Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Miongoni mwa Sunnah za lazima ambazo mwenye kuacha kipengele chake na akaacha kuikubali na kuiamini hawi katika watu wake.”

MAELEZO

Miongoni mwa misingi ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah zipo Sunnah za lazima ambazo ni lazima kuzitambua, kuzifuata na kuzitendea kazi, kwa ndani na kwa uinje. Mwenye kuacha kitu katika Sunnah hizo amekhasirika na ametoka nje ya Sunnah katika kitu hicho cha faradhi. Aidha amejikosesha ujira wa kushikamana na Sunnah kikamilifu.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekuja na Sunnah sampuli mbili:

1- Ambayo ni ya faradhi.

2- Iliopendekezwa.

Yule mwenye kuacha Sunnah ya faradhi pasi na udhuru anapata dhambi.

Yule mwenye kuacha Sunnah iliopendekezwa basi amejikosesha ujira, lakini haadhibiwi.

Maimamu, akiwemo imamu Ahmad bin Hanbal na wafuasi wake, wanalingania kushikamana barabara na Sunnah ili Ummah uweze kuishi chini ya kivuli chake. Ndani ya Sunnah ndio ipo furaha ya Ummah. Haijuzu kuzembea juu ya Sunnah iliofaradhishwa. Kuhusu Sunnah iliopendekezwa pia inatakiwa kutendewa kazi kutokana na zile fadhilah, ujira mwingi na daraja nyingi za juu.

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 55-56
  • Imechapishwa: 02/10/2019