Lengo la tisa: Kuingia ndani zaidi katika kumfuata Mtume

Miongoni mwa malengo makuu ya hajj ni kuingia ndani zaidi katika kumfuata Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa ajili hii ndio maana utamuona yule mwenye kuhiji anatilia pupa kwelikweli kila kitendo chake kiwe ni chenye kuafikiana na Sunnah. Utamuona vilevile yule mwenye kuhiji anawauliza wanachuoni mara nyingi “Kuna ubaya nikifanya kitu fulani? Je, kitendo changu ni cha sawa? Je, ni chenye kuafikiana na Sunnah?” Utamuona yule mwenye kuhiji anatilia pupa kwelikweli kitendo chake kiwe ni chenye kuafikiana na Sunnah. Sote tunajua maneno ya Mtume wetu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Hadiyth ya Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) katika “as-Swahiyh” ya Muslim:

“Chukueni kutoka kwangu ´ibaadah zenu za hajj!”[1]

Aliyasema hayo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika hajj yake.

Utamuona yule mwenye kuhiji inapokuja katika maamrisho basi anatilia umuhimu kwelikweli kuyafanya na kuyatekeleza kikamilifu.  Inapokuja katika makatazo basi anatilia umuhimu kwelikweli kuyaacha na kujiepusha nayo. Utamuona anauliza kwa umakini na anachunga kikweli matendo yake yawe ni yenye kuafikiana na mwongozo wa Mtume mtukufu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Tazama yale maneno matukufu yaliyosemwa na ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) wakati alipolibusu jiwe:

“Ninaapa kwa Allaah kwamba hakika mimi najua kuwa wewe ni jiwe; hudhuru na wala hunufaishi. Lau nisingelimuona Mtume wa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akikubusu basi nami nisingekubusu.”[2]

Ya´laa bin Umayyah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia:

“Nilifanya Twawaaf pamoja na ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh). Nilipofika kwenye kona inayotazamana na mlango ilio baada ya mlango, nilimshika mkono wake ili aiguse. Akasema: “Una nini wewe?” Nikasema: “Si ulisalimie?” Akasema; “Wewe hukufanya Twawaaf na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)?” Nikasema: “Ndio.” Akasema: “Ulimuona akizigusa nguzo mbili hizi za magharibi?” Nikasema: “Hapana.” Ndipo akasema: “Kwani wewe huna kiigizo chema kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)?” Nikasema: “Ndio.” Akasema: “Basi nenda!”[3]

Bi maana hatufanyi kitu chochote katika matendo isipokuwa kile chenye kuafikiana na Sunnah za Mtume (Swall Allaahu ´alayhi wa sallam).

Kujengea juu ya haya miongoni mwa malengo makubwa na faida tukufu ambazo anafaidika nazo muislamu katika hajj yake ni yeye apupie katika maisha yake yote ´ibaadah zake zote ziwe ni zenye kuafikiana na Shari´ah ya Allaah (´Azza wa Jall) na aisemeze nafsi yake ´kama jinsi mimi katika hajj nilikuwa nikichunga, nikiiulizia, nikichunga jambo la kuafikiana na mwongozo wa Mtume (Swall Allaahu ´alayhi wa sallam), basi nitakuwa vivyo hivyo katika utiifu na ´ibaadah zangu zote`. Hivyo achunge Sunnah katika swalah yake, swawm yake na katika kila ´ibaadah ambayo anajikurubisha kwayo kwa Allaah. Atahadhari kwelikweli kutokamana na matamanio na Bid´ah ambazo Allaah hakuteremsha hoja yoyote juu yake.

Huenda mtu akakulia katika jamii ambazo Bid´ah zimekuwa nyingi na watu wamezizowea. Lakini ni lazima kwake kufaidika na hajj yake. Kama ambavo katika hajj yake alikuwa akitahadhari kutokamana na Bid´ah na akipupia Sunnah, basi pia kadhalika apupie juu ya hilo katika ´ibaadah zake zote. Matokeo yake ile hajj yake iwe itampa matunda ya kulazimiana na mwongozo wa Mtume mtukufu, kuafikiana na mfumo wake (Swall Allaahu ´alayhi wa sallam) na kutahadhari kutokamana na Bid´ah kwa aina zake mbalimbali.

[1] (1297).

[2] al-Bukhaariy (1597) na Muslim (1270).

[3] ”Musnad” ya Imaam Ahmad (313).

  • Mhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Maqaaswid-ul-Hajj, uk. 44-48
  • Imechapishwa: 20/08/2018