wanachuonii wamempa hukumu moja kama mwanaume kwa sababu anaweza kununuliwa na kuuzwa. Hivyo wanaona kuwa ´Awrah yake ni kama ´Awrah ya mwanaume. Wanachuoni wengine wanaonelea kuwa ana hukumu moja kama mwanamke muungwana kutokana na ujumla wa dalili. Kwa ajili ya kuepuka tofauti lililo salama zaidi kwake ni kujisitiri kama mwanamke muungwana. Jengine ni kwa sababu ya ueneaji wa dalili:

“Mwanamke ni ´Awrah.”

Kile kitendo cha mnunuzi kumtazama na kujadiliana naye bei hakuna maana ya kwamba hatakiwi kujisiri ndani ya swalah na mbele ya wanaume ajinabi ili wasije kufitinishwa naye. Hili khaswa khaswa kama ni mrembo. Katika hali hii anatakiwa kutilia umuhimu suala la kujisitiri na kujiepusha na sababu zote zinazopelekea katika shari. Ni jambo linalojulikana ya kwamba masuala ya tofauti ni miongoni mwa mambo yenye kutatiza pale ambapo dalili haiko wazi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kiache kile chenye kukutia shaka na ukiendee kile kisichokutia shaka.”[3]

“Yule atakayejiepusha na mambo yenye kutia shaka basi ameitakasa dini na heshima yake.”[4]

Ni mambo yenye kutia shaka. Kwa hiyo lililo salama zaidi kwake pale anaposwali ni yeye kufunika mwili wake mzima kama anavofanya mwanamke muungwana.

[1] 07:31

[2] at-Tirmidhiy (1173), Ibn Hibbaan (5599) na Ibn Khuzaymah (1685). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaami´” (6690).

[3] at-Tirmidhiy (2518), an-Nasaa’iy (5711) na Ahmad (1723). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniykatika ”Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb” (2930).

[4] al-Bukhaariy (52) na Muslim (1599).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ash-Sharh al-Mumtaaz, uk. 81-82
  • Imechapishwa: 30/06/2018