08. ´Aqiydah ya Ibn ´Abdil-Wahhaab juu ya sifa sifa za Allaah


Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

“Sizifanyii namna na wala sizifananishi sifa Zake (Ta´ala) na sifa za viumbe Wake. Kwa sababu Yeye (Ta´ala) hana anayelingana Naye, mwenza, mshirika na wala halinganishwi na viumbe Wake. Hakika (Subhaanah) ni Mwenye kujijua zaidi na Yeye na wengineo na ni mkweli zaidi katika maneno na katika mazungumzo.”

MAELEZO

Hili ni fungu la pili la upotevu katika majina na sifa Zake: Mumaththilah. Wamezidisha katika kuthibitisha na wakapindukia katika kuthibitisha. Hawakutofautisha kati ya sifa za Allaah na sifa za viumbe Wake. Hawakutofautishi kati ya majina Yake na majina ya viumbe Wake. Hawa ndio washabihishaji. Kwa ajili hii ndio maana wanachuoni wakasema:

“Mkanushaji anaabudu kitu kisichokuweko na mfananishaji anaabudu sanamu.”[1]

Waliposema kuwa mkanushaji anaabudu kitu kisichokuweko ni kwa sababu ambacho hakina majina wala sifa ni kitu kisichokuweko. Upande wa pili mfananishaji anaabudu sanamu katika watu. Kwa sababu amemfanya Allaah kama mtu – Allaah (Ta´ala) ametakasika kutokamana na hilo.

Sizifanyii namna… – Sijui namna wala mfano wake. Haya ni miongoni mwa ujuzi wa Allaah (Jalla wa ´Alaa). Hakuna ajuaye namna ya sifa Zake isipokuwa Yeye Mwenyewe na wala hakuna ajuaye namna ilivyo dhati Yake isipokuwa Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala):

يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ وَلَا يُحِيطُونَ بِهِ عِلْمًا

“Anajua yale yaliyoko mbele yao na yale yaliyoko nyuma yao na wala hawawezi kumzunguka Yeye wote kiujuzi.”[2]

Waumini wanamjua Mola wao na kwamba Yeye ndiye Mola na Muumbaji wao na wanatambua uwepo na ukamilifu Wake. Lakini hawamzunguki Yeye wote kiujuzi.

Hana anayelingana Naye – Bi maana hakuna yeyote anastahiki jina Lake kikweli. Haina maana kwamba hakuna yeyote anayeitwa kwa jina Lake. Kwa sababu viumbe huitwa “al-´Aziyz”, “al-Malik” na majina mengine ambayo yanayokutana na majina ya viumbe kiherufi na kimaana. Lakini hayakutani katika namna. Kwa hiyo maana ya hana anayelingana Naye ni kwamba hakuna yeyote anayestahiki jina Lake kikweli. Amesema (Ta´ala):

فَاعْبُدْهُ وَاصْطَبِرْ لِعِبَادَتِهِ ۚ هَلْ تَعْلَمُ لَهُ سَمِيًّا

“Hivyo basi mwabudu Yeye tu na dumisha subira katika kumwabudu. Je, unamjua yeyote mwenye jina kama Lake?”[3]

Bi maana hakuna yeyote anayelingana na Allaah (Jalla wa ´Alaa) katika majina na sifa Zake.

Mwenza – Amesema (Ta´ala):

وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ

”Wala hakuna yeyote anayefanana na kulingana Naye.”[4]

Bi maana hakuna yeyote anayelingana Naye (Jalla wa ´Alaa).

Mshirika – Mshirika ndio huyohuyo anayelingana Naye:

وَجَعَلُوا لِلَّـهِ أَندَادًا

“Wakamfanyia Allaah walinganishi.”

Wingi wa mwenza. Ni anayelingana Naye:

وَجَعَلُوا لِلَّـهِ أَندَادًا لِّيُضِلُّوا عَن سَبِيلِهِ ۗ قُلْ تَمَتَّعُوا فَإِنَّ مَصِيرَكُمْ إِلَى النَّارِ

“Wakamfanyia Allaah walinganishi ili wapoteze watu kutokamana na njia Yake. Sema: ”Burudikeni! Kwani hakika mahali penu pa kurudia mwishoni ni Motoni.”[5]

Wale walioabudu masanamu wamemfanyia Allaah washirika wakimshabihisha Naye (Subhaanahu wa Ta´ala). Vinginevyo ni kwa nini wamewaabudu pamoja Naye? Kwa ajili hiyo siku ya Qiyaamah watasema:

تَاللَّـهِ إِن كُنَّا لَفِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ إِذْ نُسَوِّيكُم بِرَبِّ الْعَالَمِينَ

”Naapa kwa Allaah! Hakika tulikuwa katika upotevu wa wazi, pindi tulipokusawazisheni na Mola wa walimwengu.”[6]

Watakubali kwamba waliyalinganisha na Mola wa walimwengu huko duniani. Hivyo wakawa ni wenye kustahiki Moto siku ya Qiyaamah. Amesema (Ta´ala):

الَّذِينَ كَفَرُوا بِرَبِّهِمْ يَعْدِلُونَ

“Wale ambao wamekufuru wanawasawazisha wengine na Mola wao.”

