07. Ulazima wa kuijua dini ya Kiislamu kwa dalili na si kibubusa

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

… na ujuzi wa kuijua dini ya Kiislamu kwa dalili.

MAELEZO

Ujuzi wa kuijua dini ya Kiislamu – Ndio dini ya Mtume huyu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Bali ndio dini ya Allaah (´Azza wa Jall) ambayo amewaamrisha kwayo waja Wake na ambayo umeamrishwa kuifuata na wewe inakupasa. Ni lazima kuijua dini hii na Uislamu. Hii ndio dini ya Mitume wote. Kila Mtume dini yake ilikuwa ni Uislamu kwa maana ya kijumla. Kila ambaye alikuwa akimfuata Mtume miongoni mwa Mitume basi huyo ni mwenye kujisalimisha kwa Allaah (´Azza wa Jall), kunyenyekea Kwake na kumpwekesha. Huu ndio Uislamu kwa maana ilionea. Ni dini ya Mitume wote.

Uislamu ni kujisalimisha kwa Allaah kwa kumpwekesha, kunyenyekea Kwake kwa kumtii na kujitakasa kutokamana na shirki na washirikina. Ama Uislamu kwa maana yake maalum ni ule ambao Allaah kamtumiliza kwao Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa sababu baada ya kutumilizwa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuna dini inayokubaliwa isipokuwa dini yake na Uislamu umefupilizika kwa kumfuata yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa msemo mwingine baada ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutumilizwa myahudi au mkristo hawawezi kusema kuwa ni waislamu ilihali hamfuati. Uislamu baada ya kutumilizwa Mtume ni kumfuata yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amesema (Ta´ala):

قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللَّـهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّـهُ

“Sema: “Mkiwa mnampenda Allaah, basi nifuateni mimi. Hivyo atakupendeni Allaah.”[1]

Huu ndio Uislamu kwa maana yake ilioenea na kwa maana yake maalum.

Kwa dalili – Si kwa kufuata kibubusa. Bali ni kwa dalili kutoka katika Qur-aan na kutoka kaitka Sunnah. Hii ndio elimu. Ibn-ul-Qayyim amesema katika “al-Kaafiyah ash-Shaafiyah:

Elimi ni yale aliyosema Allaah na Mtume Wake

Yale waliyosema Maswahabah – wao ndio wajuzi zaidi

Elimu si kuvamia kukhilafiana bila ya kuwa na mazingatio

baina ya Mtume na baina ya rai ya fulani

Hii ndio elimu. Elimu ni ile yenye kunukuliwa kutoka katika Qur-aan na Sunnah. Kuhusu maoni ya wanachuoni ni yenye kusherehesha na kuweka wazi zaidi maneno ya Allaah na maneno ya Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ndani yake au baadhi yake kunaweza kuwa makosa. Dalili sio maneno ya wanachuoni. Dalili ni zile Aayah za Qur-aan na Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Maneno ya wanachuoni ni yenye kufafanua, yenye kuweka wazi zaidi na yenye kubainisha. Si kwamba yenyewe kama yenyewe ni dalili.

Hili ndio suala la kwanza na ndio msingi ambao ameanza nao Shaykh (Rahimahu Allaah). Kwa sababu ndio msingi. Kunaanzwa kwa ´Aqiydah na msingi katika kujifunza, kufundisha na kulingania kwa Allaah (´Azza wa Jall). Ndio asili na ndio msingi.

[1] 03:31

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 22-24
  • Imechapishwa: 23/11/2020