08. Talbiyah na kunyanyua sauti kwa ajili yake

13- Halafu ataelekea Qiblah[1] hali ya kuwa ni mwenye kusimama, kisha ataleta Talbiyah ya ´Umrah, au hajj pamoja na ´Umrah, na kusema:

“Ee Allaah! Hakika hii ni hajj na hakuna kujionyesha ndani yake wala kutaka kusikika.”[2]

14- Halafu alete Talbiyah kama alivofanya (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Nimekuitikia, ee Allaah, nimekuitikia. Nimekuitikia, hauna Wewe mshirika, nimekuitikia. Hakika sifa himdi zote, neema na ufalme ni Wako. Hauna mshirika Wewe.”

Alikuwa hazidishi zaidi ya hapo.

Katika Talbiyah yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ilikuwa ni pamoja na:

“Nimekuitikia, ee Mola wa kweli.”

15-  Lililo bora ni kulazimiana na Talbiyah yake, japokuwa kuzidisha juu yake ni jambo linalofaa, kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwakubalia watu ambao walikuwa wanazidisha wakisema:

“Nimekuitikia Wewe uliye na njia za kuelekea mbinguni. Nimekuitikia Wewe mwenye fadhilah.”

Ibn ´Umar alikuwa akizidisha juu yake na akisema:

“Nimekuitikia. Utukufu ni Wako. Kheri iko mikononi Mwako. Kujipendekeza na matendo ni kwa ajili Yako.”[3]

16- Mwenye kufanya Talbiyah anaamrishwa anyanyue sauti yake kwa ajili ya Talbiyah. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Jibriyl amenijia mimi na akaniamrisha niwaamrishe Maswahabah wangu na wale wiotewalio pamoja mimi wanyanyue sauti zao kwa Talbiyah.”[4]

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Bora ya hajj ni ile mtu ananyanyua sauti kwa Talbiyah na kumwaga damu.”[5]

Kwa sababu hiyo Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikuwa wakipiga ukelele kwelikweli kwa hiyo Talbiyah. Abu Haazim amesema:

“Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pindi walipokuwa wanaingia kwenye Ihraam, zinakauka sauti zao kabla ya kufika Rawhaa´.”[6]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kama kwamba namtazama Muusa (´alayhis-Salaam) akiteremka katika bonde hili na hali ya kuwa ana ukelele kwa Mola wake (Ta´ala) kwa kuleta Talbiyah.”[7]

17- Kwa sababu ya kuenea kwa zile Hadiyth mbili zilizotangulia, basi wanawake wanatakiwa kufanya vilevile kama wanavofanya wanamme wakati wa Talbiyah. Wanatakiwa kunyanyua sauti zao maadamu hakuchelewi fitina. Sababu nyingine ni kwa kuwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) alikuwa akinyanyua sauti yake mpaka wanaisikia wanaume. Abu ´Atwiyyah amesema:

“Nimemsikia ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) akisema: “Hakika mimi najua ni vipi ilikuwa Talbiyah ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).” Baada ya hapo nikamsikia akisema: “Nimekuitikia, ee Allaah.”[8]

al-Qaasim bin Muhammad amesema:

“Usiku wa Nafr Mu´aawiyah alitoka na akasikia sauti ya Talbiyah. Akasema: “Ni nani huyu?” Kukasemwa: “Ni ´Aaishah, mama wa waumini ambaye amefanya ´Umrah kutokea Tan´iym.” Baada ya hapo akaelezwa hayo ´Aaishah. Akasema: “Lau angeniuliza, basi ningemweleza.”[9]

18- Atalazimiana na Talbiyah, kwa sababu ni katika nembo za hajj[10]. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakuna yeyote ambaye anafanya Talbiyah, isipokuwa kuna miti na mawe yaliyoko kuliani kwake na kushotoni kwake ambavo navyo vinafanya Talbiyah mpaka ardhi ikatike kutokea huku na huku.”[11]

Khaswa khaswa kila pale ambapo anapanda sehemu ya juu au anaposhuka. Dalili ya hilo ni Hadiyth iliotangulia punde kidogo isemayo:

“Kama kwamba namtazama Muusa (´alayhis-Salaam) akiteremka katika bonde hili na hali ya kuwa ana ukelele kwa Mola wake (Ta´ala) kwa kuleta Talbiyah.”

