09. Lini inamfaa yule mwenye kulitamka na lini halimfai

Tumetangulia kusema ya kwamba kusema ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah` ni lazima kuambatane na kuelewa maana yake na kutendea kazi yale inayopelekea. Lakini pale ilipokuwa kuna baadhi ya dalili zinaweza kufahamika kuwa inatosha kule kulitamka peke yake na kuna baadhi ya watu ambao wameshikilia uelewa huo, ndipo ikapelekea kuliweka wazi hilo ili kuondosha dhana hiyo kwa yule anayetaka haki. Shaykh Sulaymaan (Rahimahu Allaah) amesema kuhusu Hadiyth ya ´Utbaan ambayo ndani yake mna:

“Hakika Allaah ameharamisha Moto kwa yule mwenye kusema ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah` akikusudia kwa kusema hivo uso wa Allaah.”[1]

Akasema:

“Tambua ya kwamba kumepokelewa Hadiyth ambazo udhahiri wake yule mwenye kutamka shahaadah basi Moto umeharamishwa juu yake. Mfano wa Hadiyth hizo ni kama hii na Hadiyth ya Anas ambaye ameeleza kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Mu´aadh walikuwa juu ya kipando ambapo akasema: “Ee Mu´aadh!” Akasema: “Nakuitikia, ee Mtume wa Allaah!” Halafu akasema: “Hakuna mja anayesema ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah` isipokuwa Allaah anamharamishia Moto.”[2]

Muslim amepokea kupitia kwa ´Ubaadah ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kushuhudia ya kwamba ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni mja na Mtume wa Allaah`, basi Allaah amemharamishia Moto.”[3]

Kumepokelewa vilevile Hadiyth nyinginezo ya kwamba yule atayetamka shahaadah mbili ataingia Peponi na hazikutaja kuwa ameharamishiwa Moto. Miongoni mwazo ni Hadiyth ya Abu Hurayrah ya kwamba walikuwa pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika vita vya Tabuuk na ndani yake inasema kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Hakuna mja atayekutana na Allaah akiwa amesema ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba mimi ni Mtume wa Allaah` hali ya kuwa hana shaka akazuiwa kutokamana na Pepo.”

Ameipokea Muslim.

Maana yake bora iliyosemwa ni yale yaliyosemwa na Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah na wengineo ya kwamba Hadiyth hizi zinahuzu yule mwenye kuisema na akafa juu yake, akaisema akiwa mtakasifu moyoni mwake, akiwa na yakini kwenye moyo wake bila ya mashaka nayo pamoja na ukweli na yakini. Uhakika wa Tawhiyd ni roho kumwelekea Allaah kikamilifu. Mwenye kushuhudia ya kwamba ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah` hali ya kuwa ni mtakasifu moyoni mwake, basi ataingia Peponi. Kwa sababu kumtakasia nia Allaah ni kule kuuelekeza moyo kwa Allaah (Ta´ala) kwa kutubu kutokamana na madhambi tawbah ya kweli. Mtu atapokufa katika hali hiyo atafikia hilo. Kumepokelewa Hadiyth nyingi kabisa ya kwamba atatoka Motoni yule aliyesema ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah` na moyoni mwake kukawa kuna kheri sawa na uzito wa punje ya shayiri, punje ya hardali na chembe ndogo kabisa. Imepokelewa vilevile kwa mapokezi tele kabisa ya kwamba wengi ya ambao wanasema ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah` wataingia Motoni kisha baadaye watatoka humo. Imepokelewa pia mapokezi mengi kabisa kwamba Allaah ameuharamishia Moto kuunguza mahali pa sujudu kwa mwanaadamu. Hawa inahusu wale waliokuwa wakiswali na wakimsujudia Allaah. Kumepokelewa mapokezi tele kabisa pia kwamba Moto umeharamishwa kwa yule mwenye kusema ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah` na yule mwenye kushuhudia kwamba ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah`. Lakini hata hivyo imetajwa hali ya kuwa ni yenye kufungamanishwa kwa vikwazo vigumu. Wengi wanaoitamka hawajui ni nini kumtakasia nia Allaah wala ni nini yakini. Asiyejua hayo kunachelea juu yake asije kutahiniwa wakati wa kufa na akaja kuzuiawa baina yake na yenyewe.

