08. Ni wajibu kwa waislamu wote kufuata Qur-aan na Sunnah vyote viwili

Katika hayo kunabainika upotevu wa wanachuoni wa falsafa tangu hapo kale na sasa na kwenda kwao kinyume na Salaf (Radhiya Allaahu ´anhum) katika I´tiqaad zao, sembuse kuhusu hukumu zao, ambapo wanakuwa mbali na Sunnah, kuitambua na kuhukumu akili na matamanio yao katika Aayah za sifa za Allaah na nyenginezo. Ni uzuri uliyoje wa yale yaliyotajwa katika “Sharh-ut-Twahaawiyyah”:

“Ni vipi atazungumza juu ya misingi ya dini yule asiyepokea kutoka katika Qur-aan na Sunnah na kinyume chake anapokea kutoka katika maneno ya fulani? Endapo atadai kuwa anachukua kutoka katika Kitabu cha Allaah basi hapokei tafsiri ya Qur-aan kutoka katika Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), wala hatazami humo na wala katika yale yaliyosemwa na Maswahabah na wale waliowafuata kwa wema ambao wametunukulia kutoka kwa waaminifu wasiokuwa na shaka. Hawakutunakilia ule mpangilio wa Qur-aan peke yake. Bali wametunakilia ule mpangilio wake na maana yake. Isitoshe mambo ni kuwa hawakuwa wakijifunza Qur-aan kama wanavyojifunza watoto. Bali walikuwa wakijifunza nayo kwa maana yake pia. Yule asiyefuata mfumo wao huzungumza kwa maoni yake. Atakayezungumza kwa maoni yake na kwa yale anayodhani kuwa ndio dini ya Allaah na wakati huo huo akawa hakuyapokea hayo kutoka katika Qur-aan ni mwenye kupata dhambi hata kama atapatia. Atakayechukua kutoka katika Qur-aan na Sunnah ni mwenye kupata thawabu hata kama atakosea. Hata hivyo endapo atapatia basi thawabu zake zinalipwa maradufu.”

Kisha akasema:

“Lililo la wajibu ni mtu ajisalimishe kikamilifu kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kunyenyekea amri yake, kuyapokea maelezo yake kwa kuyakubali na kuyasadikisha bila kupingana nayo na fikira batili tutazoziita kuwa ´ni zenye kuingia akilini`, tukayawekea utata, mashaka au tukayatangulizia maoni ya wanaume na takataka ya akili zao. Tunachotakiwa ni kumpwekesha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) inapokuja katika kuhukumu, kujisalimisha na kunyenyekea kama tunavyompwekesha Yule mtumaji (Subhaanahu wa Ta´ala) kwa ´ibaadah, kunyenyekea, kudhalilika, kutubia na kutegemea.”[1]

Kwa kifupi ni kuwa ni wajibu kwa waislamu wote kutotofautisha kati ya Qur-aan na Sunnah inapokuja katika uwajibu wa kuvitendea kazi vyote viwili na kusimamisha uwekaji wa Shari´ah kwa vyote viwili. Hii ndio dhamana kwao ili wasije kupinda kulia na kushoto na wakaja kurejea katika upotevu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameyasema hayo kwa ufaswaha pale aliposema:

“Nimekuachieni mambo mawili ambayo hamtopotea midhali mtashikamana nayo: Kitabu cha Allaah na Sunnah zangu na havitotengana mpaka nijiwe katika hodhi.”

Ameipokea Maalik hali ya kufikishiwa[2], al-Haakim hali ya kuwa ni yenye mlolongo wa wapokezi wenye kuungana[3] kwa isnadi nzuri.

[1] Uk. 217

[2] Balaaghan.

[3] Mawsuul.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Manzilat-us-Sunnah fiyl-Islaam, uk. 16-18
  • Imechapishwa: 10/02/2017