08. Asiyemkufurisha kafiri au akatilia shaka ukafiri wake

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

03 – Asiyekuwakufurisha washirikina au akawa na shaka juu ya ukafiri wao au akaonelea kuwa madhehebu yao ni sahihi amekufuru.

MAELEZO

Kichenguzi cha tatu miongoni mwa mambo yanayotengua Uislamu ni yule asiyemkufurisha mshirikina au akatilia shaka ukafiri wao au akaonelea kuwa madhehebu yao ni sahihi amekufuru kwa maafikiano.

Neno “mshirikina” linakusanya makafiri wote ikiwa ni pamoja na mayahudi, manaswara, wenye kuabudia makaburi, wakomunisti na wakanamungu. Wote hawa ni washirikina. Kinachowakutanisha ni kitu kimoja: kumshirikisha Allaah (´Azza wa Jall).

Mayahudi ni washirikina kwa sababu hawamwamini Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), jambo ambalo ni shirki. Manaswara ni washirikina kwa kuwa na wao hawamwamini Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na pia wanamwabudu ´Iysaa (´alayhis-Swalaatu was-Salaam). Waabudia makaburi, waabudia moto na wanafiki ni washirikina. Hivyo basi, yule asiyekuwakufurisha washirikina ni kafiri.

Vivyo hivyo mwenye kuwa na shaka juu ya ukafiri wa makafiri. Mwenye kutilia shaka kuwa mayahudi, manaswara au wenye kuabudia makaburi ni makafiri basi na yeye ni kafiri kutokana na shaka yake hii.

Vilevile mwenye kuonelea kuwa madhehebu yao ni sahihi. Kwa mfano mtu akasema kuwa anaona kuwa mayahudi wako katika dini sahihi na manaswara wako katika dini sahihi. Mfano mwingine ni kama mtu aulizwe juu ya mayahudi na manaswara ambapo akasema kuwa hawezi kusema lolote juu yao. Akajibu kwa kusema kuwa mayahudi, manaswara na waislamu wote wako katika dini na ambaye anataka kuamini Uislamu, uyahudi au ukristo ana haki ya kufanya hivo. Hii ni shirki. Huyu kwa maafikiano anakuwa kafiri kwa sababu ameonelea kuwa madhehebu ya washirikina ni sahihi na vilevile hakuwakufurisha.

Kadhalika pale atapotilia shaka na kusema kuwa hajui kama ni makafiri au sio makafiri kwa sababu mayahudi wameteremshiwa Kitabu ambacho ni Tawraat, manaswara wameteremshiwa Injiyl na waislamu wameteremshiwa Qur-aan. Kwa hivyo mimi sijui kama ni makafiri au sio makafiri. Huyu anakufuru akitilia shaka. Ni lazima akate kabisa ukafiri wa mayahudi, manaswara na waabudia makaburi. Dalili ya hili ni maneno Yake (Ta´ala):

فَمَن يَكْفُرْ بِالطَّاغُوتِ وَيُؤْمِن بِاللَّـهِ فَقَدِ اسْتَمْسَكَ بِالْعُرْوَةِ الْوُثْقَىٰ

“Basi atakayemkanusha twaaghuwt [miungu ya uongo] na akamwamini Allaah kwa hakika atakuwa ameshikilia imara kishikilio madhubuti.”[1]

Asiyekuwakufurisha washirikina au akawa na shaka juu ya ukafiri wao au akaonelea kuwa madhehebu yao ni sahihi, basi hakukufuru Twaaghuut. Imani haisihi isipokuwa kwa kupatikana mambo mawili:

1 – Kukufuru Twaaghuut.

2 – Kumuamini Allaah.

[1] 02:256

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tabswiyr-ul-Anaam bisharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 22-25
  • Imechapishwa: 09/04/2023