Wengi wanaoitamka kwa kufuata kichwa mchunga na kimazowea imani haijachanganyika na ladha ya moyo. Wengi wanaopewa mtihani wakati wa kufa na ndani ya makaburi ni watu sampuli hii. Imekuja katika Hadiyth:

“Nimesikia watu wakisema kitu na mimi nikakisema.”[4]

Mara nyingi matendo ya watu hawa yanakuwa yamejengwa juu ya kufuata kichwa mchunga na kuwaiga watu mfano wao. Watu hawa wamefanana zaidi na wale ambao Amesema (Ta´ala) juu yao:

إِنَّا وَجَدْنَا آبَاءَنَا عَلَىٰ أُمَّةٍ وَإِنَّا عَلَىٰ آثَارِهِم مُّهْتَدُونَ

“Hakika sisi tumewakuta baba zetu juu ya dini na hakika sisi tunaongoka kwa nyayo zao.” (43:22)

Kwa hiyo hakuna mgongano kati ya Hadiyth hizi. Msingi ni kuwa akiwa ataisema kwa moyo mtakasifu na yakini kamilifu basi atakuwa sio mwenye kuendelea kutenda dhambi. Hakika ikhlaasw na yakini yake kamilifu itamfanya Allaah kuwa ni mwenye kupendwa zaidi kwake kuliko kila kitu. Kwa hiyo moyoni mwake kutakuwa hakuna hamu ya yale aliyoharamisha Allaah wala hatochukia yale Allaah aliyoamrisha. Huyu ndiye aliyeharamishiwa Moto hata kama atakuwa alifanya madhambi kabla ya hapo. Hakika imani, tawbah, ikhlaasw, mapenzi na yakini yake hii haitomwachia dhambi yoyote isipokuwa itaifuta kama jinsi usiku unavyoufunika mchana.”

Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab amesema:

“Wana hoja tata nyingine. Wanasema: “Kwa hakika Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimkemea Usaamah pindi alipomuua mtu aliyesema: “Hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah”. Na akamwambia:

“Hivi kweli umemuua baada ya yeye kusema “Hapana mungu isipokuwa Allaah?”

Amesema vilevile:

“Nimeamrishwa kuwapiga vita watu mpaka watakaposema “Hapana mungu isipokuwa Allaah”.”[5]

Na kuna Hadiyth nyinginezo zinazozungumzia kumsalimisha yule mwenye kuitamka. Makusudio ya hawa wajinga ni kwamba mwenye kuitamka hawezi kukufuru wala kuuliwa, pasi na kujali yale atayoyafanya.

Ndio maana inatakiwa kusemwa kuambiwa washirkina hawa wajinga: “Ni jambo linalojulikana ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwapiga vita mayahudi na akawafanya mateka ilihali na wao wanasema “Hapana mungu isipokuwa Allaah”. Aidha Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) waliwapiga vita Banuu Haniyfah nao wanashuhudia “Hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah”, wanaswali na kudai Uislamu. Hali kadhalika wale aliowaunguza ´Aliy bin Abiy Twaalib kwa moto. Na wajinga hawa wanakubali kuwa yule mwenye kupinga kufufuliwa anakufuru na kuuawa, hata kama atasema “Hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah”, na kwamba yule mwenye kupinga chochote katika nguzo za Uislamu amekufuru na kuuawa, hata ikiwa ataitamka [Shahaadah]. Vipi basi isimfai ikiwa kapinga kitu katika mambo ya matawi, lakini imfae akipinga Tawhiyd ambayo ndio msingi na asli ya dini ya Mitume? Lakini maadui wa Allaah hawakufahamu maana ya Hadiyth hizi.

