09. Mtume na makhaliyfah wake waliswali ´iyd jangwani

Lililo la ajabu ni kuwa Shaafi´iyyah wameonelea kule Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) siku zote kuswali swalah ya Ijumaa kwenye msikiti mmoja ni dalili ya kutofaa kuswali swalah ya Ijumaa kwenye msikiti zaidi ya mmoja katika mji mmoja, na hawakufanya kule (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) siku zote kuswali swalah za ´Iyd mahali pa uwanja kuwa ni dalili ya kuwa bora zaidi ni kuziswali mahali pa uwanja kuliko msikitini. Kama unavyoona mwenyewe dalili ya mambo haya mawili ni moja. Haya yote yanatilia nguvu yale maoni ya kwanza ambayo yametajwa na Imaam an-Nawawiy (Rahimahu Allaah) na yako kwa wanachuoni wa Shaafi´iyyah. Haya pamoja na kuwa tofauti ilio kati ya hayo mawili ni ya rasmi na sio ya kiutenda kazi katika miji mikubwa kama Dameski, kwa sababu maoni ya pili yameweka wazi kuwa lililo bora zaidi ni kuswali msikitini kwa sharti waswaliji wote wapate nafasi. Tatizo ni kuwa misikiti kama hiyo haipatikani. Katika hali hiyo kauli mbili hizo zinakutana, kama yalivyo maoni ya wanachuoni wengi, ya kwamba lililo bora zaidi ni kuswali mahali pa uwanja. Vilevile Imaam ash-Shaaafi´iy (Rahimahu Allaah) anaonelea kuwa imechukizwa kuswali msikitini ikiwa nafasi ni finyu, kama itakavyokuja huko mbeleni.

Haafidhw Ibn Hajar al-Asqalaaniy amesema chini ya Hadiyth ya kwanza:

“Hiyo imetumiwa kama dalili kuwa imependekezwa kutoka kwenda jangwa katika swalah ya ´Iyd na kwamba hilo ndio bora zaidi kuliko kuswali msikitini, kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) siku zote alikuwa akifanya hivo licha ya fadhila zinazopatikana katika msikiti wake. Imaam ash-Shaafi´iy amesema katika “al-Umm”:

“Tumefikiwa na khabari ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akitoka kwenda mahali pa uwanja Madiynah katika swalah za ´Iyd na kadhalika yakafanywa na waliokuja baada yake. Udhuru uliokuwepo ilikuwa tu pale ambapo kunanyesha mvua au kitu kingine mfano wake. Kitendo hichi kinafanywa na watu wa miji yote isipokuwa tu Makkah.”

Halafu akaashiria kuwa sababu ilikuwa ni kutokana na upana wa msikiti na ufinyu wa sehemu zilizoko nje ya Makkah. Amesema:

“Kama wakazi wa mji wana msikiti ambao watu wote wa mji watapata nafasi humo kwa ajili ya sikukuu, basi naonelea kuwa wasiuache. Hata hivyo ikiwa hakutokuwa nafasi ya kuwatosha, basi imechukizwa kuswali ndani yake na hivyo swalah isikaririwe.”[1]

Kwa msemo mwingine ni kwamba sababu ni yenye kuzungukia ufinyu na upana, na sio kutoka kwenda jangwani. Lengo ni kutaka kuwafanya watu wote wawe kitu kimoja. Ikiwa hili litapatikana msikiti pamoja na ubora wake, itazingatiwa kuwa ni bora zaidi.”[2]

Imaam ash-Shawkaaniy ameliwekea hilo taaliki na kusema (03/248):

“Hapa sababu inakuja kuwa ni “ufinyu na upana” ni jambo tu la kudhania lisilotilia nguvu udhuru wa kutomuigiliza (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutoka kwenda kwenye jangwa baada ya kukiri kuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) siku zote alikuwa akifanya hivo. Ama kutumia hoja kwa kuswaliwa Makkah ya kwamba ndio sababu ya kutotoka kwenda jangwani, hilo linaraddiwa na uwezekano wa ufinyu kwa sehemu za nje ya Makkah, na sio kwa sababu msikiti wake haukukuwa na nafasi.”

Uwezekano huu ambao umetajwa na Imaam ash-Shawkaaniy Imaam ash-Shaaafi´iy yeye mwenyewe ameuashiria, kama ambavyo punde kidogo nimetoka kunukuu kutoka kwa Haafidhw. Imaam ash-Shaafi´iy amesema:

“Nimesema haya kwa sababu hawakuwa na nafasi kubwa katika sehemu za nje ya Makkah.”[3]

Haya yanatilia nguvu maoni ya ash-Shawkaaniy (Rahimahu Allaah) yaliyopo juu.

[1] al-Umm (01/207).

[2] Fath-ul-Baariy (02/450 – Salafiyyah)

[3] al-Umm (01/207).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swalaat-ul-´Iydayn, uk. 23-26
  • Imechapishwa: 13/05/2020