08. Kumekanushwa ufanano na zimethibitishwa sifa

Kuthibitisha majina na sifa za Allaah hakupelekei kabisa kufanana kama wanavoona Mu´attwilah na Mu´awwilah. Hayo yanatokana na upungufu wa uelewa wao, upotofu wao na kutoitaka haki. Kila mmoja anajua kwamba kuna tofauti kati ya viumbe na Muumba (Subhaanahu wa Ta´ala). Tofauti iliopo mpaka kwa viumbe wenyewe. Kwa mfano ndovu sio kama paka japokuwa wanashirikiana katika baadhi ya sifa. Mbu anasikia na farasi anasikia, mbu anaona na ndovu na farasi wanaona. Je, hayo yanapelekea kwamba mbu ni kama ndovu au farasi? Hapana. Japokuwa majina ni yenye kushirikiana lakini hawashirikiani katika uhakika na namna. Ni vipi tofauti kati ya Muumbaji na viumbe ikiwa tofauti ni kubwa namna hii kati ya viumbe?

Sisi tunamthibitishia Allaah yale aliyojithibitishia Mwenyewe na yale aliyomthibitishia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pasi na kupotosha, kukanusha, kuzifanyia namna wala kufananisha. Amesema (Ta´ala):

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”[1]

Amekanusha ufanano na akathibitisha kusikia na kuona. Hiyo imefahamisha kwamba kuthibitisha kusikia na kuona hakupelekei ufanano:

فَلَا تَضْرِبُوا لِلَّـهِ الْأَمْثَالَ

”Basi msimpigie Allaah mifano!”[2]

Hakuna kiumbe yeyote anayefanana na Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

[1] 42:11

[2] 16:74

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: I´aanat-ul-Mustafiyd bi Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 24-25
  • Imechapishwa: 07/08/2019