Lengo la nane: Kukumbuka hali za Mitume

Miongoni mwa malengo makubwa ya hajj ni kukumbuka hali za Manabii na historia za Mitume wa Allaah – swalah na salaam ziwe juu yao wote. Hajj imejaa visimamo, nembo na alama mbalimbali kuu ambazo zinamkumbusha muumini juu ya Mitume wa Allaah. Ardhi hii ambayo Allaah ametukirimu na tunatoka sehemu moja ya ´ibaadah kwenda sehemu nyingine, matendo haya ya ´ibaadah kutoka sehemu moja kwenda kwenye mengine, waliwahi kuyakanyaga kabla yetu Mitume na Manabii wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam). Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mitume sabini waliswali katika msikiti wa Khayf.”[1]

Walikuja katika ardhi hii iliyobarikiwa viumbe watakasifu zaidi wa Allaah kabla ya wewe kuja katika matendo mema haya. Unatakiwa kuyahisi haya, kuingie ndani zaidi moyoni mwako kule kufungamana kwako na Mitume wa Allaah, ufuate mfumo wao na ufuate nyayo zao. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ هَدَى اللَّـهُ ۖ فَبِهُدَاهُمُ اقْتَدِهْ

“Hao ndio ambao Allaah amewaongoza, basi fuata mwongozo wao.”[2]

Kumbukumbu hizi kuu zinakujia wewe katika matendo yote ya hajj:

1- Unapokuja katika Nyumba ya Allaah basi unatakiwa kukumbuka kwamba yule aliyeijenga Nyumba ni kipenzi wa Allaah Ibraahiym na Ismaa´iyl (Swalla Allaahu ´alayhimaa wa sallam):

وَإِذْ يَرْفَعُ إِبْرَاهِيمُ الْقَوَاعِدَ مِنَ الْبَيْتِ وَإِسْمَاعِيلُ رَبَّنَا تَقَبَّلْ مِنَّا

“Pindi aliponyanyua Ibraahiym na Ismaa’iyl msingi wa Nyumba: “Ee Mola wetu! Tutakabalie! Hakika Wewe ni Mwenye kusikia, Mjuzi wa yote.”[3]

2- Utapomaliza kufanya Twawaaf basi pafanye pale mahali pa kusimama Ibraahiym (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwa ni mahali pa kuswali. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَاتَّخِذُوا مِن مَّقَامِ إِبْرَاهِيمَ مُصَلًّى

“Fanyeni mahali pa kusimama Ibraahiym kuwa ni sehemu ya kuswalia.”[4]

3- Utapokunywa zamzam na ukafanya Sa´y baina ya Swafaa na Marwah, basi hayo yatakukumbusha kisa cha Haajar. Mwanamke huyo ambaye alikuwa ni muumini, mkweli na mwenye kumtegemea Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) wakati ambapo Ibraahiym (´alayhis-Salaam) alipokuja naye sehemu hii na baadaye akataka kwenda zake na kumwacha yeye na mtoto wake peke yao katika bonde lisilokuwa na mimea. Haajar akamwambia:

“Ni nani aliyekuamrisha uniache sehemu ambayo hakuna mnyama, mmea, mtu wa karibu wa kuzungumza naye, masurufu wala maji?” Akasema: “Mola wangu ndiye kaniamrisha.” Haajar akasema: “Basi hatotuacha bure.”

Mwanamke huyo muumini na ambaye anamtegemea Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) akabaki peke yake sehemu hiyo. Baadaye alipohisi kiu sana na akachelea juu ya mtoto wake asije kufa, ndipo akapanda mlima wa Swafaa akitafuta maji na mara anaenda Marwah akitafuta maji halafu anarudi tena Swafaa. Anaposhuka chini kwenye mlima anatembea kwa haraka na kukaza mwendo. Ndipo Allaah akaidhinisha kutokeze chemchem ya maji ya zamzam na yakabaki tokea kipindi hicho kuwa ni maji yaliyobarikiwa. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu maji ya zamzam:

“Hakika ni yenye baraka. Ni chakula chenye kushibisha na ni ponyo kwa maradhi.”

“Maji ya zamzam ni kwa ile nia iliyonywewa.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alijimwagia kichwani mwake. Aliyabeba na kwenda nayo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hakika ni maji yenye baraka. Ulimwenguni kote hakuna maji mazuri, yenye manufaa na yenye baraka zaidi kama hayo.

Baada ya hapo ikawa kutembea (Sa´y) baina ya Swafaa na Marwah ni nembo miongoni mwa nembo za Allaah na moja katika matendo mema tangu hayo yafanywe na mwanamke huyu muumini. Mpaka Mitume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) walikuwa wakifanya Sa´y sehemu hiyo.

4- Utapoenda ´Arafah ipo Hadiyth ya kwamba (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema kuwaambia Maswahabah:

“Kuweni katika sehemu zenu za ´ibaadah. Kwani hakika mko katika urathi miongoni mwa urathi wa baba yenu Ibraahiym (´alayhis-Salaam).”

