09. Mahimizo ya umoja ndani ya matendo ya Maswahabah


Kuhusu matendo ya Salaf kulitokea kati yao (Rahimahumu Allaah) tofauti lakini haikupelekea wakafarikiana, kufanyiana uadui wala kuchukiana. Tofauti ilitokea kati yao kipindi cha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa baina yao. Miongoni mwa hayo ni kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipotoka katika vita vya Ahzaab na akaja Jibriyl akimwamrisha kutoka kwenda kwa Banuu Quraydhwah ili kuvunja mkataba. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawaambia Maswahabah wake:

“Asiswali mmoja ´Aswr isipokuwa kwa Banuu Quraydhwah.”

Wakatoka Madiynah wakielekea Banuu Quraydhwah. Ukawafikia wakati wa swalah ya ´Aswr ambapo baadhi yao wakaona waswali watapofika Banuu Quraydhwah hata kama jua litazama. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Asiswali mmoja ´Aswr isipokuwa kwa Banuu Quraydhwah.”

Wakasema kuwa wanamsikiliza na kumtii.

Wengine wakaona waswali ndani ya wakati wa swalah kwa sababu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikusudia kufanya haraka kutoka na hakukusudia eti tucheleweshe swalah. Hayo yakamfikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) lakini hakumkemea yeyote katika wao na wala hakumkaripia kutokana na yale aliyofahamu. Wao wenyewe walikhitilafiana kwa ajili ya kutofautiana kwa maoni katika kuzifahamu Hadiyth za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sittah, uk. 15
  • Imechapishwa: 21/06/2021