5- Wanatakiwa waharakishe kumwandaa na kumtoa kikihakikishwa kifo chake. Hayo ni kutokana na Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Liharakisheni jeneza… “

Ukamilifu wake utakuja katika kipengele cha 47.

Katika mlango huu zipo Hadiyth zengine mbili zinazosema kwa uwazi zaidi kuliko hii. Lakini hata hivyo ni dhaifu na ndio maana tukaziacha.

Kuhusu Hadiyth ya kwanza ni kutoka kwa Ibn ´Umar aliyeirufaisha na tamko lake linasema:

“Anapokufa mmoja wenu msimzuie. Muharakisheni kwenda kaburini mwake. Asomewe upande wa kichwa chake [Aayah za] mwanzomwanzo za al-Baqarah na upande wa miguu yake [asomewe Aayah za] mwishomwisho wake.”

Ameipokea at-Twabaraaniy “al-Mu´jam al-Kabiyr” (03/208/02), al-Khallaal katika “al-Qiraa-atu ´indal-Qubuur” (02/25) kupitia kwa njia ya Yahyaa bin ´Abdillaah bin adh-Dhwahhaaq al-Baabulutiy ametuhadithia Ayyuub bin Nuhayk al-Halabiy az-Zuhriy – mtumwa aliyeachwa huru na Sa´d bin Abiy Waqqaas – aliyesema: “Nimemsikia ´Atwaa´ bin Abiy Rabaah al-Makkiy ambaye amesema: “Nimemsikia Ibn ´Umar akisema: “Akaitaja.”

Cheni ya wapokezi hii ni dhaifu sana. Ina kasoro mbili:

Ya kwanza: al-Baabulutiy ni dhaifu, kama alivosema al-Haafidhw katika “at-Taqriyb”.

Ya pili: Mwalimu wake, ambaye ni Ayyuub bin Nuhayk, yeye ni mdhaifu zaidi kuliko. Abu Haatim na wengineo wamemdhoofisha. al-Azdiy amesema:

“Ni mwenye kuachwa.”

Abu Zur´ah amesema:

“Hadiyth zake ni munkari.”

al-Haafidhw ameiwekea mlolongo wa Hadiyth nyingine katika “al-Lisaan” ambayo umunkari wake uko wazi kupitia kwa Yahyaa bin ´Abdillaah aliyesema: “Ayyuub ametuhaditia, kutoka kwa Mujaahid, kutoka kwa Ibn ´Umar aliyerufaisha. Kisha akasema:

“Yahyaa ni dhaifu. Lakini hili haliwezekani kwake.”

Ukishayajua haya basi utashangazwa na al-Haafidhw pale aliposema katika “al-Fath” (03/143) kuhusu Hadiyth ya at-Twabaraaniy hii:

“Cheni ya wapokezi wake ni nzuri (Hasan).”

ash-Shawkaaniy pia akamnukuu katika “Nayl al-Awtwaar” (03/309) na akamkubalia.

Kuhusu al-Haythamiy amesema “al-Mujma´” (03/44):

“Ameipokea at-Twabaraaniy katika “al-Kabiyr”. Ndani yake yumo Yahyaa bin ´Abdillaah al-Baabulutiy ambaye ni dhaifu.”

Alipitwa kwamba ndani yake yumo vilevile Ayyuub Nuhayk ambaye ni muovu zaidi kuliko yeye, kama ilivyotangulia.

Kuhusu Hadiyth ya pili ni kutoka kwa Huswayn bin Wahwah:

“Kwamba Twalhah bin al-Baraa´ aligonjweka. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamjia kumtembelea. Akasema: “Mimi sioni vyengine isipokuwa Twalhah amekwishafikwa na mauti. Nijulisheni kuhusu yeye ili nihudhurie kwake na kumswalia. Mumuharakishe. Kwani haitakikani kwa kiwiliwili cha muislamu kizuiliwe kati ya watu wake.”

Ameipokea Abu Daawuud na al-Bayhaqiy (03/386-387). Ndani yake yumo ´Arwah. Huitwa pia ´Azrah bin Sa´iyd al-Answaariy kutoka kwa baba yake. Wote wawili hawajulikani, kama alivosema al-Haafidhw katika “at-Taqriyb”.

Jengine ni kwamba kutumia kwetu dalili kwa Hadiyth ya Abu Hurayrah juu ya yale tuliyoyataja ni kujengea kwamba makusudio ya:

“Liharakisheni”

ni kuharakisha kumwandaa. Kuhusu maoni yanayosema kuwa kinacholengwa ni kuharakisha wakati wa kumbeba kwenda kwenye kaburi lake, hakutimii dalili yake. Maoni haya ndio ambayo al-Qurtwubiy ameiona iko wazi, kisha an-Nawawiy. al-Haafidhw [Ibn Hajar] ametia nguvu maoni ya kwanza kwa Hadiyth mbili tulizozizungumzia punde tu. Hayafichikani yaliyomo ndani yake.

Ipo Hadiyth ya tatu ambayo inajulikana sana kwa watu wa kawaida. Nayo inasema:

“Kumkirimu maiti ni kumzika.”

Haina msingi wowote. Kama ilivyo katika “al-Maqaaswid al-Hasanah” (nambari. 151) cha as-Sakhaawiy.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 23-24