08. Ahl-us-Sunnah – watu walio kati na kati


Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

3- Hakuna kitu mfano Wake.

MAELEZO

Haya ni kutokana na maneno Yake (Ta´ala):

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖوَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”[1]

وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ

”Wala hakuna yeyote anayefanana na kulingana Naye.”[2]

فَلَا تَجْعَلُوا لِلَّـهِ أَندَادًا وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ

”Hivyo basi msimfanyie Allaah washirika na hali ya kuwa nyinyi mnajua.”[3]

Bi maana wanaolingana Naye na washirika.

هَلْ تَعْلَمُ لَهُ سَمِيًّا

“Je, unamjua yeyote mwenye jina kama Lake?”[4]

Bi maana ambaye anafanana Naye. Hakuna chochote kinacholingana wala kufananishwa na Allaah (´Azza wa Jall). Hakuna kiumbe chochote kinachofanana Naye. Ni lazima kuthibitisha na kuamini yale ambayo Allaah amejithibitishia Mwenyewe na wakati huohuo tusimfananishe wala kumlinganisha na viumbe Wake. Hapa kuna Radd kwa Mushabbihah ambao wanamfananisha Allaah na viumbe Wake. Hawapambanui kati ya Muumbaji na kiumbe. ´Aqiydah hii ni batili.

Walio kinyume nao ni Mu´attwilah. Hawa wamepindukia katika kutakasa mpaka wakafikia kuyakanusha majina na sifa za Allaah alizojithibitishia Mwenyewe. Madai yao ni kwamba wanaepuka kufananisha.

Mapote yote mawili yamekosea. Mu´attwilah wamechupa mipaka katika kutakasa na kukanusha ufanano, Mushabbihah wamechupa mipaka katika kuthibitisha. Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ndio wako kati na kati. Wamemthibitishia Allaah yale aliyojithibitishia Mwenyewe kwa njia inayolingana na utukufu Wake, pasi na kukengeusha wala kupotosha. Wanaamini kwa mujibu wa maneno Yake (Ta´ala):

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖوَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”[5]

Maneno Yake:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye.”

hapa kumekanushwa ufanano. Maneno Yake:

وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”

hapa kumekanushwa ukanushaji. Hii ndio ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Kwa ajili hiyo imesemwa kwamba Mu´attwilah anaabudu kisichokuwepo, Mushabbihah anaabudu sanamu na mpwekeshaji anaabudu Mungu mmoja asiyemuhitajia yeyote lakini ambaye kila mmoja anamuhitajia.

[1] 42:11

[2] 112:04

[3] 02:22

[4] 19:65

[5] 42:11

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 32-33
  • Imechapishwa: 12/06/2019