08. Aina mbili za uongofu


Akamwongoza amtakaye kutokana na fadhilah Zake… – Mitume wamebainisha, Vitabu vya kiungu pia vimebainisha, lakini hatimaye Allaah ndiye humwongoza amkaye.

Kuna aina mbili ya uongofu:

1- Uongofu kwa njia ya maelekezo. Uongofu huu umemfikia kila mtu. Allaah amewaelekeza waja juu ya yale yenye kheri na akawaamrisha kuifuata, na pia amewaelekeza juu ya yale yenye shari na akawakataza kuifuata.

2- Uongofu kwa njia ya kuwafikishwa. Uongofu aina hii unakuwa kwa waumini peke yao. Waumini ambao wameikubali haki, wakaifanyia bidii na wakaitendea kazi. Ndio maana Allaah (´Azza wa Jall) akasema:

إِنَّكَ لَا تَهْدِي مَنْ أَحْبَبْتَ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ يَهْدِي مَن يَشَاءُ ۚ وَهُوَ أَعْلَمُ بِالْمُهْتَدِينَ

”Hakika wewe huwezi kumwongoza umpendaye, lakini Allaah humwongoza amtakaye; Naye ndiye mjuzi zaidi ya waongokao.”[1]

Bi maana huongozi uongofu wa kuwafikisha. Kuhusu uongofu wenye kuenea ambao ni ule uongofu wa maelekezo umemfikia kila mmoja. Amesema (Ta´ala):

وَأَمَّا ثَمُودُ فَهَدَيْنَاهُمْ فَاسْتَحَبُّوا الْعَمَىٰ عَلَى الْهُدَىٰ

“Na ama kina Thamuud, tuliwaongoza, lakini walipendelea upofu kuliko uongofu.”[2]

إِنَّا خَلَقْنَا الْإِنسَانَ مِن نُّطْفَةٍ أَمْشَاجٍ نَّبْتَلِيهِ فَجَعَلْنَاهُ سَمِيعًا بَصِيرًا إِنَّا هَدَيْنَاهُ السَّبِيلَ إِمَّا شَاكِرًا وَإِمَّا كَفُورًا

”Hakika Sisi tumemuumba mtu kutokana na tone la manii iliyochanganyika ili tumjaribu, tukamjaalia mwenye kusikia na kuona. Hakika Sisi tumemuongoza njia, ima awe ni mwenye kushukuru au mwenye kukufuru.”[3]

Bi maana tumemuelekeza katika ambayo ni kheri na ambayo ni shari. Huu ni uongofu kwa njia ya mabainisho na maelekezo. Ni uongofu wenye kumfikia kila mtu. Amesema (Ta´ala):

وَلَـٰكِن جَعَلْنَاهُ نُورًا نَّهْدِي بِهِ مَن نَّشَاءُ مِنْ عِبَادِنَا ۚ وَإِنَّكَ لَتَهْدِي إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ

“Lakini tumeifanya ni nuru tunaongoa kwayo tumtakaye katika waja Wetu; na hakika wewe bila shaka unaongoza kuelekea njia iliyonyooka.”[4]

Mtume pia anaongoza kwa maana ya kwamba anawaelekeza viumbe katika kheri. Kuhusu uongofu kwa njia ya kukubali haki uko mikononi mwa Allaah (´Azza wa Jall):

إِنَّكَ لَا تَهْدِي مَنْ أَحْبَبْتَ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ يَهْدِي مَن يَشَاءُ ۚ وَهُوَ أَعْلَمُ بِالْمُهْتَدِينَ

”Hakika wewe huwezi kumwongoza umpendaye, lakini Allaah humwongoza amtakaye; Naye ndiye mjuzi zaidi ya waongokao.”[5]

Katika Aayah moja Allaah amethibitisha kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni mwenye kuongoza kisha katika Aayah nyingine akakanusha kwamba haongozi. Namna ya kuoanisha Aayah mbili hizo ni kwamba Aayah ya kwanza inahusiana na uongofu wa maelekezo na Aayah ya pili inahusiana na uongofu wa kuafikishwa na kukubali ambao unakuwa mikononi mwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) peke yake.

[1] 28:56

[2] 41:17

[3] 76:2-3

[4] 42:52

[5] 28:56

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 14-15
  • Imechapishwa: 01/07/2021