08. Sharti ya tano ya swalah


Shaykh-ul-Islaam na Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Sharti ya tano ni kuondosha najisi yote sehemu tatu; kwenye mwili, kwenye nguo na mahala pa kuswalia. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَثِيَابَكَ فَطَهِّرْ

“Nguo zako zisafishe.”[1]

MAELEZO

Mswaliji ni lazima awe msafi kwenye mavazi yake, mwili wake na ile sehemu anayoswalia. Akiswali kwenye nguo ambayo ni najisi, mwili ambao una najisi au sehemu ambayo kuna najisi, basi swalah yake haisihi akiwa ni mwenye kulijua hilo na ni mwenye kukumbuka. Ama akiwa si mwenye kujua hilo na ni mwenye kusahau, basi swalah yake ni sahihi kwa mujibu wa maoni ambayo ni sahihi. Dalili ya hilo ni kwamba wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipokuwa anaswali kwenye viatu vilivyokuwa na uchafu ambapo akaja Jibriyl na kumjuza hilo, alivivua na hakuirudi swalah yake[2]. Dalili nyingine ni ujumla wa maneno ya Allaah (Ta´ala):

رَبَّنَا لَا تُؤَاخِذْنَا إِن نَّسِينَا أَوْ أَخْطَأْنَا

”Ee Mola wetu usituchukulie tukisahau au tukikosea.”[3]

Makusudio ya najisi ni kujiweka nayo mbali na sio kama twahara/wudhuu´. Twahara ni ´ibaadah ambayo inatakikana kwa dhati yake ilihali najisi ni kitu ambacho mtu anatakiwa kujitenga nacho mbali na nguo zake, mwili wake na sehemu. Ndio maana swalah ni sahihi endapo mtu atasahau au akawa hajui juu ya najisi iliyoko kwa mfano nguoni au mwilini mwa mtu. Vivyo hivyo inahusiana na pale mtu ataposwali sehemu ambayo kuna najisi pasi na kujua kuhusu najisi hiyo. Kwa mujibu wa maoni ya sawa ni kwamba swalah yake ni sahihi.

[1] 74:04

[2] Abu Daawuud (650), Ahmad (17/242), Ibn Khuzaymah (2/107), Ibn Hibbaan (5/560) na al-Haakim (1/260) ambaye ameisahihisha. Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Sunan Abiy Daawuud” (657).

[3] 02:286

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ash-Sharh al-Mumtaaz, uk. 79-80
  • Imechapishwa: 27/06/2018