09. Kuoga kwa ajili ya kuingia Makkah

21- Kwa ambaye itamsahilikia kuoga kabla ya kuingia Makkah, basi afanye hivo. Vilevile aingie Makkah mchana kwa ajili ya kumuiga Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)[1].

22- Aingie kwa upande wa juu ambako hii leo kuna mlango wa Mu´allaah. Kwa sababu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliingia kupitia nyayo za mlima ulio juu. Unaitwa Kadaa´[2] na imetokezea sehemu ya makaburi. Akaingia msikitini kwa upade wa mlango wa Banuu Shaybah. Hii ndio njia iliyo karibu zaidi na jiwe jeusi.

23- Inafaa kwake yeye kuingia Makkah kupitia upande wowote anaotaka. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Njia zote za Makkah ni njia za kupita na ni sehemu za kuchinja.”

Katika Hadiyth nyingine imekuja:

“Makkah yote ni njia; aingie na hapa na kutoka na hapa.”[3]

24- Utapoingia msikitini, basi usisahau kutanguliza mguu wako wa kulia kwanza[4] na kusema:

اللهم صل على محمد وسلم اللهم افتح لي أبواب رحمتك

“Ee Allaah! Mswalie Muhammad na umpe amani. Ee Allaah! Nifungulie mlango wa rehema Zako.”[5]

au pia anaweza kusema:

أعوذ بالله العظيم وبوجهه الكريم وسلطانه القديم من الشيطان الرجيم

“Najilinda kwa Allaah ambaye ni Mkubwa, kwa uso Wake mtukufu na kwa ufalme Wake wa kale kutokamana na shaytwaan aliyewekwa mbali na rehema.”[6]

25- Atakapoiona Ka´bah basi atanyanyua mikono yake akitaka. Hilo limethibiti kutoka kwa Ibn ´Abbaas[7].

26- Haikuthibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba aliomba du´aa maalum katika mnasaba huu, kwa hiyo mtu aombe kile kitachomsahilikia. Hata hivyo ni jambo zuri ikiwa mtu ataomba kwa du´aa ya ´Umar:

اللهم أنت السلام ومنك السلام فحينا ربنا بالسلام” فحسن لثبوته عنه رضي الله عنه

“Ee Allaah! Hakika Wewe ni as-Salaam. Amani inatoka Kwako. Ee Mola wetu, Tuhuishe kwa amani.”

Hili limethibiti kutoka kwake – Allaah amuwie radhi.

[1] Ameipookea al-Bukhaariy (779) kwa ufupisho wangu) na ”Swahiyh Abiy Daawuud” (1630).

[2] Ameipokea al-Bukhaariy (780) kwa ufupisho wangu) na ”Swahiyh Abiy Daawuud” (1929).

[3] Ameipokea al-Faakihiy kwa cheni ya wapokezi ilio nzuri.

[4] Kuhusiana na hili kuna Hadiyth ya Hasan, imepokelewa katika ”as-Swahiyhah 2478”.

[5] Tazama ”al-Kalim at-Twayyib”, uk. 51-52 kwa uhakiki wangu.

[6] Ameipokea Ibn Abiy Shaybah kwa cheni ya wapokezi Swahiyh. Wengine wameipokea kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa cheni ya wapokezi dhaifu, kama ilivyobainishwa katika ”adh-Dhwa´iyfah” (1054).

[7] Ameipokea al-Bayhaqiy (5/72) kwa cheni ya wapokezi ilio nzuri kutoka kwa Sa´iyd bin al-Musayyab ambaye amesema:

“Nimemsikia ´Umar akisema maneno ambayo hayakusikiwa na mwengine yeyote. Nimemsikia akisema anapoona Nyumba… “

Imepokelewa vilevile kupitia sanadi nyingine ilio nzuri kutoka kwa Sa´iyd bin al-Musayyab aliyesema hivo. Pia ameipokea Ibn Abiy Shaybah (04/97) kutoka kwa wawili hao.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Manaasik-ul-Hajj wal-´Umrah, uk. 19-20
  • Imechapishwa: 07/07/2018