09. Sababu ya tano: mume na mke kuishi kwa wema

Miongoni mwa sababu familia kupata furaha ni kuishi kuwe kwa wema. Amesema (Ta´ala):

وَعَاشِرُوهُنَّ بِالْمَعْرُوفِ

“Ishini nao kwa wema.” 04:19

Hapana shaka kwamba kuishi kwa wema ni sababu miongoni mwa sababu za kupata furaha. Kuishi kwa wema ni jambo linalotakikana kutoka kwa mume na mke na familia nzima. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَعَاشِرُوهُنَّ بِالْمَعْرُوفِ

“Ishini nao kwa wema.”

وَلَهُنَّ مِثْلُ الَّذِي عَلَيْهِنَّ بِالْمَعْرُوفِ

“Nao wake wana haki kama ambayo [wako nayo waume zao] iliyo juu yao kwa mujibu wa Shari´ah.” 02:228

Hii ni miongoni mwa sababu zinazofanya familia kupata furaha. Qurtwubiy (Rahimahu Allaah) amesema alipokuwa akifasiri maneno ya Allaah (Ta´ala):

وَعَاشِرُوهُنَّ بِالْمَعْرُوفِ

“Ishini nao kwa wema.”

“Kwa yale aliyoamrisha Allaah katika kuishi kwa wema. Makusudio ya jambo hili ni kwa waume wengi – ndani yake wanaingia pia wake kama ilivyokuja katika hiyo Aayah nyingine – hayo yanatekelezwa kwa kumpa haki zake mahari na matumizi. Asimkunjie uso pasi na kosa. Anatakiwa vilevile kuwa na maneno ya bashasha, asiwe na maneno makali na magumu na wala asiwadhihirishie kulemea kwa wengine.” “Jaami´-ul-Ahkaam al-Qur-aan” (05/97).

Asimkunjie uso pasi na kosa – Baadhi ya waume na wababa kucheka kwao kunakuwa kwa wengine huko nje. Ukimuona nje ya familia utamsifu. Haishi kucheka na kuwachekesha watu walio pambezoni mwake. Anapoingia nyumbani amegeuka mbaya na hatabasamu usoni mwa mke wala watoto wake. Huku sio katika kuishi kwa wema.

Anatakiwa vilevile kuwa na maneno ya bashasha… – Amzungumzishe mke na awazungumzishe watoto. Baadhi ya watu wanapokuwa nje ya nyumbani ulimi wake hauishi kuzungumza. Kama vile wasiokuwa wasomi wanavyosema:

“Mfalme wa kikao.”

Anapoingia nyumbani anakuwa bubu na anakaribia kutozungumza. Iwapo atazungumza basi anakuwa mkali na mgumu. Huku sio katika kuishi kwa wema. Kitendo hichi kinahakikisha katika familia kukosa furaha. Qurtwubiy amesema:

“Allaah (Subhaanah) ameamrisha kusuhubiana vyema na wanawake pindi wanapoolewa ili hiyo iwe ni sababu ya kudumu baina yao na usuhubiana wao uwe kwa ukamilifu. Hakika kufanya hivo kunafanya nafsi kuwa na umoja na kipongezi cha maisha.” “Jaami´-ul-Ahkaam al-Qur-aan” (05/97).

Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Hakika mimi napenda kumpambania mke wangu kama ninavyopenda yeye ajipambe kwa ajili yangu. Kwa kuwa Allaah (Ta´ala) anasema:

وَلَهُنَّ مِثْلُ الَّذِي عَلَيْهِنَّ بِالْمَعْرُوفِ

“Nao wake wana haki kama ambayo [wako nayo waume zao] iliyo juu yao kwa mujibu wa Shari´ah.” Ibn Abiy Shaybah katika “al-Muswannaf” (05/272), Ibn Abiy Haatim katika “Tafsiyr” (02/2196), at-Twabariy (04/4728) na al-Bayhaqiy (07/295).

Bi maana mwanaume anatakiwa kumpambia mke wake kwa yale yanayoendana na yeye kama ambavyo yeye mwanaume anapenda mke wake ampambie kwa yale yanayoenda na yeye. Majumba yakiishi katika kuishi kwa wema basi furaha itahakikishwa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mbora wenu ni yule ambaye ni mbora kwa familia yake na mimi mbora kwa familia yangu.” ad-Daarimiy (02/2260), at-Tirmidhiy (3895), Ibn Hibbaan (09/4177) na at-Tirmidhiy amesema:

“Nzuri geni Swahiyh”. Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “as-Swahiyhah” (285) na (1174).

Wanaume! Mbora wenu ni yule ambaye ni mbora kwa familia. Ni nani aliyeshuhudia haya? Si mwengine isipokuwa ni Mtume wa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ambaye atakuwa ni mbora kwa familia yake basi atakuwa ni sababu ya kuifanya familia yake kuwa na furaha. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ilihali yeye ndiye Mtume wa Allaah na pia kiongozi wa Ummah, alikuwa ni mpole kwa wakeze. Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiwachekesha wake zake na akiwazungumzisha wakeze hata baada ya ´ishaa. Kadhalika alikuwa akishindana na ´Aaishah. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) anasema:

“Tulishindana [mbio] na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo mimi nikamshinda. Hapo ilikuwa kabla sijanenepa.”

Ndugu wapendwa, tazamaeni! Ni nani ana ngazi ya juu kumshinda? Kipindi hicho Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa na umri wa miaka mingapi? Alikuwa ameshapitisha khamsini. Kwa kuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alihama na ´Aaishah kwenda al-Madiynah ambapo alikuwa ameshapitisha miaka khamsini na tatu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anashindana na mke wake (Radhiya Allaahu ´anhaa). Kumekuja tafsiri ya Hadiyth hii ya kwamba wakati huo alikuwa pamoja na Maswahabah wake safarini na alikuwa vilevile pamoja na ´Aaishah. Akawaambia Maswahabah wake:

“Tangulieni mbele!”

