Kutokana na haya tunasema kuwa ni lazima kwa muumini kujiepusha na jambo ambalo shaytwaan anajaribu kulipenyeza akilini mwake, jambo ambalo ni la khatari sana. Jambo hilo ndilo limewafanya Ahl-ul-Bid´ah kuyakengeusha maandiko kwa ajili yake. Jambo hilo analipenyeza shaytwaan ndani ya mioyo ya watu. Nalo ni kule kufikiria namna ya sifa miongoni mwa sifa za Allaah au kufikiria namna ilivyo dhati ya Allaah (´Azza wa Jall).

Tambua kwamba haijuzu kabisa kwa mtu kufikiria namna ilivyo dhati ya Allaah au namna ilivyo sifa yeyote miongoni mwa sifa Zake. Tambua kwamba endapo utafikiria au ukajaribu kufikiria basi ni lazima utumbukie katika moja ya makatazo mawili:

1- Kupotosha na kukanusha.

2- Kufananisha na kushabihisha.

Kwa ajili hiyo ni lazima kwenu kutofikiria chochote katika namna ya sifa za Allaah (´Azza wa Jall). Simaanishi kwamba msithibitishe maana ambayo ni lazima kuithibitisha. Lakini haiwezekani kufikiria namna ya sifa hiyo. Haijalishi kitu ni kwa kipimo gani utapima kipimo hicho. Haiwezekani kamwe kufikiria namna ilivyo sifa ya Allaah (´Azza wa Jall). Ni lazima kwako kujiepusha na jambo hilo. Kwa sababu unajaribu kitu ambacho huwezi kukifikia. Bali unajaribu kitu ambacho kuna khofu kikakutumbukiza katika jambo la khatari ambalo huwezi kujikwamua nalo isipokuwa ima kwa kufananisha au kwa kukanusha. Hayo ni kwa sababu haiwezekani kwa yeyote kumfikiria Mola kwa namna maalum. Endapo utafanya hivo basi umeyaendea yale ambayo huna ujuzi nayo. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَا تَقْفُ مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ

“Wala usifuatilie usiyo na elimu nayo.”[1]

Ukimfikiria kwa wasifu ambao umekaribia kumfananisha basi utakuwa umemfananisha Allaah. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”[2]

Kujengea juu ya haya tunapata kujua kwamba yule mwenye kupinga sifa za Allaah basi amefanya hivo kwa sababu ameanza kuzifikiria kwanza kisha akaona kuwa namna aliyomfikiria inapelekea katika kumfananisha na viumbe. Matokeo yake ndipo akakengeusha.

Kwa ajili hiyo tunasema kuwa kila mwenye kukanusha na mwenye kupinga sifa ni mwenye kufananisha. Kwani kufananisha kwake kumetanguliwa na kukanusha. Alianza kufananisha kwanza ndio baada ya hapo akapinga. Lau angelimuadhimisha Allaah ipasavyo na asijiingize katika mambo ya kufikiria namna zilivyo sifa Zake (Subhaanah) basi asingelihitajia kupinga na kukanusha huku.

[1] 17:36

[2] 42:11

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Manhaj Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah fiy-´Aqiydah wal-´Amal, uk. 15-17
  • Imechapishwa: 06/07/2019