999- Ameeleza vilevile kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Umekujieni mwezi wa Ramadhaan – ni mwezi wenye baraka. Allaah amekufaradhishieni kufunga. Ndani yake milango ya Pepo hufunguliwa, milango ya Moto hufungwa na mashaytwaan waovu hutiwa pingu. Humo Allaah ana usiku ambao ni bora kuliko miezi elfu moja. Mwenye kunyimwa kheri zake kwa kweli amenyimwa.”[1]

Ameipokea an-Nasaa´iy na al-Bayhaqiy kupitia kwa Abu Qilaabah, kutokak wa Abu Hurayrah. Kutokana na ninavyojua hakusikia kutoka kwake. al-Haliymiy amesema:

“Mashaytwaan kutiwa pingu inawezekana kunakusudiwa michana yake tu. Huoni kama amesema wale mashaytwaan waasi? Kwa sababu katika Ramadhaan ndio Qur-aan ilikuwa ikiteremshwa katika mbingu ya dunia ambapo ikilindwa na vimondo vya moto. Amesema (Ta´ala):

وَحِفْظًا مِّن كُلِّ شَيْطَانٍ مَّارِدٍ

”Hifadhi dhidi ya kila shaytwaan asi.” (37:07)

Katika mwezi wa Ramadhaan kunazidishwa usalama zaidi kwa pingu – na Allaah ndiye anajua zaidi.

Kuna uwezekano vilevile ikawa Ramadhaan na wakati mwingine. Maana yake ni kwamba mashaytwaan wanashindwa kuwaharibu watu kama wanavofanya wakati mwingine. Kwa sababu waislamu wanajishughulisha na swawm ambayo inaponda matamanio yao, kisomo cha Qur-aan na ´ibaadah nyenginezo.

[1] Swahiyh kupitia zengine.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Adhwiym bin ´Abdil-Qawiy al-Mundhiriy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb (1/585-586)
  • Imechapishwa: 26/05/2018
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy