Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Suala la pili: Kuifanyia kazi.

MAELEZO

Kuifanyia kazi: Bi maana elimu hiyo. Kwa sababu haitoshi kwa mtu kujua na kujifunza. Bali ni lazima aifanyie kazi elimu yake. Elimu pasi na matendo ni hoja dhidi ya mtu mwenyewe. Elimu haiwi ni yenye kunufaisha isipokuwa kwa matendo. Ama kwa yule mwenye kujua na asifanye matendo ni mwenye kughadhibikiwa. Kwa sababu ameijua haki na akaiacha kwa ujuzi. Mshairi amesema:

Msomi kwa elimu yake asiyoifanyia kazi

ataadhibiwa kabla ya mwabudia sanamu.

Haya yametajwa katika Hadiyth tukufu:

“Watu wa kwanza wataoingizwa Motoni siku ya Qiyaamah ni msomi ambaye hakuitendea kazi elimu yake.”[1]

Elimu imefungamana na matendo. Matendo ndio matunda ya elimu. Elimu pasi na matendo ni kama mti bila matunda. Haina faida yoyote. Elimu imeteremshwa kwa ajili ya kutendewa kazi. Ni kama ambavo matendo bila ya elimu yanakuwa ni janga na upotevu kwa mwenye nayo. Ikiwa mtu anafanya matendo bila ya elimu basi matendo yake yanakuwa ni janga na kujichosha kwa mwenye nayo. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yule atakayefanya kitendo kisichoafikiana na amri yetu atarudishiwa mwenyewe.”[2]

Kwa ajili hii tunasoma katika “al-Faatihah” katika kila Rak´ah:

اهْدِنَا الصِّرَاطَ الْمُسْتَقِيمَ صِرَاطَ الَّذِينَ أَنْعَمْتَ عَلَيْهِمْ غَيْرِ الْمَغْضُوبِ عَلَيْهِمْ وَلَا الضَّالِّينَ

“Tuongoze njia iliyonyooka. Njia ya wale Uliowaneemesha, si ya walioghadhibikiwa wala waliopotea.”[3]

Allaah amewaita kuwa ni wapotevu wale wanaotenda pasi na elimu na wale wanaojua na hawafanyi matendo kwamba wameghadhibikiwa. Kwa hiyo mzinduke juu ya hilo kwa kuwa ni jambo muhimu sana.

[1] at-Tirmidhiy (2382).

[2] al-Bukhaariy (7350) hali ya kuiwekea taaliki na Muslim (18) (1718).

[3] 01:06-07

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 24-26
  • Imechapishwa: 23/11/2020