08. Njia ya kwanza: kumtakasia nia Allaah (´Azza wa Jall)

Miongoni mwa njia muhimu zaidi za kujifunza elimu ni kumtakasia nia Allaah (´Azza wa Jall). Tumeshasikia yaliyokuja kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ni jambo lisilokuwa na shaka ya kwamba kuwa na Ikhlaasw ndio msingi wa kila kheri. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anasema:

“Yule ambaye dunia ndio itakuwa nia yake basi Allaah atalifarikisha jambo lake, atauweka ufakiri mbele ya macho yake na hatojiwa na dunia isipokuwa kile Allaah alichomuandikia. Na yule ambaye Aakhirah ndio itakuwa hamu yake kubwa, Allaah atalikusanya jambo lake, atauweka utajiri kwenye moyo wake na atajiwa na dunia hali ni mwenye kutoijali.”[1]

Ambaye sio mwenye kumtakasia Allaah nia Allaah hulifarikisha jambo lake na moyo wake unakuwa hauna utulivu juu ya kitu na Allaah huuweka ufakiri mbele ya macho yake. Wanachuoni wanasema kuwa mtu kama huyo haoni jengine zaidi ya umasikini hata kama hazina zake zitajaa mali na mali. Mtu kama huyu Allaah amemuadhibu na ameuweka ufakiri mbele ya macho yake. Haoni jengine isipokuwa ufakiri na hatojiwa na dunia isipokuwa tu kile alichoandikiwa na Allaah.

Kuhusu ambaye ni mwenye kumtakasia nia Allaah na Aakhirah ndio ikawa hamu yake kubwa, Allaah hulikusanya jambo lake, moyo wake hupata utulivu, moyo wake hupata starehe, jambo lake humkusanyikia mbele yake na Allaah huweka utajiri ndani ya moyo wake. Mtu kama huyu huhisi utajiri kwenye moyo wake na dunia humjia hali ya kuwa si mwenye kuijali. Allaah (´Azza wa Jall) humruzuku kile anachotaka kumruzuku. Ni jambo lisilokuwa na shaka kuwa Ikhlaasw ni miongoni mwa njia kuu za kutafuta elimu.

[1] Ahmad (2159), Ibn Maajah (4105) na Ibn Hibbaan (680). Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “as-Swahiyhah” (405) na (950)

  • Mhusika: Shaykh Sulaymaan bin Saliymillaah ar-Ruhayliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Ilm wa Wasaaailuh wa Thimaaruh
  • Imechapishwa: 22/10/2016