Maneno Yake:

يَعْدِلُونَ

“Wanawasawazisha.”

Bi maana wanamlinganisha na wengineo katika viumbe.

Halinganishwi na viumbe Wake – Yeye (Subhaanah) halinganishwi na viumbe Wake katika majina na sifa Zake. Majina na sifa, ingawa ni vyenye kushirikiana katika matamshi na jumla ya maana, lakini ni vyenye kutofautiana katika uhakika na namna.

Hakika (Subhaanah) ni Mwenye kujijua zaidi… – Yeye ni Mwenye kujijua zaidi. Kuhusu wengine hawajui kuhusu Allaah isipokuwa yale Allaah (Jalla wa ´Alaa) aliyowafunza. Malaika walisema:

سُبْحَانَكَ لَا عِلْمَ لَنَا إِلَّا مَا عَلَّمْتَنَا

“Utakasifu ni Wako hatuna elimu isipokuwa Uliyotufunza.”[7]

Allaah (Jalla wa ´Alaa) anasema kumwambia Mtume Wake:

وَقُل رَّبِّ زِدْنِي عِلْمًا

”Sema: “Mola wangu! Nizidishie elimu.”[8]

Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

وَفَوْقَ كُلِّ ذِي عِلْمٍ عَلِيمٌ

”Na juu ya kila mwenye elimu yuko mwenye elimu zaidi.”[9]

وَمَا أُوتِيتُم مِّنَ الْعِلْمِ إِلَّا قَلِيلًا

“Hamkupewa ujuzi isipokuwa kidogo tu.”[10]

Yeye (Subhaanah) ni Mwenye kujijua zaidi Yeye na wengineo. Kuhusu wengine hakuna anayejua uhakika wa Allaah wala namna Allaah (Jalla wa ´Alaa) alivyo. Hakuna ayajuaye isipokuwa Allaah pekee (Subhaanahu wa Ta´ala).

Ni mkweli zaidi katika maneno na katika mazungumzo – Imetajwa katika Qur-aan:

وَمَنْ أَصْدَقُ مِنَ اللَّـهِ قِيلًا

“Na nani mkweli zaidi kwa kauli kuliko Allaah?”[11]

وَمَنْ أَصْدَقُ مِنَ اللَّـهِ حَدِيثًا

”Na nani mkweli zaidi katika mazungumzo kuliko Allaah?”[12]

Hakuna aliye mbora zaidi kumshinda Allaah wala aliye mkweli zaidi kumshinda Allaah. Allaah amesema katika Kitabu Chake kwamba ni Mwenye kusikia, kwamba ni Mwenye kuona, kwamba ni Mwenye hekima, kwamba ni mjuzi wa kila jambo, kwamba ana uso na kwamba ana mikono. Ameyasema haya juu Yake Mwenyewe (Subhaanahu wa Ta´ala). Kwa hivyo Yeye ndiye mjuzi zaidi wa nafsi Yake. Halafu wanakuja Mu´ttwilah hawa na kusema kwamba mambo haya hayaendani na Allaah. Wanasema kuwa hailingani kusema juu ya Allaah kwamba anao uso, anayo mikono, kwamba anasikia na kwamba anaona. Hoja yao ni kwamba eti sifa hizi zinapatikana kwa viumbe na tukizithibitish tutakuwa tumemfananisha Allaah na viumbe Wake.

[1] Tazama ”al-Jawaab-us-Swahiyh” (04/406), “Minhaaj-us-Sunnah an-Nabawiyyah” (02/526) na “Majmuu´-ul-Fataawaa” (05/196) vya Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah na “as-Swawaa´iq al-Mursalah” (01/148) cha Ibn-ul-Qayyim.

[2] 20:110

[3] 19:65

[4] 112:04

[5] 14:30

[6] 26:97-98

[7] 02:32

[8] 20:114

[9] 12:76

[10] 17:85

[11] 04:122

[12] 04:87

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 24-26
  • Imechapishwa: 03/03/2021