Mitume hawakurithisha dinari wala dirhamu. Walichorithisha ni dini ya Allaah. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Du´aa bora ni du´aa ya siku ya ´Arafah. Bora niliyosema mimi na Mitume wengine kabla yangu ni ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah, hali ya kuwa pekee hana mshirika, ufalme ni Wake Yeye na himdi zote ni Zake Yeye. Naye juu ya kila jambo ni muweza`.”[5]

5- Utaporusha vijiwe basi hayo yanakukumbusha asili ya kurusha mawe. Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba amesema:

“Wakati Ibraahiym, kipenzi wa hali ya juu wa Allaah, alipoenda zile sehemu za ´ibaadah katika hajj basi shaytwaan akajidhihirisha kwake katika nguzo ya ´Aqabah. Akamtupia vijiwe saba mpaka akadidimia chini ardhini. Kisha akajidhihirisha kwake tena katika ile nguzo ya pili ambapo akamrushia vijiwe saba mpaka akadidimia chini ardhini. Halafu akajidhihirisha kwake tena katika ile nguzo ya tatu ambapo akamrushia vijiwe saba mpaka akadidimia chini ardhini.”[6]

Hiyo ikawa ni moja katika nembo kuu za hajj zinazofanywa na waumini katika hajj zao katika Nyumba ya Allaah (´Azza wa Jall) kwa ajili ya kusimamisha ukumbusho wa Allaah.

6- Katika kuchinja wanyama inakukumbusha kile kisa muhimu na cha ajabu wakati Ibraahiym (´alayhis-Salaam) alipoota usingini kwamba anamchinja mwanae Ismaa´iyl (´alayhis-Salaam). Akamtaka ushauri juu ya hilo:

قَالَ يَا أَبَتِ افْعَلْ مَا تُؤْمَرُ ۖسَتَجِدُنِي إِن شَاءَ اللَّـهُ مِنَ الصَّابِرِينَ فَلَمَّا أَسْلَمَا وَتَلَّهُ لِلْجَبِينِ

“Akasema: “Ee baba yangu! Fanya yale uliyoamrishwa. Utanikuta – Allaah akitaka – ni miongoni mwa wenye kusubiri.” Basi wote wawili walipojisalimisha na akamlaza kifudifudi juu ya kipaji.”[7]

Akaenda na mtoto wake akiwa na kisu na akaweka kisu shingoni mwake kutaka kumchinja – yote hayo wanajisalimisha wote wawili na amri ya Allaah – ndipo Allaah akamkomboa kwa kumleta kondoo aliyenona.

Matendo yote haya yanakumbushia Mitume wa Allaah. Matokeo yake yule mwenye kuhiji anatoka katika hija yake akiwa na jumla nzuri na kumbukumbu nzuri zinazomfungamanisha na viumbe wakatasifu zaidi ambao ni Manabii na Mitume wa Allaah ambao ndio viumbe wema na wabora zaidi wa Allaah. Sambamba na hilo huku akihisi mienendo yao, mifumo yao pamoja na kulazimiana na matendo yao – swalah na salaam ziwaendee wote pamoja na wale watakaowafuata kwa wema.

Kwa ajili hii unatakiwa kumshukuru Allaah (´Azza wa Jall) kukufanya kuwa ni katika warithi wa Mitume hali ya kuwa ni mwenye kufuata mfumo wao, kupita juu ya njia yao na kufuata nyayo zao. Hii ni fadhilah na neema ya Allaah kwako. Haya yanamfanya mja kuzidi kutilia umuhimu njia hii na kufuata mfumo huu na khaswakhaswa inapokuja katika Tawhiyd, ´Aqiydah na kumtakasia nia Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Mtume wetu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mitume ni kama ndugu kwa baba. Mama zao wako mbalimbali lakini baba yao ni mmoja.”[8]

Bi maana ´Aqiydah yao ni moja na Shari´ah zao ni zenye kutofautiana.

Mja atilie umuhimu ´Aqiydah hii iliyonyooka na sahihi. Atilie umuhimu vilevile Tawhiyd hii takasifu ambayo ndio mfumo wa Mitume na msingi wa ulinganizi wao.

[1] al-Haakim katika ”al-Mustadrak” (4228), at-Twabaraaniy katika ”al-Mu´jam al-Kabiyr” (12283).

[2] 06:90

[3] 02:127

[4] 02:125

[5] at-Tirmidhiy katika ”Jaamiy´” yake (3585). Ni nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”as-Swahiyhah” (1503).

[6] al-Haakim (1715) ambaye ameisahihisha na adh-Dhahabiy akaafikiana naye. Tazama ””Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb” (1156) ya al-Albaaniy.

[7] 37:102-103

[8] al-Bukhaariy (3443) na Muslim (2365).

  • Mhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Maqaaswid-ul-Hajj, uk. 37-44
  • Imechapishwa: 20/08/2018