Ni wajibu pia kukataa kuhukumiwa kwa sheria zilizotungwa na watu. Kwa kuwa ni wajibu kuhukumiana kwa Qur-aan na kutupilia mbali mifumo na sheria zilizotungwa na watu. Amesema (Ta´ala):

فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ

“Mkizozana katika jambo lolote, basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume.” (04:59)

وَمَا اخْتَلَفْتُمْ فِيهِ مِن شَيْءٍ فَحُكْمُهُ إِلَى اللَّـهِ ۚ ذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبِّي

”Na katika lolote lile mlilokhitilafiana, basi hukumu yake ni kwa Allaah. Huyo ndiye Allaah, Mola wangu.” (42:10)

Hakika (Subhaanah) amemhukumu ukafiri, dhuluma na dhambi yule asiyehukumu kwa yale aliyoteremsha Allaah na amemkanushia imani. Ni dalili inayofahamisha kuwa kuhukumu kinyume na yale aliyoteremsha Allaah endapo yule aliyefanya hivo atakuwa amejuzisha hilo, inasilihi zaidi au akaona kuwa ni bora zaidi kuliko hukumu ya Allaah, hii ni kufuru na shirki inayopingana na upwekeshaji na pia inayopingana na shahaadah kuanzia kwenye msingi wake. Iwapo hahalalishi hilo na anaamini kuwa hukumu ya Allaah ndio ambayo ni wajibu kuhukumu kwayo, lakini matamanio ndio yaliyompelekea kwenda kinyume nayo, hii ni kufuru na shirki ndogo inayopingana na maana ya shahaadah na yale inayopelekea.

Kwa hiyo shahaadah ni mfumo mkamilifu. Ni lazima kuidhibiti katika maisha yote ya waislamu, ´ibaadah zao zote na matendo yao yote. Sio tamko linalotamkwa kwa ajili ya kutafuta baraka na katika nyuradi za asubuhi na jioni pasi na kufahamu maana yake, kutendea kazi yale inayopelekea na kupita juu ya mfumo wake. Hivyo ndivyo wanavyofikiria wengi ambao wanalitamka kwa ndimi zao na wanaenda kinyume nalo katika I´tiqaad na vitendo vyao.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqaatunnajia.com
  • Marejeo: Ma´naa laa ilaaha illa Allaah, uk. 27-28
  • Imechapishwa: 23/09/2023