Katika Hadiyth nyingine imekuja:

“Kama kwamba namtazama yeye pale anapoteremka katika bonde na analeta Talbiyah.”[12]

19- Inafaa kwake yeye kuchanganya kati ya Talbiyah na kusema hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah. Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Nilitoka pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na hakuacha kufanya Talbiyah mpaka alipopiga kwenye kile kiguzo cha ´Aqabah. Hata hivyo alikuwa akichanganya kati ya Talbiyah na kusema kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah.”[13]

20- Atapofika katika maeneo matakatifu ya Makkah na akayaona majumba ya wakazi wake, atajizuia kuleta Talbiyah[14] ili apate nafasi ya kujishughulisha na ´ibaadah nyenginezo zitazokuja.

[1] Ameipokea al-Bukhaariy kwa cheni ya wapokezi iliyopungua na al-Bayhaqiy ameipokea kwa kuungana kwa cheni ya wapokezi Swahiyh.

[2] Ameipokea adh-Dhwiyaa´ kwa cheni ya wapokezi Swahiyh.

[3] Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim. Tazama “Swahiyh Abiy Daawuud” (1590).

[4] Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, an-Nasaa’iy, Ibn Maajah na wengineo. Tazama ”Swahiyh Abiy Daawuud” (1592).

[5] Hadiyth ni nzuri. Tazama ”Swahiyh al-Jaamiy´ as-Swahiyh wa Ziyaadatih” (1112)

[6] Ameipokea Sa´iyd bin Mansuur kwa cheni ya wapokezi ilio nzuri, kama ilivyotajwa katika “al-Muhallaa” (07/94). Vilevile imepokelewa na Ibn Abiy Shaybah kwa cheni ya wapokezi Swahiyh, cheni ya wapokezi iliokatika kutoka kwa al-Muttwalib bin ´Abdillaah, kama ilivyotajwa katika “Fath-ul-Baariy” (3/324).

[7] Ameipokea Muslim. Tazama ”as-Swahiyhah” (2023).

[8] Ameipokea al-Bukhaariy (679 – chapisho fupi), at-Twayaalisiy (1513) na Ahmad (6/32, 100, 180 na 243).

[9] Ameipokea Ibn Abiy Shaybah kwa cheni ya wapokezi Swahiyh, kama alivyopokea katika “al-Muhallaa” (7/94-95). Shaykh-ul-Islaam amesema katika “al-Mansik” amesema:

“Mwanamke anatakiwa kunyanyua sauti kiasi cha kwamba rafiki yake wa kike anaweza kumsikia. Imependekezwa kufanya hivo katika hali mbalimbali.”

[10] Hiki ni kipande cha Hadiyth Swahiyh kilichotajwa katika “as-Swahiyhah” (828). Muundo wake ni kama ifuatavyo:

“Jibriyl ameniamrisha kunyanyua sauti wakati wa Talbiyah, kwani hakika kufanya hivo ni katika nembo za hajj.”

[11] Ameipokea Ibn Khuzaymah na al-Bayhaqiy kwa cheni ya wapokezi Swahiyh, kama ilivyotajwa katika ”at-Targhiyb wat-Tarhiyb” (2/118).

[12] Ameipokea al-Bukhaariy ((60/8) kwa ufupisho wangu). Haafidhw amesema:

“Katika Hadiyth inapata kufahamika kwamba Talbiyah ni katika Sunnah za Mitume na khaswa khaswa inasomwa wakati wa kupanda na wakati wa kushuka mahali.”

[13] Ameipokea Ahmad (1/417) kwa cheni ya wapokezi nzuri. Inazingatiwa kuwa ni Swahiyh na al-Haakim na adh-Dhahabiy, kama ilivyotajwa katika ”al-Hajj al-Kabiyr”

[14] Ameipokea al-Bukhaariy ((779) kwa ufupisho wangu) na al-Bayhaqiy. Tazama ”al-Majma´” (3/225-239).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Manaasik-ul-Hajj wal-´Umrah, uk. 16-19
  • Imechapishwa: 07/07/2018