Ama Hadiyth kuhusu Usaamah, alimuua mtu ambaye alidai Uislamu kwa sababu alidhani ya kwamba anadai Uislamu kwa khofu tu ya kuuliwa na mali yake. Na mtu akidhihirisha Uislamu, basi ni wajibu kumwacha mpaka kubainike yanayokhalifu hilo. Allaah ameteremsha juu ya hilo:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا ضَرَبْتُمْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ فَتَبَيَّنُوا

”Enyi mlioamini! Mnapotoka katika njia ya Allaah basi hakikisheni.” (04:94)

Bi maana “thibitisheni”. Aayah inafahamisha ya kwamba ni wajibu kumsalimisha mpaka mtu athibitishe. Baada ya muda kukibainika kutoka kwake yanayokhalifu Uislamu, anauawa, kutokana na maneno Yake (Ta´ala):

 فَتَبَيَّنُوا

“… basi hakikisheni.”

Na lau ingelikuwa hauawi kabisa akiitamka, basi kuhakikisha kungekuwa hakuna maana yoyote. Vivyo hivyo Hadiyth nyengine na mfano wake. Maana yake ni haya tuliyoyataja; ya kwamba mwenye kudhihirisha Tawhiyd na Uislamu, basi ni wajibu kumsalimisha isipokuwa ikibainika kutoka kwake yanayochengua hilo. Dalili ya hili ni kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyesema:

“Hivi kweli umemuua baada ya yeye kusema “Hapana mungu isipokuwa Allaah?””[6]

Amesema vilevile:

“Nimeamrishwa kuwapiga vita watu mpaka watakaposema “Hapana mungu isipokuwa Allaah.””

ndiye huyohuyo aliyesema kuhusu Khawaarij:

“Popote mtapokutana nao basi waueni”[7],

“Lau nitakutana nao, basi nitawaua kama walivyouawa kina ´Aad”[8],

pamoja na kuwa ni katika watu wenye kufanya ´ibaadah sana, Tahliyl[9] na Tasbiyh[10]. Mpaka hata Maswahabah walikuwa wakizidharau swalah zao wakilinganisha na zao. Pia wamejifunza elimu kutoka kwa Maswahabah, hata hivyo haikuwafaa kitu “Hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah”, wala wingi wa kufanya ´ibaadah wala kudai kwao Uislamu pindi ilipodhihiri kwao kukhalifu kwao Shari´ah. Kadhalika kuhusu tuliyoyataja kupigwa vita mayahudi na Maswahabah kuwapiga vita Banuu Haniyfah.””

Haafidhw Ibn Rajab amesema katika kijitabu chake kinachoitwa “Kalimat-ul-Ikhlaasw”:

“Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Nimeamrishwa kuwapiga vita watu mpaka washuhudie ya kwamba ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah.”

yalimfanya ´Umar na baadhi ya Maswahabah kufahamu kuwa mwenye kutamka shahaadah basi anasalimika na adhabu ya duniani kwa kule kutamka kwake tu na hivyo wao wakawa wamejizuia kuwapiga vita wale waliokataa kutoa zakaah. Lakini [Abu Bakr] as-Swiddiyq yeye akaelewa kuwa kutamka maneno hayo hayamzuii mtu kupigwa vita isipokuwa mpaka ayatekelezee haki yake kwa kuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“…. watapofanya hayo, basi imesalimika kwangu damu na mali yao na hesabu yao iko kwa Allaah.”

Akasema [Abu Bakr as-Swiddiyq]:

“Mali ni haki ya zakaah.”

Hivi alivyofahamu as-Swiddiyq yamepokelewa waziwazi na Maswahabah wengi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ikiwa ni pamoja vilevile na Ibn ´Umar, Anas na wengineo na kwamba amesema:

“Nimeamrishwa kuwapiga vita watu mpaka washuhudie ya kwamba ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah´, wasimamishe swalah, watoe zakaah.””

