08. Makatazo ya kuwa kama mayahudi na manaswara waliofarikiana katika dini yao

Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimhu Allaah) amesema:

Ametukataza kuwa kama wale waliotofautiana na wakafarikiana kabla yetu na wakaangamia na akataja kuwa amewaamrisha waislamu kuwa na umoja katika dini na kuwakataza kufarikiana katika hiyo dini. Linazidisha hilo uwazi zaidi kwa yale yaliyokuja katika Sunnah – ni katika ajabu ya maajabu katika hayo.

Halafu jambo la kutofautiana katika misingi na matawi ikawa ndio elimu na uelewa katika dini.

MAELEZO

Ametukataza kuwa kama wale waliotofautiana… – Walipobaki katika tofauti zao wakaangamia na kuchukiana na kupigana vita. Watu wa tofauti wanakuwa namna hii. Ama watu wa mkusanyiko wanakuwa na nguvu na hawawi na vifundo ndani ya mioyo yao:

فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لَا يَجِدُوا فِي أَنفُسِهِمْ حَرَجًا مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُوا تَسْلِيمًا

“Basi Naapa kwa Mola Wako, hawatoamini mpaka wakufanye wewe ni hakimu [mwamuzi] katika yale wanayozozana kati yao, kisha wasipate katika nyoyo zao uzito katika yale uliyohukumu na wajisalimishe ukweli wa kujisalimisha.” (04:65)

Watu hawawi wenye kuridhika na mizozo ikaisha isipokuwa kwa kurejea katika Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Na akataja kuwa amewaamrisha waislamu kuwa na umoja katika dini… – Allaah (Ta´ala) amesema:

شَرَعَ لَكُم مِّنَ الدِّينِ مَا وَصَّىٰ بِهِ نُوحًا وَالَّذِي أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ وَمَا وَصَّيْنَا بِهِ إِبْرَاهِيمَ وَمُوسَىٰ وَعِيسَىٰ ۖ أَنْ أَقِيمُوا الدِّينَ وَلَا تَتَفَرَّقُوا فِيهِ

“Amekuamuruni katika dini yale Aliyomuusia kwayo Nuuh na ambayo tumekuletea Wahy na tuliyomuusia kwayo Ibraahiym na Muusaa na ‘Iysaa kwamba: “Simamisheni dini na wala msifarikiane ndani yake”.” (42:13)

Bi maana isiwe kila mmoja yuko na dini yake. Dini ni moja na hakuna mfarakano.

Linazidisha hilo uwazi zaidi kwa yale yaliyokuja katika Sunnah… – Imethibiti kutoka katika Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo Hadiyth zote zinasisitiza kuwa na umoja na zinakataza mfarakano na tofauti. Kwa mfano Hadiyth ifuatayo:

“Hakika yule atakayeishi muda mrefu katika nyinyi basi ataona tofauti nyingi. Hivyo basi, lazimianeni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu wenye kuongoza…”

Halafu jambo la kutofautiana… – Kule kutofautiana katika misingi na matawi ndio uelewa. Pamoja na kwamba wajibu ni kinyume chake; kuwa na umoja ndio kuwa na uelewa katika dini ya Allaah. Kwa mujibu wao kule kutofautiana na kuwaacha watu wakawa huru na kutowatia uzito ndio uelewa. Sisi tunasema uelewa ni kule kuwa na umoja juu ya Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kuna wanaosema huku ni katika utanukaji wa Uislamu. Bi maana ya kwamba akiwepo mtu mwenye kutuharamishia kitu fulani tunapata mwingine ambaye anakihalalisha. Wamewafanya watu ndio watungaji Shari´ah. Kwa mtazamo wa watu hawa fulani akisema kitu fulani ni halali, basi inakuwa ni halali kwetu hata kama itakuwa ni haramu katika Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume Wake! Tunasema inapaswa kurejea katika Qur-aan. Atayeshuhudiwa kuwa yuko katika haki, sisi tuko nyuma yake. Na yule atayeshuhudiwa kuwa yuko makosani, tunaachana naye. Hili ndio la wajibu.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sittah, uk. 22-23
  • Imechapishwa: 18/05/2021