08. Maneno yaliyopokelewa kutoka kwa Salaf kuhusu sifa

Kumepokelewa maneno maarufu, ya kijumla na maalum, kutoka kwa Salaf kuhusiana na Aayah na Hadiyth zenye kuzungumzia sifa. Miongoni mwa maneno yao ya kijumla ni:

“Zipitisheni kama zilivyokuja bila ya kuzifanyia namna.”[1]

Haya yamepokelewa kutoka kwa Mak-huul, az-Zuhriy, Maalik bin Anas, Sufyaan ath-Thawriy, al-Layth bin Sa´d na al-Awzaa´iy. Hapa kuna radd kwa Mu´attwilah na Mushabbihah. Katika “zipitisheni kama zilivyokuja… ” wanaraddiwa Mu´attwilah na “… bila ya kuzifanyia namna” wanaraddiwa Mushabbihah. Kadhalika tunaona jinsi Salaf walivyokuwa wakithibitisha maana sahihi ya sifa kwa njia inayolingana na Allaah. Hilo linafahamishwa kwa njia mbili:

Ya kwanza: Maneno yao “Zipitisheni kama zilivyokuja… ” maana yake ni kwamba maana yake inatakiwa kubaki kama ilivyotajwa. Ni jambo lisilokuwa na shaka ya kwamba zimetajwa ili kuthibitisha maana inayolingana na Allaah (Ta´ala). Lau wangelikuwa wanaamini kuwa hazina maana basi wangelisema: “Pitisheni matamshi yake na wala msiingilie maana yake” na mfano wake.

Ya pili: Maneno yao “… bila ya kuzifanyia namna” hii ni dalili ya wazi kuwa maana yake ya kihakika inatakiwa kuthibitishwa. Lau wasingelithibitisha, basi wasingelikuwa na haja ya kukanusha namna. Kwani ambacho hakikuthibitishwa uhakika wa mambo ni kuwa hakina uwepo. Hivyo kukanusha namna ni upuuzi mtupu.

Pengine mtu akauliza maneno ya Imaam Ahmad yana maana gani wakati aliposema kuhusu Hadiyth ya kushuka:

“Tunazithibitisha na kuzisadikisha bila ya namna wala maana.”

Maana iliyokanushwa na Imaam Ahmad ni ile iliyochukuliwa na Mu´attwilah kama Jahmiyyah na wengineo. Walipotosha maandiko ya Qur-aan na Sunnah kutoka katika maana yake ya dhahiri kwenda katika maana inayoenda kinyume nayo. Chenye kuthibitisha hilo, ni yale aliyosema mwandishi kuhusu maneno ya Muhammad bin al-Hasan “Wanachuoni wote wa mashariki na wa magharibi wamekubaliana juu ya kuamini Qur-aan na Hadiyth yaliyosimuliwa na waaminifu kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya sifa za Mola (´Azza wa Jall) bila ya tafsiri, wasifu na ushabihisho”:

“Anamaanisha tafsiri ya Mu´attwilah Jahmiyyah. Wamezusha tafsiri ya sifa yenye kupingana na mfumo wa Maswahabah na Taabi´uun katika kuthibitisha.”[2]

Haya yanatoa dalili kuonyesha kuwa Aayah na Hadiyth zinazozungumzia sifa zinaweza kufasiriwa kwa njia mbili:

Ya kwanza: Tafsiri yenye kukubaliwa. Hii ni ile tafsiri ya Maswahabah na Taabi´uun ambayo inathibitisha maana inayolingana na Allaah (´Azza wa Jall) kutokamana na udhahiri wa Qur-aan na Sunnah.

Ya pili: Tafsiri isiyokubaliwa. Hii ni ile tafsiri yenye kutofautiana na ile tuliyoitaja.

Kwa njia hiyo maana pia inakuwa ima ni yenye kukubaliwa au yenye kurudishwa kutokamana na yale tuliyoyataja.

Mtu akiuliza kama sifa za Allaah zina namna, tutasema kuwa zina namna. Lakini hata hivyo namna hii sisi hatuijui. Ili kuweza kujua namna ya kitu, kunahitajia mtu awe amekwishakiona, kiwe na chenye kufanana nacho au kusikia maelezo ya mkweli juu yacho. Yote haya hayawezekani inapokuja katika sifa za Allaah. Hivyo mtu anapata kujua kuwa maneno ya Salaf “bila ya namna” maana yake ni “bila ya kuzifanyia namna”. Hawakuwa wanamaanisha kuwa hazina namna kwa sababu hiyo maana yake ni kukanusha kutupu.

[1] Tazama ”I´tiqaad Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah” (3/537/930) ya al-Laalakaa’iy, ”Fath-ul-Baariy” (3/407) na wengineo.

[2] Tazama ”Majmuu´-ul-Fataawaa” (5/50) na ”Fath-ul-Baariy” (13/407).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyah, uk. 34-37
  • Imechapishwa: 09/01/2020