08. Uharamu wa kumwingilia mwanamke kwenye tupu ya nyuma


6- Uharamu wa kumwingilia mwanamke katika tupu ya nyuma

Ni haramu kwake kumwingilia katika tupu ya nyuma kwa ufahamu wa Aayah iliotangulia:

نِسَاؤُكُمْ حَرْثٌ لَّكُمْ فَأْتُوا حَرْثَكُمْ أَنَّىٰ شِئْتُمْ

“Wake zenu ni konde kwenu. Hivyo ziendeeni konde zenu vyovyote mpendavyo.”[1]

Dalili ya hilo pia ni zile Hadiyth zilizotangulia. Kuna Hadiyth zengine pia:

1- Umm Salamah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia akisema:

“Muhaajiruuna walipofika al-Madiynah kwa Answaar walioa katika wanawake wao. Wanawake wa Muhaajiruun walikuwa wakilala kiifudifudi wakati wa jimaa na Answaar walikuwa hawapendezwi na hivo. Mwanamume mmoja wa Muhaajiruun akamtaka mwanamke wake afanye hivo ambapo mwanamke yule akawa amekataa mpaka kwanza amuulize Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Nikamwende ambapo nikaona haya kumuuliza na badala yake nikamuuliza Umm Salamah ambapo kukawa kumeteremka:

نِسَاؤُكُمْ حَرْثٌ لَّكُمْ فَأْتُوا حَرْثَكُمْ أَنَّىٰ شِئْتُمْ

“Wake zenu ni konde kwenu. Hivyo ziendeeni konde zenu vyovyote mpendavyo.”

Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

Hapana [si kwenye tupu ya nyuma]! Isipokuwa ni pale kwenye tupu ya mbele.”[2]

2-  Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) alikuja kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Nimeangamia!” Akasema: “Ni kipi kilichokuangamiza?” Akajibu: “Nimepindua kipando changu usiku wa leo.” Pamoja na hivyo hakumjibu kitu. Ndipo kukateremshwa kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Aayah ifuatayo:

نِسَاؤُكُمْ حَرْثٌ لَّكُمْ فَأْتُوا حَرْثَكُمْ أَنَّىٰ شِئْتُمْ

“Wake zenu ni konde kwenu. Hivyo ziendeeni konde zenu vyovyote mpendavyo.”

Akasema: “Kupitia kwa mbele, kupitia kwa nyuma na jichunge tupu ya nyuma na wakati anapokuwa na hedhi.”[3]

3- Khuzaymah bin Thaabit (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia:

“Kuna mwanamume mmoja alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu kuwaingilia wanawake kupitia kwa nyuma au mwanaume kumwingilia mwanamke kwa nyuma yake ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Ni halali.” Wakati mtu yule alipoanza kuondoka zake akamwita au aliamrisha aitwe. Akasema: “Ulisema nini?” Kupitia njia gani ulikuwa wamaanisha?” Ukiwa unamaanisha kumwingilia kutoka kwa nyuma ni sawa. Ama ikiwa wamaanisha kumwingilia kwenye tupu yake ya nyuma haifai. Hakika Allaah hastahiki juu ya haki. Msiwaendee wanawake kwenye tupu zao za nyuma.”[4]

4- Allaah hamtazami mwanaume mwenye kumwendea mkewe kwenye tupu yake ya nyuma[5].

5- Amelaaniwa yule mwenye kuwaendea wanawake kwenye tupu zao za nyuma[6].

6- Mwenye kumwingilia mwenye hedhi, mwanamke kwenye tupu yake au kuhani na akamsadikisha kwa yale aliyoyasema basi amekufuru yale yaliyoteremshwa kwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)[7].

[1] 02:223

[2] Ameipokea Ahmad (06/305), 310-318 na siyaaq ni yake, at-Tirmidhiy (03/75) ambaye ameisahihisha, Abu Ya´laa (01/329), Ibn Abiy Haatim katika “Tafsiyr” yake (01/39), Mahmudiyyah na al-Bayhaqiy (07/195),

[3] Ameipokea an-Nasaa´iy katika “al-´Asharah” (02/76), at-Tirmidhiy (02/162), Ibn Haatim (01/39), at-Twabaraaniy (02/156/03), al-Waahid, uk. 53 kwa mlolongo wa wapokezi mzuri. Ni nzuri kwa mujibu wa at-Tirmidhiy.

[4] Ameipokea ash-Shaafi´iy (02/260) na ameipa nguvu, al-Bayhaqiy (07/196), ad-Daarimiy (01/145), at-Twahaawiy (02/25), al-Khattwaabiy katika “Ghariyb-ul-Hadiyth” (02/73) na mlolongo wa wapokezi wake ni Swahiyh.

[5] Ameipokea an-Nasaa´iy katika “al-´Asharah”, at-Tirmidhiy, Ibn Hibbaan kupitia Hadiyth ya Ibn ´Abbaas na mlolongo wa wapokezi wake ni mzuri. Vilevile ni nzuri kwa mujibu wa at-Tirmidhiy. Ni Swahiyh kwa mujibu wa Ibn Raahuuyah kama ilivyo katika “Masaa-il al-Marwaziy”. Ina njia nyingine kwa Ibn Jaaruud kwa mlolongo wa wapokezi mzuri. Ameipa nguvu Ibn Daqiyq al-´Iyd, an-Nasaa´iy, Ibn ´Asaakir na Ahmad kupitia Hadiyth ya Abu Hurayrah.

[6] Ameipokea Ibn ´Uday  (01/211) kupitia Hadiyth ya ´Uqbah bin ´Aamir kwa mlolongo wa wapokezi mzuri. Ni katika mapokezi ya Ibn Wahb, Ibn Luhay´ah. Ina shawahidi kupitia Hadiyth ya Abu Hurayrah aliyepokea kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ameipokea Abu Daawuud kwa nambari. 2162, Ahmad (02/444) na 479.

[7] Ameipokea waandishi wa “as-Sunan” wane isipokuwa an-Nasaa´iy ambaye ameipokea katika “al-´Asharah” (78), ad-Daarimiy, Ahmad (02/408) na 476 na matamshi ni yake na wengineo.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Aadaab-uz-Zafaaf, uk. 101-107
  • Imechapishwa: 04/03/2018