3- Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kwamba Mtume wa Allaah  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Je, nisikwambieni kile ninachokukhofieni kuliko hata huyo al-Masiyh ad-Dajjaal?” Wakasema: “Ndio, ee Mtume wa Allaah.” Akasema: “Ni shirki iliyojificha; anasimama mtu kuswali na akaipamba swalah yake kwa kuwa anaona watu wanamwangalia.”[1]

Abu Sa´iyd al-Khudriy jina lake ni Maalik bin Sinaan al-Khudriy na ni mmoja katika Maswahabah watukufu na maarufu. Allaah amuwie radh.

Maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Je, nisikwambieni kile ninachokukhofieni kuliko hata huyo al-Masiyh ad-Dajjaal?”

Hadiyth ina sababu yake; siku moja Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alijitokeza na Maswahabah wamekaa chini wakizungumzia kuhusu ad-Dajjaal na juu ya fitina zake. Walikuwa ni wenye woga ambao (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Je, nisikwambieni kile ninachokukhofieni kuliko hata huyo al-Masiyh ad-Dajjaal?” Wakasema: “Ndio, ee Mtume wa Allaah.”

Hapa kuna dalili inayoonyesha kuwa kufundisha kwa njia ya kuuliza na kujibu ni jambo limewekwa katika Shari´ah. Kufunza kwa mtindo huo kunafanya mafunzo yakakita kichwani. Wakati anapotaka kuwafunza Maswahabah zake kitu muhimu, basi anafanya hivo kwa njia ya kuuliza ili wao wenyewe waweze kutafuta jawabu kisha baadaye awajibie. Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ni shirki iliyojificha; anasimama mtu kuswali na akaipamba swalah yake kwa kuwa anaona watu wanamwangalia.”

Hapa kuna dalili inayoonyesha kuwa kujionyesha ni shirki iliyojificha. Imejificha kwa sababu inakuwa kwenye nia, makusudio na moyo. Hakuna anayejua hayo isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Hakuna yeyote anayejua wanayokusudia watu isipokuwa tu Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Katika Hadiyth kuna dalili inayofahamisha ukhatari wa kujionyesha. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameichelea juu ya watu ambao ni wabora zaidi wa Ummah huu – nao ni Maswahabah. Kusemwe nini juu ya wengine? Ameichelea juu yao zaidi kuliko alivyochelea juu yao fitina ya al-Masiyh ad-Dajjaal kwa sababu ni wachache tu wanaosalimika nayo. Ama kuhusu al-Masiyh ad-Dajjaal pamoja na ukubwa wa fitina zake – Allaah atukinge nazo sisi na nyie – madhara yake yatawafika tu wale ambao watakutana naye wakati atapojitokeza ilihali bado wakohai. Ama khatari ya kujionyesha inakuwa katika zama zote.

[1] Ahmad (11270) na Ibn Maajah (4203). Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Sunan Ibn Maajah” (3389).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: I´aanat-ul-Mustafiyd bi Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 445-446
  • Imechapishwa: 02/09/2019