Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Tambua – Allaah akurehemu – kwamba ni wajibu kwa kila muislamu mwanaume na mwanamke, kujifunza masuala haya matatu na kuyatendea kazi:

La kwanza: Allaah ametuumba…

MAELEZO

Dalili za Qur-aan na Sunnah na za kiakili zinazothibitisha kuwa Allaah ametuumba ni hizi zifuatazo:

1- Dalili za Qur-aan na Sunnah ni nyingi na miongoni mwazo ni maneno Yake (Ta´ala):

هُوَ الَّذِي خَلَقَكُم مِّن طِينٍ ثُمَّ قَضَىٰ أَجَلًا ۖ وَأَجَلٌ مُّسَمًّى عِندَهُ ۖ ثُمَّ أَنتُمْ تَمْتَرُونَ

“Yeye ndiye ambaye amekuumbeni kutokana na udongo kisha akakidhia muda [juu ya kila kiumbe] – na muda maalum uko Kwake, kisha nyinyi mnafanya shaka!” (al-An´aam 06 : 02)

وَلَقَدْ خَلَقْنَاكُمْ ثُمَّ صَوَّرْنَاكُمْ

“Hakika Tumekuumbeni kisha tukakutieni sura.” (al-A´raaf 07 : 11)

وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ مِن صَلْصَالٍ مِّنْ حَمَإٍ مَّسْنُونٍ

“Hakika Tumemuumba mtu kutokana na udongo wa mfinyanzi unaotoa sauti unaotokana na tope nyeusi iliyofinyangwa.” (al-Hijr 15 : 26)

وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَكُم مِّن تُرَابٍ ثُمَّ إِذَا أَنتُم بَشَرٌ تَنتَشِرُونَ

“Miongoni mwa ishara Zake ni kwamba amekuumbeni kutokana na udongo tahamaki mmekuwa watu mnaotawanyika.” (ar-Ruum 30 : 20)

خَلَقَ الْإِنسَانَ مِن صَلْصَالٍ كَالْفَخَّارِ

“Amemuumba mtu kutokana na udongo wa mfinyanzi unaotoa sauti kama wa vyungu uliookwa moto.” (ar-Rahmaan 55 : 14)

اللَّـهُ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ

“Allaah ni Muumbaji wa kila kitu.” (az-Zumar 39 : 62)

وَاللَّـهُ خَلَقَكُمْ وَمَا تَعْمَلُونَ

“Allaah amekuumbeni na yale yote mnayoyafanya” (asw-Swaaffaat 37 : 96)

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Sikuumba majini na watu isipokuwa waniabudu.” (adh-Dhaariyaat 51 : 56)

2- Dalili za kiakili ishara yake imekuja katika maneno Yake (Ta´ala):

أَمْ خُلِقُوا مِنْ غَيْرِ شَيْءٍ أَمْ هُمُ الْخَالِقُونَ

“Au wameumbwa pasipo na kitu chochote? Au wao wenyewe ndio waumbaji?” (at-Twuur 52 : 35)

Hakika mtu hakujiumba mwenyewe kwa sababu hapo kabla hakuwepo na kitu kisichokuwepo hakiwezi kuumba. Kitu kisichokuwepo hakiwezi kuumba kitu kilichopo. Hakuumbwa na wazazi wake wala kiumbe yeyote na vilevile hakuja patupu bila ya muumbaji. Kila kilochozuka ni lazima kiwe na ambaye alikizusha. Jengine ni kwamba kuwepo kwa viumbe hivi kumejengwa kwa ubora na kwa mpangilio na nidhamu, jambo ambalo haliwezekani kabisa wakawa wametokana patupu au kwa bahati nasibu. Uwepo wa patupu asli hauumbwi kwa nidhamu yoyote na kwa hivyo kubaki kwake na maendeleo yake hayawezi pia kuwa hivo. Hii inakuwa ni sababu ya wazi inayoonyesha kuwa Muumbaji ni Allaah lekee – hakuna Muumbaji wala Mwamrishaji yeyote isipokuwa Allaah pekee. Allaah (Ta´ala) Amesema:

أَلَا لَهُ الْخَلْقُ وَالْأَمْرُ

“Zindukeni! Ni Vyake pekee uumbaji na amri.” (al-A´raaf 07 : 54)

Haijulikani kwamba kuna kiumbe yeyote aliyekanusha uola wa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) isipokuwa kwa njia ya kiburi, kama alivofanya Fir´awn.

Siku moja Jubayr bin Mutw´im alisikia jinsi Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anavosoma Suurah at-Twuur na akafika katika Aayah inayosema:

أَمْ خُلِقُوا مِنْ غَيْرِ شَيْءٍ أَمْ هُمُ الْخَالِقُونَ أَمْ خَلَقُوا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ ۚ بَل لَّا يُوقِنُونَ أَمْ عِندَهُمْ خَزَائِنُ رَبِّكَ أَمْ هُمُ الْمُصَيْطِرُونَ

“Au wameumbwa pasipo na kitu chochote? Au wao wenyewe ndio waumbaji? Au wameumba mbingu na ardhi? Bali hawana yakini. Au wanazo hazina za Mola wako? Au wao ndio wenye mamlaka nayo?” (at-Twuur 52 : 35-37)

Wakati huo Jubayr bin Mutw´im alikuwa ni mshirikina na akawa amesema:

“Moyo wangu ulikuwa unakaribia kuruka na hapo ndio ilikuwa mara ya kwanza imani kuingia kwenye moyo wangu.”[1]

[1] al-Bukhaariy (4853), Muslim (463), Abu Daawuud (806), an-Nasaa’iy (986), Ibn Maajah (832), Maalik (167), ash-Shaafi´iy, uk. 214, ad-Daarimiy (1295), Ibn Khuzaymah (514), at-Twahaawiy (1/211-212), Abu ´Awaanah (1766) na Ibn Hibbaan (1831).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 28-30
  • Imechapishwa: 18/05/2020