08. Shirki inabatilisha matendo


2- Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba Mtume wa Allaah  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah (Ta´ala) amesema: “Hakika Mimi ni Mwenye kujitosheleza kutohitajia washirika. Hivyo basi yule atakayefanya kitendo akanishirikisha Mimi pamoja na mwingine, basi nitamwacha yeye na shirki yake.”[1]

Ameipokea Muslim.

Hii ni Hadiyth Qudsiy. Maana yake ni kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kaipokea kutoka kwa Mola Wake (´Azza wa Jall). Imeitwa neno hilo القدس ambalo maana yake ni usafi. Allaah (´Azza wa Jall) ni msafi na ametakasika kutokamana na mapungufu yote. Hadiyth ambayo ni Qudsiy matamshi na maana yake ni kutoka kwa Allaah (´Azza wa Jall), lakini imepokelewa na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Tofauti baina ya Hadiyth kama hiyo na Hadiyth ya kinabii ni kwamba Hadiyth Qudsiy ni ile ambayo matamshi na maana yake vimepokelewa kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Ama Hadiyth ya kinabii ni ile ambayo maana yake ni yenye kutoka kwa Allaah lakini matamshi yake ni yenye kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَا يَنطِقُ عَنِ الْهَوَىٰ إِنْ هُوَ إِلَّا وَحْيٌ يُوحَىٰ

”Hatamki kwa matamanio yake. Hayo ayasemayo si chochote isipokuwa ni Wahy unaofunuliwa kwake.”[2]

Maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Allaah (Ta´ala) amesema… “

Hapa kuna dalili inayoonyesha kuwa Allaah anazungumza kwa njia inayolingana na utukufu Wake (Subhaanahu wa Ta´ala).

Maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika Mimi ni Mwenye kujitosheleza kutohitajia washirika.”

Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) hahitajii ´ibaadah ya viumbe Wake. Amewaamrisha wamwabudu kwa ajili ya manufaa yao wenyewe. Wao ni wenye kumuhitajia Allaah na hakuna chengine kiwezacho kuwakurubisha kwa Allaah isipokuwa ´ibaadah. Kwa hiyo wanamwabudu Allaah kwa ajili ya manufaa yao wenyewe ili Allaah aweze kuwasamehe, awaruzuku na awaingize Peponi. Kwa hiyo manufaa yanarudi kwa waja wenyewe. Kuhusu Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala), haumnufaishi kitu utiifu wa wenye kutii kama ambavyo hayamdhuru kitu maasi ya wenye kuasi. Yeye ndiye mwenye kunufaisha na mwenye kudhuru. Ndio maana Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

إِن تَكْفُرُوا فَإِنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ عَنكُمْ ۖ وَلَا يَرْضَىٰ لِعِبَادِهِ الْكُفْرَ ۖ وَإِن تَشْكُرُوا يَرْضَهُ لَكُمْ

“Mkikufuru, basi hakika Allaah ni mkwasi kwenu, na wala haridhii kwa waja Wake ukafiri na mkishukuru huridhika nanyi.”[3]

وَقَالَ مُوسَىٰ إِن تَكْفُرُوا أَنتُمْ وَمَن فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا فَإِنَّ اللَّـهَ لَغَنِيٌّ حَمِيدٌ

“Muusa akasema: “Mkikufuru nyinyi na wote walioko ardhini, basi hakika Allaah ni mkwasi, Mwenye kustahiki kuhimidiwa.”[4]

Katika Hadiyth ya Qudsiy iliopokelewa na Abu Dharr (Radhiya Allaahu ´anh) imekuja:

“Enyi waja wangu! Lau wa kwanza wenu na wa mwisho wenu, watu wenu na majini wenu, watakuwa kwenye moyo mmoja wa mtu mwema kabisa miongoni mwenu basi hayo yasingezidisha chochote katika ufalme Wangu. Na lau wa kwanza wenu na wa mwisho wenu, watu wenu na majini wenu, watakuwa kwenye moyo mmoja wa mtu muovu kabisa miongoni mwenu basi hayo yasingepunguza chochote katika ufalme Wangu.”[5]

Kwa msemo mwingine watu wenyewe ndio wenye kufaidika kwa kumwabudu Allaah. Ama Allaah (Jalla wa ´Alaa) si muhutaji. Kwa hiyo itakuwa ni jambo lenye haki zaidi kitendo kilichofanywa kwa ajili ya mwengine asiyekuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) kurudishwa. Matendo yanayokubaliwi ni yale masafi tu kwa ajili ya manufaa ya waja. Kujionyesha kunaingia ndani ya maudhui hayo. Allaah anakirudisha kitendo kilichofanywa kwa ajili ya kujionyesha na kwa ajili ya mwengine asiyekuwa Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala). Wala hakikubali. Hiki ndicho kilichokusudiwa katika Hadiyth ilioko kwenye mlango.

 Maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hivyo basi yule atakayefanya kitendo akanishirikisha Mimi pamoja na mwingine, basi nitamwacha yeye na shirki yake.”

Hapa kuna dalili inayoonyesha kuwa shirki inaharibu kitendo, ni mamoja ikawa shirki kubwa au ndogo. Kinachokusudiwa ni kwamba kujionyesha ni aina moja wapo ya shirki inayosababisha kurudishwa nyuma kwa kitendo na kutokukubaliwa na Allaah.

[1] Muslim (2985).

[2] 53:03-04

[3] 39:07

[4] 14:08

[5] Muslim (2577) na Ahmad (21420).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: I´aanat-ul-Mustafiyd bi Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 444-445
  • Imechapishwa: 02/09/2019