Haya yanatiliwa nguvu na maneno Yake (Ta´ala):

فَإِن تَابُوا وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَآتَوُا الزَّكَاةَ فَخَلُّوا سَبِيلَهُمْ

“Wakitubu na kusimamisha swalah na kutoa zakah, basi waacheni huru.” (09:05)

فَإِن تَابُوا وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَآتَوُا الزَّكَاةَ فَإِخْوَانُكُمْ فِي الدِّينِ

“Wakitubu na kusimamisha swalah na kutoa zakah, basi ni ndugu zenu katika dini.” (09:11)

ya kwamba udugu wa dini hauthibiti isipokuwa kwa kutekeleza faradhi pamoja na kumwabudu Allaah pekee na kujiepushe na shirki. Malengo hayafikiwi isipokuwa kwa Tawhiyd. Pindi Abu Bakr alipowathibitishia haya Maswahabah hatimaye waliafikiana na maoni yake na wakaona kuwa ndio ya sawa.

Kwa hiyo ikitambulika kuwa adhabu za kidunia haziondoki moja kwa moja kwa yule mwenye kutamka shahaadah, bali uhakika wa mambo ni kuwa yule mwenye kutumia vibaya haki za Uislamu anaadhibiwa, basi vivyo hivyo ndivyo inakuwa kwa adhabu za Aakhirah.”

Amesema vilevile:

“Kuna kundi la wanazuoni waliosema kuwa malengo ya Hadiyth hizi ni kwamba kutamka shahaadah ni sababu inayopelekea kuingia Peponi na kusalimika kutokamana na Moto na kwamba ndivyo inavyopelekea. Lakini malengo hayatofikiwa isipokuwa kwa kukusanyika sharti zake na kutokuwepo vizuizi. Malengo yanaweza kutofikiwa kwa kukosekana moja katika sharti zake au kuwepo kizuizi. Hivi ndivyo alivyosema al-Hasan [al-Baswriy] na Wahb bin Munabbih na ndio yako wazi zaidi.”

Halafu akasimulia kutoka kwa al-Hasan ya kwamba alimwambia al-Farazdaq pindi alipokuwa akimzika mke wake: “Umeiandalia nini siku kama hii ya leo?” Akasema: “Nashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah tangu miaka sabini iliyopita.” Ndipo al-Hasan akamwambia: “Ndio, ni kweli kuwa ni maandalizi. Lakini ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah` ina masharti. Kwa hiyo tahadhari na kuwatuhumu machafu wanawake wenye kujisitiri.”

Kulisemwa kuambiwa al-Hasan kwamba kuna watu wanaosema mwenye kutamka shahaadah ataingia Peponi ambapo akawa amesema: “Mwenye kusema ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah` na akaitekelezea haki yake na faradhi zake, basi ndiye ataingia Peponi.”

Wahb bin Munabbih alisema baada ya kuulizwa: “Je, ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah` si ni ufunguo wa Pepo?” Akasema: “Ndio, ni kweli. Lakini hakuna ufunguo wowote isipokuwa unakuwa na meno. Ukija na ufunguo ulio na meno utafunguliwa. Vinginevyo hutofunguliwa.”

Natumai kuwa kiwango hichi tulichonukuu kutoka katika maneno ya wanazuoni kinatosha katika kuraddi hoja tata hizi zilizoshikiliwa na wale wenye kudhani kwamba mwenye kusema ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah` hakufuru ingawa atafanya yakufanya katika aina mbalimbali za shirki za leo zinazofanywa kwenye makaburi ya watu wema, kitendo ambacho kinachengua na kupingana na neno la Tawhiyd kikamilifu.

