08. Kuswali ´iyd uwanjani kwa sababu ya ufinyu wa nafasi msikitini

Hivi ndivo walivosema, lakini ni jambo linatakiwa kujadiliwa. Lau mambo yangelikuwa hivyo wanavyosema, basi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) asingelikuwa siku zote anaswali mahali pa uwanja, kwa sababu hakuwa ni mwenye kuendelea kulazimiana na jambo isipokuwa tu ikiwa kama ni kibora.

Kusema kuwa alifanya hivo kwa sababu ya kujibana kwa msikiti, ni madai yasiyokuwa na dalili yoyote. Linalotilia nguvu hilo ni kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiswali swalah ya Ijumaa msikitini. Watu walikuwa wakija kutoka pande mbalimbali za Madiynah na kwenginepo na akiswali pamoja nao swalah ya Ijumaa ndani yake. Hakudhihiri tofauti yoyote kati ya idadi ya Maswahabaha wanaohudhuria swalah ya Ijumaa na idadi ya wanaokuja katika swalah za ´Iyd mpaka mtu aseme kwamba nafasi ilikuwa ni yenye kuwatosha wale na haiwatoshi hawa. Mwenye kudai kinyume na haya basi ni lazima kwake kuleta dalili, jambo ambalo sidhani kuwa analiweza.

Lau swalah za ´Iyd ingelikuwa ni bora kuziswali msikitini kuliko mahali pa uwanja na wakati huohuo msikiti kukawa na nafasi finyu, basi (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) angelikimbilia kuupanua kama walivyofanya baadhi ya makhaliyfah wake baada yake, jambo ambalo yeye alikuwa ana haki zaidi ya kulifanya kuliko wao. Ni jambo lisiloweza kufikiriwa kuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliacha kupanua baada ya kukubaliana na fadhila zilizotajwa. Isipokuwa hilo linaweza kukwepwa kwa kusema ya kwamba kulikuwepo kizuizi kilichofanya kusifanyike hilo, lakini sidhani kama kuna mwanachuoni anaweza kuthubutu kutamka madai kama hayo. Endapo atafanya hivo, tutakabiliana naye kwa maneno ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala):

هَاتُواْ بُرْهَانَكُمْ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ

“Leteni ushahidi wenu wa wazi mkiwa ni wakweli.”[1]

[1] 02:111

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swalaat-ul-´Iydayn, uk. 22-23
  • Imechapishwa: 13/05/2020