09. Njia ya pili: kutendea kazi uliyojifunza

Miongoni mwa njia za kuipata elimu na kuithibitisha ni kuitendea kazi ile elimu. Hakika kutendea kazi elimu ni miongoni mwa njia muhimu sana za kuithibitisha elimu. ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh) anasema:

“Elimu inabaki kwa matendo. Akiitikia [hilo hubaki] vinginevyo inaondoka.”[1]

Ambaye anatendea kazi elimu yake huifikia elimu na huthibiti kwenye nafsi yake. Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) walilitambua hilo kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo walikuwa hawazivuki Aayah kumi kutoka katika Qur-aan mpaka kwanza wajifunze maana, watambue maana yake na watendee kazi yaliyomo ndani yake. Wamesema:

“Tukajifunza elimu na matendo kwa wakati mmoja.”[2]

Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) waliendelea na mwenendo huu baada ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo walikuwa wakiwafunza wanafunzi wao elimu ikiambatana pamoja na matendo. Ni jambo lisilo na shaka kuwa ambaye atajaribu hilo na kufungamanisha elimu pamoja na matendo itabaki kwenye nafsi yake.

[1] Ibn ´Asaakir katika “Dhamm man laa ya´mal bi ´Ilmih” (14)

[2] Ibn Wadhdhwaah katika “Maa jaa´ fiy Bid´ah” (255)

  • Mhusika: Shaykh Sulaymaan bin Saliymillaah ar-Ruhayliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Ilm wa Wasaaailuh wa Thimaaruh
  • Imechapishwa: 22/10/2016