Dalili za Sunnah juu ya msingi huu mtukufu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Muislamu ni ndugu yake muislamu; hamdhulumu, hamtosi wala hamdharau. Uchaji ni hapa, uchaji ni hapa – akaashiria kifuani mwake. Inatosha shari juu ya mtu kule kumdharau nduguye muislamu. Kila muislamu juu ya muislamu mwenzie ni haramu; damu yake, heshima yake na mali yake.”[1]

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Msifanyiane hasadi, msichukiane, msipelelezane, msifanyiane umbea, msizozane na muwe waja wa Allaah ndugu.”[2]

Amesema tena (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Muumini juu ya muumini ni kama jengo; upande mmoja unaupa nguvu upande mwingine.”[3]

Amesema tena (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumwambia Abu Ayyuub:

“Je, nisikujuze juu ya biashara?” Akasema: “Bali ndio, ee Mtume wa Allaah.” Akasema: “Jaribu kutengeneza kati ya watu wakiharibika na kurubia kati yao wakijitenga mbali.”

Vilevile Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewaamrisha waumini kupendana, kuungana, kupendeana kheri, kusaidiana juu ya wema na kumcha Allaah, kufanya sababu zinazotia hilo nguvu na kulikuza. Upande wa pili Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kila kinachosababisha waislamu kufarikiana na kutengana. Hilo ni kwa sababu katika kufarikiana na kuchukiana kuna maharibifu makubwa. Kufarikina ndio jambo linaloburudisha macho ya mashaytwaan wa kiwatu na wa kijini. Mashaytwaan wa kiwatu na wa kijini hawapendi kuwaona waislamu wako na umoja juu ya jambo. Wanachopenda ni kuwaona wamefarikiana. Kwa sababu wanatambua kwamba kufarikiana kunasambaratisha ile nguvu inayopatikana kwa kushikamana na kumwelekea Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amehimiza kuungana na kupendana kwa maneno na vitendo vyake na amekataza kufarikiana na kutofautiana ambako kunasababisha kufarikisha umoja na kuondoka kwa ile nguvu.

[1] al-Bukhaariy (6951) na Muslim (2564).

[2] al-Bukhaariy (6064) na Muslim (2563).

[3] al-Bukhaariy (6026) na Muslim (2563).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sittah, uk. 14-15
  • Imechapishwa: 17/06/2021