09. Mwenye kuwachukia Salaf ameangamia


Hii ndio Salafiyyah ya kihakika. Hizi ndio sifa za Salaf-us-Swaalih; elimu yenye manufaa na matendo mema. Hizi ndio sifa za Salaf-us-Swaalih. Salaf ni wale waliotangulia.

وَالَّذِينَ جَاؤُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَؤُوفٌ رَّحِيمٌ

“Na waliokuja baada yao wanasema: “Mola Wetu! Tusamehe sisi na ndugu zetu waliotutangulia kwa imani wala usijaalie ndani ya nyoyo zetu chuki kwa walioamini. Mola Wetu! Hakika Wewe ni Mpole na Mwenye kurehemu”.” (59:10)

Yule anayewachukia waliotangulia miongoni mwa Maswahabah katika al-Muhaajiruun na al-Answaar na wale wenye kuwafuata kwa wema, anayewachukia watu hawa Allaah amemkasirikia na kumghadhibikia na matendo yake hayana faida yoyote. Hakuyajenga matendo yake juu ya uongofu. Matendo yanakubali kwa kupatikana masharti mawili:

1- Yafanywe kwa ajili ya Allaah Pekee.

2- Yawe ni yenye kuafikiana na Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amesema (Ta´ala):

بَلَى مَنْ أَسْلَمَ وَجْهَهُ لِلّهِ وَهُوَ مُحْسِنٌ

“Sivyo hivyo! Yeyote anayeelekeza uso wake kwa Allaah naye ni mtenda mema.”

Maneno Yake (Ta´ala):

أَسْلَمَ وَجْهَهُ لِلّهِ

“Yeyote anayeelekeza uso wake kwa Allaah… “

Hii ndio Ikhlaasw. Kwa msemo mwingine mtu ajitenge mbali na shirki na washirikina.

Maneno Yake (Ta´ala):

وَهُوَ مُحْسِنٌ

“Naye ni mtenda mema.”

Bi maana ni mwenye kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa msemo mwingine aache Bid´ah na mambo ya kuzua. Badala yake anatenda kwa mujibu wa Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

بَلَى مَنْ أَسْلَمَ وَجْهَهُ لِلّهِ وَهُوَ مُحْسِنٌ فَلَهُ أَجْرُهُ عِندَ رَبِّهِ وَلاَ خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلاَ هُمْ يَحْزَنُونَ

“Sivyo hivyo! Yeyote anayeelekeza uso wake kwa Allaah naye ni mtenda mema, basi ana malipo yake kwa Mola Wake, wala haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika.” (02:112)