Wakatangulia mbele. Akasema:

“Ee ´Aaishah! Njoo tushindane.”

Ametakasika Allaah! Ni kuishi kuzuri kukubwa kulikoje! Ni furaha kubwa iliyoje! Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yuko pamoja na kundi la Maswahabah wake anawaambia:

“Tangulieni mbele!”

Kwa nini? Ili ashindane na ´Aaishah. Alisema:

“Ee ´Aaishah! Njoo tushindane.”

´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) anasema:

“Nikashindana naye. Hapo ilikuwa kabla sijanenepa.”

Hapo alikuwa bado mdogo. Ni jambo lenye kujulikana kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwingilia ´Aaishah akiwa na umri wa miaka tisa. Anaendelea kueleza (Radhiya Allaahu ´anhaa):

“Wakati mwingine nikashindana naye baada ya kuwa nimeshanepepa. Akanishinda ambapo akasema.” Akasema: “Ee ´Aaishah! Nimekulipa mara ile.”

Imekuja katika upokezi mwingine ya kwamba (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa mara ya pili alikuwa pamoja na Maswahabah katika safari moja hivi ambapo akawaambia Maswahabah wake:

“Tangulieni mbele!”

Halafu akasema:

“Ee ´Aaishah! Njoo tushindane.” Akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Nimenenepa.”

Bi maana nimekuwa mzito na siwezi kushindana. Akamwambia:

“Ee ´Aaishah! Njoo tushindane.”

Anashindana naye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kipindi hicho yuko na umri wa miaka sitini na mfano wa hiyo. Hatukupata sehemu walipolenga. Lakini ni jambo lisilokuwa na shaka kwamba kipindi hicho umri wake ulikuwa umeshasogea mbele kwa kuwa ´Aiashah (Radhiya Allaahu ´anhaa) anasema kwamba alikuwa ameshanenepa ambapo wakashindana na akamshinda na kucheka. Halafu akasema:

“Ee ´Aaishah! Nimekulipa mara ile.” Ahmad (06/264), an-Nasaa´iy (05/8944), Ahmad (06/39), al-Bayhaqiy (10/17) mfano wake. Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “as-Swahiyhah” (131) na ni Swahiyh kwa mujibu wa Abu Daawuud (07/2323).

Hakusahau jambo lile na akamfanya ´Aishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) kufurahi. Huku ndio kuishi kwa wema ambako kunafanya wanandoa kufurahi. Majukumu makubwa aliobeba ya Ummah hayakumshughulisha na kuishi huku kwa wema. Ni uzuri uliyoje mume akamtengea mke na watoto wake siku maalum ambayo anawachezesha!

Baadhi ya waalimu zetu watuwazima kiumri wamewatengea watoto wao siku maalum kwa wiki ambapo anatoka pamoja nao, anacheza nao na anawabeba juu ya mgongo wake. Anafanya haya yote ilihali yuko juu ya zaidi ya miaka sabini. Vilevile anamchezesha mke wake. Hivi ndivyo walivyotueleza watoto wake. Wameyatoa wapi? Wanamuiga Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Ndugu wapendwa! Mfano wa haya hayafanyi familia kuondokewa na ukosaji furaha? Ikiwa familia inajua kuwa baba amewatengea siku maalum ambayo anawafanya kufurahi basi utakuta familia nzima inajiandaa ikisubiri siku hii. Hii ni miongoni mwa sababu kubwa za kupata furaha japokuwa ni kitu tumeghafilika nacho. Baadhi wanafanya ni jambo kubwa na kusema kuwa wameshakuwa wazee, mwalimu, imamu wa msikiti na kadhalika na kuuliza ataanzazaje kuwachezesha watoto wake na kucheza na mke na kushindana naye! Huyu ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anayeyafanya haya. Hii ndio furaha kubwa. Ndugu wapendwa! Mambo haya hayana umri maalum. Baadhi ya watu ukiwaeleza haya wanasema kuwa ni mambo ya vijana na kwamba wao wameshazeeka. Ametakasika Allaah! Huyu ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye umri wake umeshasogea mbele. Lakini hata hivyo hakughafilika na jambo hili.

Kwa hivyo, ndugu wapendwa, tunatakiwa kutoghafilika na jambo hili. Mume, mke na watoto wote wana haja ya kuchangia kupatikana furaha ya familia hata kama umri wao wote watakuwa wameshakuwa watuwazima. Mwanadamu anahitajia furaha. Bali nasema kuwa mtu umri wake ukishakuwa mkubwa ndio anahitajia zaidi sababu za kuleta furaha. Hii ni sababu kubwa. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ameeleza pindi alipokuwa akieleza hali ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anapokuwa nyumbani kwake:

“Alikuwa akiisaidia familia yake. Ukifika wakati wa swalah anatoka kuiendea.”

Allaah ni mkubwa! Huyu ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anapokuwa nyumbani kwake anakuwa mwenye kuihudumikia familia yake. Hili linamfanya mke kufurahi pindi mume anaposimamia jambo la mke wake, kumhudumikia na kumsaidia nyumbani kwake. Hii ni miongoni mwa sababu kubwa familia kuwa na furaha.

  • Mhusika: Shaykh Sulaymaan bin Saliymillaah ar-Ruhayliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Asbaab sa´aadat-il-Usrah, uk. 31-38
  • Imechapishwa: 08/10/2016