08. Mfano wa tatu kuonyesha jinsi Raafidhwah wanavodai kuwa Maswahabah wamepotosha Qur-aan


al-Qumiy (02/285-286) amesema:

“Amesema:

وَلَمَّا ضُرِبَ ابْنُ مَرْيَمَ مَثَلًا إِذَا قَوْمُكَ مِنْهُ يَصِدُّونَ

“Na alipopigiwa mfano mwana wa Maryam, tahamaki watu wako wanaupigia kelele kuucheka.” (43:57)

Amesema kuwa baba yake alimweleza, kutoka kwa Wakiy´, kutoka kwa al-A´mash, kutoka kwa Salamah bin Kuhayl, kutoka kwa Abu Swaadiq, kutoka kwa Abul-A´azz, kutoka kwa Salmaan al-Faarisiy ambaye amesema: “Wakati ambapo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa amekaa na Maswahabah zake alisema: “Hivi kutakuja mtu anayefanana na ´Iysaa bin Maryam.” Baadhi ya wale waliokuwa wamekaa pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakatoka nje ili wawe yule atayeingia. Hapo ndipo ´Aliy akaingia. Mtu mmoja akawaambia marafiki zake: “Je, Muhammad anaridhia kumchukulia ´Aliy kuwa bora juu yetu ili aweze kufanana na ´Iysaa bin Maryam? Ninaapa kwa Allaah ya kwamba wale tuliokuwa tukiwaabudu katika kipindi cha ushirikina walikuwa ni bora kuliko yeye.” Ndipo Allaah Akawa Ameteremsha:

وَلَمَّا ضُرِبَ ابْنُ مَرْيَمَ مَثَلًا إِذَا قَوْمُكَ مِنْهُ يضجون

“Na alipopigiwa mfano mwana wa Maryam, tahamaki watu wako wanalaumu… ” (43:57)

Wakabadilisha neno “kupiga kelele”:

وَقَالُوا أَآلِهَتُنَا خَيْرٌ أَمْ هُوَ ۚ مَا ضَرَبُوهُ لَكَ إِلَّا جَدَلًا ۚ بَلْ هُمْ قَوْمٌ خَصِمُونَ[1] إن علي إلا عبد أنعمنا عليه وجعلناه مثلا لبني إسرائيل

“… na wakasema: “Je, miungu yetu ni bora au yeye?” Hawakukupigia isipokuwa tu kutaka kujadili. Bali wao ni watu makhasimu!”[2] ´Aliy si chochote isipokuwa ni mja Tuliyemneemesha na Tukamfanya kuwa ni mfano kwa wana wa Israaiyl.”

Wakalitoa jina lake mahala pake.”

1- Allaah Amemtakasa Swahabah mtukufu Salmaan al-Faarisiy na uongo huu na upotoshaji wenye kutia aibu.

2- Si wewe ndiye ulisema kuwa Aayah hii iliteremshwa Makkah? Je, wewe na wengine hamjui kuwa Salmaan aliingia katika Uislamu baada ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhamia al-Madiynah? Allaah Ametaka kukufedhehesha.

3- Maswahabah wanafaidi nini kupotosha neno “kupiga kelele” kwenda “kulaumu”?

4- Unawasemea uongo unaposema kuwa Maswahabah wamesema:

“Ninaapa kwa Allaah ya kwamba wale tuliokuwa tukiwaabudu katika kipindi cha ushirikina walikuwa ni bora kuliko yeye.”

Je, unataka kusema kwamba walikuwa wanaonelea masanamu ni bora kuliko Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au ´Aliy?

5- Manaswara walivuka mipaka kwa ´Iysaa na kusema kuwa ni Allaah, mmoja kwenye utatu au mwana wa Allaah. Ndipo Allaah Alipobainisha ya kwamba ni mmoja katika waja Wake ambaye Amemneemesha kwa unabii, utume na miujiza mikubwa na sivyo kama wanavodai ya kwamba ni mwana wa Allaah wala jengine. Baatwiniyyah wanataka kubadilisha neema hii na kuonekana kuwa ni ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anhu) ndiye kaipata.

6- Kinachotupilia mbali uongo na upotoshaji wenu ni kwamba ´Iysaa ndio makusudio ya Kauli ya Allaah (Ta´ala):

وَجَعَلْنَاهُ مَثَلًا لِّبَنِي إِسْرَائِيلَ

“… na Tukamfanya mfano kwa wana wa Israaiyl.” (43:59)

Allaah Alimfanya ´Iysaa kuwa ni mfano wa wana wa Israaiyl. Bi maana Alimfanya kuwa dalili, hoja na burhani kwa Uwezo wa Allaah kwa vile Alimuumba bila ya baba. Kauli ya Allaah (Ta´ala):

وَإِنَّهُ لَعِلْمٌ لِّلسَّاعَةِ فَلَا تَمْتَرُنَّ بِهَا

“Na hakika yeye [kurudi kwake duniani] ni alama ya [kukurubia kwa] Qiyaamah; basi msiitilie shaka.” (43:61)

inahusiana na ´Iysaa (´alayhis-Salaam) na kwamba atashuka kutoka mbinguni katika zama za mwisho. Kushuka kwake itakuwa ni moja katika alama kubwa za Qiyaamah. Je, mnataka kumpokonya tuzo hili?

7- ´Iysaa alikuwa ni Mtume kwa wana wa Israaiyl tu. Allaah Alimfanya kuwa ni mfumo kwao, bi maana ujumbe na dalili. Ujumbe wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kwa watu wote. Ni vipi ´Aliy atakuwa ni mfano kwa wana wa Israaiyl na isiwe ni Muhammad na ´Iysaa (Swalla Allaahu ´alayhimaa wa sallam)? Je, yeye pia hakuwa ni mfano kwa walimwengu wote?

8- Baatwiniyyah wamepotosha maana na matamshi ya Aayah ili baadaye wawapachike ukafiri huu Maswahabah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Zingatieni, enyi wenye kuona!

[1] 43:58

[2] 43:58

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Intiswaar li Kitaab-il-´Aziyz al-Jabbaar, uk. 38-39
  • Imechapishwa: 19/03/2017