Huu ndio mfumo wa wapindaji ambao wanachukua sehemu ya maandiko yaliyo kwa jumla na huku wakidhani kuwa yanawasapoti na wanaacha yale maandiko yaliyopambanuliwa yanayoyabainisha na kuyaweka wazi. Hali yao ni kama ya wale wenye kuamini sehemu katika Qur-aan na wanakanusha sehemu nyingine. Allaah amesema kuhusu sampuli ya watu hawa:

هُوَ الَّذِي أَنزَلَ عَلَيْكَ الْكِتَابَ مِنْهُ آيَاتٌ مُّحْكَمَاتٌ هُنَّ أُمُّ الْكِتَابِ وَأُخَرُ مُتَشَابِهَاتٌ ۖ فَأَمَّا الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِمْ زَيْغٌ فَيَتَّبِعُونَ مَا تَشَابَهَ مِنْهُ ابْتِغَاءَ الْفِتْنَةِ وَابْتِغَاءَ تَأْوِيلِهِ ۗ وَمَا يَعْلَمُ تَأْوِيلَهُ إِلَّا اللَّـهُ ۗ وَالرَّاسِخُونَ فِي الْعِلْمِ يَقُولُونَ آمَنَّا بِهِ كُلٌّ مِّنْ عِندِ رَبِّنَا ۗ وَمَا يَذَّكَّرُ إِلَّا أُولُو الْأَلْبَابِ رَبَّنَا لَا تُزِغْ قُلُوبَنَا بَعْدَ إِذْ هَدَيْتَنَا وَهَبْ لَنَا مِن لَّدُنكَ رَحْمَةً ۚ إِنَّكَ أَنتَ الْوَهَّابُ رَبَّنَا إِنَّكَ جَامِعُ النَّاسِ لِيَوْمٍ لَّا رَيْبَ فِيهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُخْلِفُ الْمِيعَادَ

“Yeye ndiye Aliyeteremsha kwako Kitabu – humo mna Aayah zilizo na maana ya wazi – hizo ndio msingi wa Kitabu – na nyinginezo zisizokuwa wazi maana. Basi wale ambao katika nyoyo zao mna upotevu hufuata zile zisizokuwa wazi maana zake kutafuta fitina na kutafuta kuzipindisha, na hakuna ajuae maana zake isipokuwa Allaah. Ama wale waliobobea katika elimu husema: “Tumeziamini; zote ni kutoka kwa Mola wetu”, na hawakumbuki isipokuwa wale wenye akili. Ee Mola wetu! Usizipotoe nyoyo zetu baada ya kutuongoza na tutunukie kutoka kwako rehema – hakika Wewe ni Mwingi wa kutunuku. Ee Mola wetu! Hakika Wewe utawakusanya watu katika Siku isiyo na shaka ndani yake – hakika Allaah havunji miadi.” (03:07-09)

Ee Allaah! Tunakuomba utuonyeshe haki kuwa ni haki na utuwezeshe kuweza kuifuata na utuonyeshe batili kuwa ni batili na utuwezeshe kuweza kuiepuka.

[1] al-Bukhaariy (415) na Muslim (33).

[2] al-Bukhaariy (128), Muslim (32) na Ahmad (03/261).

[3] Muslim (29), at-Tirmidhiy (2638) na Ahmad (05/318).

[4] al-Bukhaariy (86), Muslim (905) na Ahmad (06/355).

[5] al-Bukhaariy (385), Muslim (133), at-Tirmidhiy (2608) na wengineo.

[6] al-Bukhaariy (4021), Muslim (96) na Ahmad (05/200).

[7] al-Bukhaariy (3611), Muslim (2511), Abu Daawuud (4769) na wengineo.

[8] al-Bukhaariy (3344), Muslim (2499), Abu Daawuud (4766) na wengineo.

[9] Kusema ”Laa ilahaa illa Allaah”.

[10] Kusema: ”Subhaan Allaah”.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ma´naa laa ilaaha illa Allaah, uk. 31-40
  • Imechapishwa: 23/09/2023