2- Safari. Ni halali kwa msafiri kula katika Ramadhaan. Ni lazima kwake baadaye kulipa. Amesema (Ta´ala):

فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

“Basi atakayekuwa mgonjwa miongoni mwenu au yuko safarini, hivyo basi akamilishe idadi katika siku nyinginezo.”[1]

 فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ

“Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi mpya na afunge.”[2]

Alisema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumwambia aliyemuuliza kuhusu kufunga safarini:

“Ukitaka funga na ukitaka acha kufunga.”[3]

Alitoka kuelekea Makkah akiwa ni mwenye kufunga katika Ramadhaan. Alipokuwa njiani akafungua na akaawaamrisha watu nao wafungue[4].

Ni halali kula katika safari ndefu ambayo ni halali kufupiza swalah[5]. Nayo ni ile safari inayokadiriwa kwa maili arobaini na nane ambapo ni takriban 80 km.

Safari inayomhalalishia mtu kula katika Ramadhaan ni ile safari ambayo ni halali. Kwa msemo mwingine ni kwamba ikiwa ni safari ya maasi au ni safari ambayo mtu anataka kufanya ujanja wa kupata kula, basi haitohalalika kwake kula kwa safari hii.

Msafiri akifunga funga yake itasihi na itatosheleza. Hilo ni kutokana na Hadiyth ya Anas (Radhiya Allaahu ´anh) aliyeeleza:

“Tulikuwa tunasafiri pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Aliyefunga hakumtia dosari ambaye hakufunga wala asiyefunga hakumtia dosari ambaye amefunga.”[6]

Lakini hilo ni kwa sharti kwamba kufunga kusimtie uzito safarini. Kukimtia uzito au kukamdhuru, basi bora juu yake kula kwa ajili ya kutendea kazi ruhusa. Mtume  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwona bwana mmoja katika safari aliyefunga ametengenezewa kivuli kutokana na ukali wa joto na watu wamekusanyika pambizoni mwake. Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Sio katika wema kufunga safarini.”[7]

[1] 02:184

[2] 02:185

[3] al-Bukhaariy (1943).

[4] al-Bukhaariy (1944).

[5] ”al-Mughniy” (03/34).

[6] al-Bukhaariy (1947).

[7] al-Bukhaariy (1946).

  • Mhusika: Nukhbatin minal-´Ulamaa´
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fiqh-ul-Muyassar, uk. 155
  • Imechapishwa: 23/04/2020