11 – Idadi dhaifu ya waislamu na udhaifu wa nguvu za kijeshi ukilinganisha za makafiri

9 – Udhaifu wa waislamu

Allaah (Jalla wa ´Alaa) amebainisha dawa katika Kitabu Chake. Pindi Anapotambua kuwa kuna Ikhlaasw ya kikweli kwenye nyoyo za waja, basi Ikhlaasw hiyo natija yake itakuwa ni pamoja na kwamba itawashinda wale wenye nguvu kuliko wao. Kwa ajili hiyo wakati (´Azza wa Jalla) alipojua kwamba waislamu waliokula kiapo cha utii chini ya mti walikuwa wametimiza Ikhlaasw kama ipasavyo na akawasifu kwa hilo katika maneno Yake:

لَّقَدْ رَضِيَ اللَّـهُ عَنِ الْمُؤْمِنِينَ إِذْ يُبَايِعُونَكَ تَحْتَ الشَّجَرَةِ فَعَلِمَ مَا فِي قُلُوبِهِمْ

“Hakika Allaah amewawia radhi waumini walipokupa kiapo cha usikivu na utiifu chini ya mti alijua yale yaliyomo nyoyoni mwao”[1],

ndipo akabainisha kuwa kwa Ikhlaasw hii itawapelekea ikiwa ni pamoja na kwamba itawafanya waweze yale ambayo hapo kabla walikuwa si wenye kuyaweza. Amesema (Ta´ala):

وَأُخْرَىٰ لَمْ تَقْدِرُوا عَلَيْهَا قَدْ أَحَاطَ اللَّـهُ بِهَا

“Na [atakupeni ngawira] nyingine hamjaweza kuzipata bado [ambazo] Allaah amekwishazizingia.”[2]

Amesema wazi kwamba wasingeyaweza hapo kabla. Lakini Yeye ndiye ameyazunguka na akawafanya kuweza. Kwa hivyo akayafanya kuwa ni ngawira kwao pale alipojua Ikhlaasw waliokuwa nayo nyoyoni mwao. Siku moja pindi makafiri walipowashambulia waislamu katika vita vya Ahzaab ambapo waliwazingira kwa nguvu za kijeshi. Amesema (Ta´ala) kuhusu tukio hilo:

إِذْ جَاءُوكُم مِّن فَوْقِكُمْ وَمِنْ أَسْفَلَ مِنكُمْ وَإِذْ زَاغَتِ الْأَبْصَارُ وَبَلَغَتِ الْقُلُوبُ الْحَنَاجِرَ وَتَظُنُّونَ بِاللَّـهِ الظُّنُونَا هُنَالِكَ ابْتُلِيَ الْمُؤْمِنُونَ وَزُلْزِلُوا زِلْزَالًا شَدِيدًا

“Walipokujieni kutoka juu yenu, na kutoka chini yenu, na macho yalipokodoka, na nyoyo zikafikia kooni [kwa woga] na mkamdhania Allaah dhana mbalimbali [zisizo nzuri]. Basi hapo ndipo waumini walipojaribiwa na wakatetemeshwa tetemesho kali kabisa.”[3]

Wakati huo ilikuwa kutibu udhaifu huu na uzingiraji wa kijeshi ni kwa kumtakasia nia Allaah na kumuamini kwa imani ya nguvu. Amesema (Ta´ala):

وَلَمَّا رَأَى الْمُؤْمِنُونَ الْأَحْزَابَ قَالُوا هَـٰذَا مَا وَعَدَنَا اللَّـهُ وَرَسُولُهُ وَصَدَقَ اللَّـهُ وَرَسُولُهُ ۚ وَمَا زَادَهُمْ إِلَّا إِيمَانًا وَتَسْلِيمًا

“Basi waumini walipoona yale makundi, walisema: “Haya ndio yale aliyotuahidi Allaah na Mtume Wake na amesema kweli Allaah na Mtume Wake” na haikuwazidishia isipokuwa imani na kujisalimisha zaidi.””[4]

Ikhlaasw hii ikapelekea ikiwa ni pamoja na yale Allaah aliyoelezea:

وَرَدَّ اللَّـهُ الَّذِينَ كَفَرُوا بِغَيْظِهِمْ لَمْ يَنَالُوا خَيْرًا ۚ وَكَفَى اللَّـهُ الْمُؤْمِنِينَ الْقِتَالَ ۚ وَكَانَ اللَّـهُ قَوِيًّا عَزِيزًا وَأَنزَلَ الَّذِينَ ظَاهَرُوهُم مِّنْ أَهْلِ الْكِتَابِ مِن صَيَاصِيهِمْ وَقَذَفَ فِي قُلُوبِهِمُ الرُّعْبَ فَرِيقًا تَقْتُلُونَ وَتَأْسِرُونَ فَرِيقًا وَأَوْرَثَكُمْ أَرْضَهُمْ وَدِيَارَهُمْ وَأَمْوَالَهُمْ وَأَرْضًا لَّمْ تَطَئُوهَا ۚوَكَانَ اللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرًا

“Allaah akawarudisha nyuma wale waliokufuru kwa chuki zao hawakupata kheri yoyote na Allaah amewatosheleza waumini vitani. Na Allaah ni Mwenye nguvu kabisa, Mwenye enzi asiyeshindika. Na Aliwateremsha wale waliowasaidia [maadui] miongoni mwa Ahl-ul-Kitaab kutoka katika ngome zao na akatia khofu katika nyoyo zao; kundi mnaliua na kundi jingine mnaliteka. Na akakurithisheni ardhi yao, na majumba yao, na mali zao na ardhi hamkuwahi kuzikanyaga. Na Allaah daima juu ya kila kitu ni muweza.”[5]

Hawakuwa wakifikiria kuwa Allaah atawasaidia kwa njia hiyo, nayo ni kwa Malaika na upepo:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اذْكُرُوا نِعْمَةَ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ إِذْ جَاءَتْكُمْ جُنُودٌ فَأَرْسَلْنَا عَلَيْهِمْ رِيحًا وَجُنُودًا لَّمْ تَرَوْهَا

“Enyi mlioamini! Kumbukeni neema ya Allaah juu yenu pale yalipokujieni majeshi tukawapelekea upepo wa dhoruba na majeshi msiyoyaona.”[6]

Miongoni mwa dalili zenye kuonyesha kuwa Uislamu ndio dini ya haki, ni kuwa umati mdogo wa watu na ulio dhaifu ulioshikamana na Uislamu unashinda umati mkubwa na wenye nguvu wa makafiri:

كَم مِّن فِئَةٍ قَلِيلَةٍ غَلَبَتْ فِئَةً كَثِيرَةً بِإِذْنِ اللَّـهِ ۗ وَاللَّـهُ مَعَ الصَّابِرِينَ

“Makundi mangapi machache yameshinda makundi mengi kwa idhini ya Allaah? Na Allaah yu pamoja na wenye kusubiri.”[7]

Kwa ajili hiyo ndio maana Allaah (Ta´ala) akaita siku ya Badr kuwa ni ´alama´, `hoja´ na `pambanuzi´ kwa sababu imefahamisha kuwa Uislamu ndio dini ya haki. Amesema (Ta´ala):

قَدْ كَانَ لَكُمْ آيَةٌ فِي فِئَتَيْنِ الْتَقَتَا ۖ فِئَةٌ تُقَاتِلُ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَأُخْرَىٰ كَافِرَةٌ

“Kwa hakika ilikuwa ni alama kwenu katika makundi mawili yalipokutana. Kundi linapigana katika njia ya Allaah na jingine kafiri.”[8]

Hapa ilikuwa siku ya Badr.

إِن كُنتُمْ آمَنتُم بِاللَّـهِ وَمَا أَنزَلْنَا عَلَىٰ عَبْدِنَا يَوْمَ الْفُرْقَانِ

“… ikiwa nyinyi mumemwamini Allaah na yale tuliyoyateremsha kwa mja Wetu siku ya Upambanuzi.”[9]

Ilikuwa siku ya Badr.

لِّيَهْلِكَ مَنْ هَلَكَ عَن بَيِّنَةٍ وَيَحْيَىٰ مَنْ حَيَّ عَن بَيِّنَةٍ

“… ili aangamie yule wa kuangamia kwa hoja za wazi na ahuike mwenye kuhuika kwa hoja za wazi.”[10]

Kadhalika ilikuwa siku ya Badr kwa mujibu wa baadhi.

