Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) anawataka waja Wake wajitenge mbali na chakula, maji na kufanya jimaa katika ile siku waliyofunga. Ina maana ya kwamba ambaye atakula na atakunywa katika siku hiyo basi amefanya dhambi kubwa na ya khatari.

Lakini akila au akinywa kwa kusahau, basi atambue kuwa Allaah ndiye aliyemlisha na kumnywesha. Hata hivyo inamlazimu asiwe alimeza kitu baada ya kukumbuka kuwa amefunga. Mtu akila au akinywa kwa kusahau na akakumbuka kuwa amefunga anatakiwa moja kwa moja kutema kile kitu kilichomo mdomoni mwake. Kile alichomeza kwa kusahau ni mwenye kusamehewa na swawm yake ni kamilifu.

Ambaye anamwingilia mke wake katika kipindi ambacho amefunga amefanya dhambi kubwa. Inamlazimu kafara. Kuna mtu alimjia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia:

“Ee Mtume wa Allaah! Nimeangamia!” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia: “Ni kipi kilichokuangamiza?” Akasema: “Nimemwingilia mke wangu katika Ramadhaan.” Akasema: “Unaweza kupata mtumwa unayeweza kumwacha huru?” Mtu yule akajipiga shingoni mwake na akasema: “Ninaapa kwa Allaah similiki jengine zaidi ya shingo hii.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia: “Basi funga miezi miwili mfululizo.” Mtu yule akasema: “Ni kipi kingine kilichonifanya hivo ikiwa sio swawm?” Bi maana hawezi kumwepuka mke wake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia: “Je, unaweza kuwalisha masikini sitini?” Mtu yule akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Ninaapa kwa Allaah hatukula chakula cha jioni jana usiku.” Mtu yule akaketi chini. Tahamaki akaja mtu na tende takriban 45 kg. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwita mtu yule na akamwambia: “Chukua hizi na uwape masikini sitini.” Mtu yule akasema: “Nimpe mtu ambaye ni fakiri zaidi kuliko mimi? Ninaapa kwa Allaah kwamba hakuna nyumba kati ya miamba miwili hii ambayo ni fakiri kuliko nyumba yangu.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaanza kucheka mpaka magego yake yakaonekana na akasema: “Zichukue wewe na uwalishe familia yako.”

Kwa hiyo mwenye kufanya jimaa na mkewe katika Ramadhaan ni lazima atoe kafara kwa njia iliyotajwa:

1- Kuachia mtumwa huru akiweza.

2- Kufunga miezi miwili mfululizo.

3- Kulisha masikini sitini.

Wanachuoni wamezungumzia juu ya kucheza na mke na kumbusu. Kijana aliye na matamanio mengi akimbusu mke wake na akatokwa na manii, inamlazimu kwake kulipa siku hiyo na haimlazimu kutoa kafara. Asipomwaga, haimlazimu kitu. Lakini ni vizuri kijana asifanye jambo kama hilo ambalo linaweza kupelekea kuiharibu swawm yake. Kuhusu mzee ambaye shahawa zake ni dhaifu, hata na yeye pia lililo bora ni kuepuka na kucheza na kubusu. Lakini iwapo atafanya hivo hakuna kinachomlazimu. Imekuja katika Hadiyth ya kwamba mtu kubusu ilihali amefunga ni kama kusukutua na maji[1]. Lakini kuna wanachuoni wanaosema mtu kucheza na mke na akamwaga inamlazimu kutoa kafara. Wanachuoni wengine wanasema kuwa anachotakiwa ni kuilipa siku hiyo tu na kwamba kafara inatolewa tu wakati wa jimaa. Huenda maoni haya ya mwisho ndio bora zaidi.

Wametofautiana vilevile juu ya makohozi. Kuna wenye kuonelea kuwa swawm inatenguka ikiwa makohozi ni yenye kutoka kichwani. Lakini maoni yanayoonekana kuwa ni sahihi ni kwamba hakuna kinachotengua swawm katika vilivyo ndani ya mwili. Lakini mtu asikusanye mate, makohozi akayameza au mfano wa matendo kama hayo. Linalompasa ni yeye kujitenga mbali na yote haya.

Kujitapikisha kunakata swawm. Mwenye kutapika kwa kukusudia amekata swawm yake tofauti na yule mwenye kutapika pasi na kukusudia. Lakini anatakiwa kuwa makini asimeze kitu katika alivyotapika. Akimeza kitu katika alivyotapika swawm inakatika. Itamlazimu kujizuia siku hiyo na ailipe siku nyingine.

Sindano inayokuwa kwa njia ya mishipa inakata swawm pia. Haijuzu. Sindano inayokuwa kwa njia ya misuli ndio yenye kujuzu kwa mujibu wa maoni sahihi.

Ee waja wa Allaah! Mambo haya yanatakiwa kuepukwa.

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Istiqbaal Shahri Ramadhwaan, uk. 40-44
  • Imechapishwa: 09/06/2017