08. Mfano wa kwanza wa hekima ya Mtume (صلى الله عليه وسلم)

Matukio yaliyotokea kwa yule ambaye ndiye kiumbe aliye na hekima zaidi yanafahamisha kutumia hekima wakati wa kulingania katika dini ya Allaah. Naye si mwengine ni Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hebu wacha tupige mifano juu ya hilo.

Mfano wa kwanza: Ni yule mbedui aliyekojoa msikitini.

al-Bukhaariy na Muslim na wengineo wamepokea kupitia kwa Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia ya kwamba kuna mbedui aliyeingia msikitini na akatafuta pembe msikitini kisha akaanza kukojoa. Maswahabah wakapanda juu, wakamkataza na kumfokea. Lakini Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye Allaah amempa hekima ya kulingania katika dini Yake (´Azza wa Jall) akawakataza kumfokea na akawaambia:

“Msimkatikize.”

Bi maana msimkatikize mkojo wake. Pindi mbedui yule alipomaliza kukojoa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaamrisha wamwage ndoo ya maji juu ya ule mkojo. Baada ya hapo akamwita yule mbedui na kumwambia:

“Misikiti hii haisilihi ndani yake kitu katika dhara na taka. Imewekwa kwa ajili ya swalah, kusoma Qur-aan na kumdhukuru Allaah (´Azza wa Jall).”

Au alisema maneno mfano wa hayo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amepokea kuwa mbedui huu alisema:

“Ee Allaah! Nihurumie mimi na Muhammad na usimuhurumie kati yetu mwengine yeyote.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Dawr-ul-Mar´ah fiy Iswlaah-il-Mujtama´ https://www.sahab.net/home/?p=806
  • Imechapishwa: 02/02/2017