08. Sababu ya nne: mume na mke kupendana na kuoneana huruma

Miongoni mwa sababu za familia kupata furaha ni mtu aipe mapenzi na mahaba. Allaah (´Azza wa Jall) anasema:

وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا لِّتَسْكُنُوا إِلَيْهَا وَجَعَلَ بَيْنَكُم مَّوَدَّةً وَرَحْمَةً

“Miongoni mwa alama Zake ni kuwa amekuumbieni katika jinsi yenu wake ili mpate utulivu kwao na amekujaalieni baina yenu mapenzi na huruma.” 30:21

Katika sababu za familia kupata furaha ni waumini pande zote mbili wafanye bidii ya kupatikana mapenzi na huruma. Uislamu umehimiza kumpenda mke na kustahamili yale maudhi yanayoweza kujitokeza kwake pamoja na kuhifadhi wema wake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Muumini mwanaume asimbughudhi muumini mwanamke. Akichukia kutoka kwake tabia fulani basi kuna nyingine atairidhia.” Muslim (1469).

Hakuna furaha pasi na mapenzi na kuhurumiana. Uislamu umetaja kitu kitachoyatimiza mapenzi haya. Nayo si kingine ni mwanamke mwema. Sa´d bin Abiy Waqqaas (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mambo mane ni katika furaha; mwanamke mwema, makazi mapana, jirani mwema na kipando chenye umakini. Mambo mane ni katika kukosa furaha; jirani mbaya, mwanamke mbaya, makazi ya kubana na kipando kibaya.”

Mambo mane ni katika furaha… – Yazingatieni kwa kuwa ni katika mambo yanayofanya familia kupata furaha.

mwanamke mwema… – Familia inapata furaha kupitia kwake.

makazi mapana… – Familia itaishi ndani yake na kufurahi.

jirani mwema… – Familia itaishi pambezoni mwake ifurahi.

kipando chenye umakini… – Familia itakipanda na kufurahi.

Mambo mane ni katika kukosa furaha… – Bi maana ni katika mambo yanayofanya familia kupata furaha.

mwanamke mbaya… – Huyu ni yule mwanamke muovu asiyekuwa mwema. Familia itakosa furaha kwa sababu yake.

makazi ya kubana… – Familia itakosa furaha kwa sababu yake.

kipando kibaya… – Familia itakosa furaha kwa sababu yake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema akifasiri yaliyotajwa katika Hadiyth hii:

“Mambo matatu ni katika furaha; mwanamke mwema… “

Furaha yake ni ipi?

“… ukimtazama anakupendeza, ukiwa mbali naye una uaminifu naye juu ya nafsi yake na mali yako na kipando kinachokuwa kitiifu… ”

Bi maana kipando kinachokuwa kidhalilifu unachotembea nacho kwa urahisi.

“… kinachokukutanisha na marafiki zako na nyumba inayokuwa pana na urafiki mkubwa. Mambo matatu ni katika kukosa furaha; mwanamke ambaye ukimtazama anakufanya unaona vibaya, anaubeba umili wake dhidi yako, ukiwa mbali naye huna uaminifu naye juu ya nafsi yake na mali yako, kipando kisicho kitiifu ambacho ukikipiga kitakutaabisha na ukikiacha hakitokufanya kukutana na marafiki zako na nyumba ya kubana isiyokuwa na urafiki.” al-Haakim (02/2684) ambaye amesahihisha mlolongo wa wapokezi wake.

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Dunia ni starehe na starehe ilio bora ni mwanamke mwema.” Muslim (1467).

  • Mhusika: Shaykh Sulaymaan bin Saliymillaah ar-Ruhayliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Asbaab sa´aadat-il-Usrah, uk. 30-31
  • Imechapishwa: 08/10/2016