08. Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah ndio lengo la ulinganizi wa Mitume yote

Inaitwa vilevile Tawhiyd-ul-´Ibaadah na Tawhiyd-ul-Iraadah wal-Qaswd. Tawhiyd hii ndio lengo na ndio chanzo cha magomvi kati ya Mitume na wafuasi wao. Kila Mtume alikuja akiwaambia wafuasi wake:

يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ

“Enyi watu wangu! Mwabuduni Allaah, kwani hakika hamna mungu wa haki asiyekuwa Yeye.”[1]

Walikuwa hawawaambii:

“Enyi watu wangu! Hakika Allaah ndiye Mola wenu.”

kwa sababu walikuwa ni wenye kulikubali hili. Badala yake walikuwa wakitaka kutoka kwao wamuabudu Mola wao ambaye wamekubali juu ya uola Wake na kwamba Yeye pekee ndiye muumbaji, mruzukaji na mwenye kuyaendesha mambo. Walikuwa wakitaka kutoka kwao wampwekeshe katika ´ibaadah kama ambavyo walivyompwekesha katika uumbaji na uendeshaji wa mambo. Kunatumiwa hoja dhidi yao kwa yale waliyoyakubali.

Qur-aan inataja Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah kwa njia ya kuitumia kama hoja dhidi ya makafiri na kuwataka wafanye yale inayopelekea. Makafiri! Maadamu nyinyi ni wenye kukubali ya kwamba Allaah pekee ndiye muumbaji, mruzukaji, mwenye kuokoa kutoka katika maangamivu na matatizo peke yake. Kwa nini basi mnaabudu mwengine asiyekuwa Yeye? Isitoshe mnaviabudu visivyoumba, visivyoruzuku na havina uwezo wowote ule:

أَفَمَن يَخْلُقُ كَمَن لَّا يَخْلُقُ ۗ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ

“Je, yule anayeumba ni kama asiyeumba? Kwa nini hamzingatii?”[2]

Kwa hivyo Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah ndio ambayo Mitume waliwalingania na kuwataka watu wao. Bado mpaka hii leo aina hii ya Tawhiyd ndio ugomvi kati ya Ahl-ut-Tawhiyd na wapindaji. Watu walio na ´Aqiydah sahihi wanawataka wale waliopinda katika Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah na wakarudi katika dini ya washirikina kwa njia ya kuyaabudia makaburi na kuwatukuza watu. Wapwekeshaji wanawataka watu hawa warudi katika ´Aqiydah sahihi na wamuabudu Allaah peke yake. Wanawataka waache jambo hili la khatari ambalo wako juu yake. Kwani hii ndio dini ya kipindi kabla ya kuja Uislamu. Bali hii ni dini mbaya zaidi kuliko ile ya kipindi kabla ya kuja Uislamu. Kwa sababu watu wa kipindi kabla ya kuja Uislamu walikuwa wakimtakasia ´ibaadah Allaah katika hali ya shida na wakimshirikisha wakati wa raha. Ama kuhusu watu hawa waliopinda ushirikina wao unakuwa daima katika hali ya raha na ya shida. Sivyo bali ushirikina wao katika hali ya shida inakuwa mbaya zaidi. Mambo yakizidi kuwa magumu zaidi kwao unawasikia wanaomba uokozi kutoka kwa mawalii, walio ndani ya makaburi na wafu. Upande mwingine washirikina pindi walipokuwa wakishikwa na dhara basi wanamtakasia maombi Allaah (´Azza wa Jall). Hii ndio aina ya pili katika aina za Tawhiyd. Aina hii ndio ambayo Mitume wote waliwataka watu wao wamtakasie nayo Allaah (´Azza wa Jall). Aina hii ya Tawhiyd ndio ambayo kuna ugomvi juu yake. Aina hii ya Tawhiyd ndio ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwapiga vita washirikina mpaka wakaachana nayo. Hii ndio maana ya hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah. Mungu maana yake ni yule mwenye kuabudiwa.

Maana yake “Laa ilaaha illa Allaah” ni kuwa hakuna mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

Maana ya “mungu” haina maana kama wanavyosema baadhi ya wapotevu kuwa maana yake ni muweza wa kuvumbua na kuumba. Uhakika wa mambo ni kwamba mungu maana yake ni mwabudiwa.

[1] 07:59

[2] 16:17

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mujmal ´Aqiydat-is-Salaf as-Swaalih, uk. 08-09
  • Imechapishwa: 24/05/2022