09. Mtazamo wa Karraamiyyah juu ya imani

Kuna Murji-ah ambao wanaonelea kuwa imani ni kule kutamka kwa ulimi tu. Fikira hii wako nayo Karraamiyyah. Kwa mujibu wao mnafiki ni muumini kwa kuwa anatamka shahaadah ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah. ´Aqiydah yao inapingana na Qur-aan. Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema:

إِذَا جَاءَكَ الْمُنَافِقُونَ قَالُوا نَشْهَدُ إِنَّكَ لَرَسُولُ اللَّـهِ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ إِنَّكَ لَرَسُولُهُ وَاللَّـهُ يَشْهَدُ إِنَّ الْمُنَافِقِينَ لَكَاذِبُونَ

“Watakapokujia wanafiki watasema: “Tunashuhudia ya kwamba hakika wewe ni Mtume wa Allaah” na Allaah anajua fika kuwa hakika wewe ni Mtume Wake na Allaah anashuhudia kuwa hakika wanafiki bila shaka ni waongo.” 63:01

Kuna Aayah nyingi zinazowakemea wanafiki na kufichua hali zao na kubainisha ukafiri wao. Vilevile Allaah amesema kuwa wako katika tabaka ya chini kabisa Motoni.

Kuna ambao wanasema kuwa kipote hichi kinaonelea kuwa wanafiki wataingia Peponi kwa kuwa wameshuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah. Lakini Shaykh-ul-Islaam aliwafanyia uadilifu na kubainisha kuwa hata kama wanaonelea kuwa wanafiki ni waumini lakini hata hivyo wanaona kuwa wataingia Motoni[1]. Tatizo ni namna yao mbaya wanavyoelezea maana ya imani, nayo ni kwamba imani ni kule kutamka kwa ulimi peke yake. Wanaporomosha imani na matendo ya kwenye moyo, wanabomoa matendo ya viungo vya mwili. Wanashikamana na I´tiqaad hii mbovu ya kwamba imani ni kule kutamka kwa ulimi peke yake. Hawa pia ni katika Murji-ah waliopindukia. ´Aqiydah yao ni mbovu na wanavutia katika kutenda maasi.

[1] Tazama ”Majmuu´-ul-Fataawaa” (7/475-476).

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qurrat-ul-´Aynayn bi Tawdhwiyh Ma´aaniy ´Aqiydat-ir-Raaziyayn, uk. 18-19
  • Imechapishwa: 09/10/2016