Umati mdogo na dhaifu wa waumini kushinda umati mkubwa na wenye nguvu wa makafiri, bila ya shaka ni dalili ya kwamba umati mdogo huu uko juu ya haki na kwamba ni Allaah ndiye ambaye kaunusuru. Amesema kuhusu vita vya Badr:

وَلَقَدْ نَصَرَكُمُ اللَّـهُ بِبَدْرٍ وَأَنتُمْ أَذِلَّةٌ

“Kwa hakika alikunusuruni Allaah katika Badr na hali nyinyi mlikuwa dhaifu.”[11]

إِذْ يُوحِي رَبُّكَ إِلَى الْمَلَائِكَةِ أَنِّي مَعَكُمْ فَثَبِّتُوا الَّذِينَ آمَنُوا ۚ سَأُلْقِي فِي قُلُوبِ الَّذِينَ كَفَرُوا الرُّعْبَ

“Pale Mola wako alipowatia ilhamu Malaika [kuwaambia]: “Hakika Mimi niko pamoja nanyi, basi wathibitisheni wale walioamini. Nitatia woga kwenye nyoyo za waliokufuru.”[12]

Allaah amewaahidi waumini kuwa atawanusuru. Allaah (Ta´ala) amezitaja sifa zao na kuwapambanua kutokana na wengine:

وَلَيَنصُرَنَّ اللَّـهُ مَن يَنصُرُهُ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَقَوِيٌّ عَزِيزٌ

“Bila shaka Allaah atamnusuru yeyote anayemnusuru. Hakika Allaah ni Mwenye nguvu kabisa, Mwenye enzi asiyeshindika.”[13]

Kisha Akawapambanua na wengine wote kwa sifa zao:

الَّذِينَ إِن مَّكَّنَّاهُمْ فِي الْأَرْضِ أَقَامُوا الصَّلَاةَ وَآتَوُا الزَّكَاةَ وَأَمَرُوا بِالْمَعْرُوفِ وَنَهَوْا عَنِ الْمُنكَرِ ۗ وَلِلَّـهِ عَاقِبَةُ الْأُمُورِ

“Ambao Tukiwamakinisha katika ardhi, basi husimamisha swalah na hutoa zakaah na huamrisha mema na hukataza maovu; na kwa Allaah pekee ndio hatima ya mambo yote.”[14]

Dawa hii tuliyoiashiria dhidi ya uzingiraji wa kijeshi, kadhalika ndio dawa dhidi ya uzingiraji wa kiuchumi. Allaah (Ta´ala) ameashiria hilo katika Suurah “al-Munaafiquun” na kusema:

هُمُ الَّذِينَ يَقُولُونَ لَا تُنفِقُوا عَلَىٰ مَنْ عِندَ رَسُولِ اللَّـهِ حَتَّىٰ يَنفَضُّوا

“Wao ndio wale wasemao: “Msitoe [mali] kwa ajii ya walioko kwa Mtume wa Allaah mpaka watoweke.””[15]

Kitendo hichi ambacho wanafiki walikuwa wanataka kuwafanyia waislamu si chengine isipokuwa ni uzingiraji wa kiuchumi. Akaashiria (Ta´ala) ya kwamba dawa yake ni kuwa na imani yenye nguvu Kwake na kuelekea Kwake (Jalla wa ´Alaa) kikweli. Amesema:

وَلِلَّـهِ خَزَائِنُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَلَـٰكِنَّ الْمُنَافِقِينَ لَا يَفْقَهُونَ

“Na ni za Allaah pekee hazina za mbingu na ardhi, lakini wanafiki hawafahamu.”[16]

Ambaye mikononi Mwake mna hazina za mbingu na ardhi mtu akimuelekea, haanguki:

وَمَن يَتَّقِ اللَّـهَ يَجْعَل لَّهُ مَخْرَجًا وَيَرْزُقْهُ مِنْ حَيْثُ لَا يَحْتَسِبُ ۚ وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ فَهُوَ حَسْبُهُ

“Na yule anayemcha Allaah humjaalia njia [ya kutokea] na atamruzuku kutoka njia ambayo hatizamii. Na yule anayemtegemea Allaah, basi Yeye humtosheleza.”[17]

Akabainisha hilo vilevile kwa kusema:

وَإِنْ خِفْتُمْ عَيْلَةً فَسَوْفَ يُغْنِيكُمُ اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ إِن شَاءَ

“Na mkikhofu umasikini basi Allaah atakutajirisheni kutokana na fadhilah Zake – Akitaka.”[18]

[1] 48:18

[2] 48:21

[3] 33:10-11

[4] 33:22

[5] 33:25-27

[6] 33:09

[7] 02:249

[8] 03:13

[9] 08:41

[10] 08:42

[11] 03:123

[12] 08:12

[13] 22:40

[14] 22:41

[15] 63:07

[16] 63:07

[17] 65:02-03

[18] 09:28

  • Mhusika: Imaam Muhammad Amiyn ash-Shanqiytwiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Islaam diyn al-Kaamil, uk. 22-25
  • Imechapishwa: 14/06/2023